Benki ya Exim Yahitimisha Rasmi Kampeni Yake ya Ugawaji Madawati 1,000 Nchini, Yakabidhi Madawati 150 Dodoma. - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, February 8, 2023

Benki ya Exim Yahitimisha Rasmi Kampeni Yake ya Ugawaji Madawati 1,000 Nchini, Yakabidhi Madawati 150 Dodoma.

 Dodoma: Februari 08, 2023;  Kampeni ya ugawaji wa madawati 1000 iliyokuwa inaendeshwa na benki ya Exim Tanzania katika mikoa mbalimbali hapa nchini imehitimishwa rasmi mkoani Dodoma kwa benki hiyo kukabidhi shehena ya mwisho ya madawati 150 kwa ajili ya Shule ya Msingi Chemba iliyopo wilayani Chemba mkoani Dodoma.

Kampeni hiyo iliyozinduliwa mwishoni mwa mwaka 2021 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa benki hiyo, ilihitimishwa rasmi jana wilayani Chemba na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi Rosemary Senyamule katika hafla fupi ya kukabidhi madawati 150 iliyofanyika kwenye viunga vya shule ya Msingi Chemba na kuhudhuriwa na walimu, wanafunzi, viongozi wa wilaya pamoja na viongozi waandamizi kutoka mkoa wa Dodoma.

Akizungumza kwenye hafla hiyo RC Senyamule aliipongeza Benki ya Exim kwa kampeni hiyo iliyohusisha mikoa minane nchini kwa kuwa ililenga kuunga jitihada za serikali katika kuboresha hali ya utoaji wa elimu bora nchini kwa kukabiliana na changamoto kubwa ya uhaba wa madawati inayoikabili mikoa mbalimbali ukiwemo mkoa huo.

“Niwapongeze sana Benki ya Exim kwa kampeni hii iliyogusa maelfu ya wanafunzi katika mikoa yote ambayo imefikiwa na kampeni hii. Alama mliyoiacha itadumu kwenye mioyo ya watoto hawa kwa muda mrefu na zaidi pia mmeisaidia serikali kuwaboreshea mazingira ya wao kupata elimu…hongereni sana kwa msaada huu wa madawati bora zaidi!’’ Alisema.

Hata hiyo RC Senyamule aliiomba benki hiyo kuangalia namna ya kumalizia changamoto uhaba wa madawati  86 iliyobaki shuleni hapo.

Aidha alitoa wito kwa vijiji na Halmashauri za mkoa huo kuhakikisha zinashiriki kikamilifu kumaliza changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu mkoani humo ikiwemo uhaba wa vyumba vya madarasa, madawati na matundu ya vyoo badala ya kusubiri msaada wa serikali kwa kuwa pia wanawajibu wa kuisaidia serikali kuboresha hali ya upatikanaji wa elimu nchini.

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Chemba Bw Gerald Mongella alisema Wilaya hiyo yenye Shule 110 zikiwemo shule 107 zinazomilikiwa na serikali inakabiliwa na uhaba wa madawati 9,011 huku Shule ya Msingi Chemba pekee ikiwa na uhitaji wa madawati 236, hivyo msaada wa madawati 150 uliotolewa na Benki ya Exim unaifanya shule hiyo ibakiwe na upungufu wa madawati 86.

Hata hivyo Benki ya Exim kupitia Ofisa Mtendaji Mkuu, Jaffari Matundu iliahidi kumaliza upungufu huo uliobakia.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Matundu alisema benki hiyo ilichagua mkoa wa Dodoma kuwa sehemu ya kuhitimisha kampeni hiyo kutokana na heshima ya mkoa huo wenye hadhi ya makao makuu ya serikali sambamba na kuthibitisha dhamira ya benki hiyo katika kusaidiana na serikali kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii hususani kupitia mpango wa benki hiyo wa uwajibikaji kwa jamii unaofahamika kama ‘Exim Cares’

 “Ni heshima tuliyonayo kwa mkoa wa Dodoma ndio iliyosababisha turudi tena mara ya pili kukabidhi madawati haya 150 baada ya kukabidhi madawati 100 hapo awali na hivyo kufanya jumla ya madawati tuliyokabidhi mkoa wa Dodoma pekee yawe 250.’’

“Hatimaye leo tunahitimisha kampeni yetu ya ugawaji wa madawati 1000 iliyofanyika kwa mafanikio makubwa kutokana na ukweli kwamba mikoa yote ambayo tumekabidhi msaada huu ilionyesha kuvutiwa na ubora wa madawati haya yaliyotengenezwa kwa ubora wa hali ya juu ili yaweze kutumika kwa muda mrefu. Kimsingi tulibuni aina ya madawati yanayoendana na mazingira ya shule zetu kwa kuzingatia uimara,’’ alisema.

Aliitaja baadhi ya mikoa ambayo imenufaika na kampeni hiyo kuwa ni pamoja na Dodoma, Mwanza, Lindi, Mbeya, Mtwara, Tabora, Shinyanga na Tanga huku akibainisha kuwa benki hiyo kupitia mpango wake wa ‘Exim Cares’ inajipanga kuja na kampeni nyingine kubwa ikiwa ni muendelezo wa utaratibu wake wa kurudisha sehemu ya faida yake kwa jamii inayoihudumia.

Matundu alitoa wito kwa walimu na wanafunzi walionufaika na msaada huo kutunza madawati hayo ili yaweze kutumika kwa muda mrefu na hivyo kusaidia walengwa wengi zaidi.Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi Rosemary Senyamule (wa kwanza –upande wa kulia) akipokea msaada wa madawati 150 kutoka kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Tanzania Bw Jaffari Matundu (wa kwanza – upande wa kushoto) kwa ajili ya Shule ya Msingi Chemba iliyopo Wilayani Chemba mkoani Dodoma ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa madawati unaoikabili shule hiyo. Makabidhiano hayo yalifanyika jana kwenye viunga vya shule hiyo. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Chemba Bw Gerald Mongella  (wa tatu kulia) pamoja na viongozi waandamizi wa wilaya hiyo pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo.Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi Rosemary Senyamule Bw (katikati walioketi) sambamba na Mkuu wa Wilaya ya Chemba Bw Gerald Mongella  (Kulia walioketi) na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Tanzania Bw Jaffari Matundu (kushoto walioketi) wakiwa wameketi kwenye moja ya madawati 150 yaliyotolewa na benki ya Exim Tanzania kwa ajili ya Shule ya Msingi Chemba iliyopo Wilayani Chemba mkoani Dodoma ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa madawati unaoikabili shule hiyo. Wengine ni viongozi waandamizi wa Chama na serikali wilayani humo pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Chemba Bw Gerald Mongella akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi Rosemary Senyamule Bw (wa tatu kushoto) akisalimiana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Tanzania Bw Jaffari Matundu) wakati Mkuu wa Mkoa huyo alipowasili kwenye viunga vya Shule ya Msingi Chemba iliyopo Wilayani Chemba mkoani Dodoma ili kupokea msaada wa madawati 150 yaliyotolewa na benki ya Exim Tanzania kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya uhaba wa madawati unaoikabili shule hiyo. Wengine ni viongozi waandamizi wa Chama na serikali wilayani humo pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo.

Asante sana Benki ya Exim! Ndivyo wanavyosikika wakisema wanafunzi wa Shule ya Msingi Chemba iliyopo Wilayani Chemba mkoani Dodoma mara baada ya kupokea msaada wa madawati 150 yaliyotolewa na Benki ya Exim Tanzania kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya uhaba wa madawati unaoikabili shule hiyo. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad