Zungu agawa Mitungi ya gesi 150 kwa Baba na Mama lishe Kisutu - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, January 18, 2023

Zungu agawa Mitungi ya gesi 150 kwa Baba na Mama lishe Kisutu

 

Na Humphrey shao Michuzi Tv 

Mbunge wa Ilala, Naibu Spika,  Mussa Zungu, amekabidhi msaada wa mitungi 150 kwa mama na baba lishe wa Soko la  Kisutu  Stendi ya Zamani.

Hatua hiyo ni kuunga mkono maagizo ya Rais Dk. Samia  Suluhu Hassan,  ya kuitaka jamii kutumia nishati mbadala ili kulinda mazingira na kuepuka mabadiliko ya tabia ya nchi.

Akikabidhi mitungi hiyo iliyotolewa na Kampuni ya Taifa Gas, Dar es Salaam, Zungu, amesema serikali chini ya Rais Dk. Samia, inathamini wananchi wake na itasimamia kikamilifu kuhakikisha wanatumia nishati hiyo mbadala na kuokoa misitu.

“Kwa kutambua kauli hiyo ya Rais Dk. Samia, niliona umihimu wa kuwatafuta Taifa Gas ambao  walikubali kuwapa  mama na baba lishe mitungi hii 150 bure,” amesema Zungu.

Ameeleza, matumizi ya gesi hiyo yatasaidia  ufanisi kwa baba na mama lishe hao, kulinda mazingira na kujiepusha na matumizi ya  ambapo Dar es Salaam ndiyo jiji linalotumia kwa kiasi kikubwa  matumizi ya mkaa.

Ameishukuru Kampuni ya  Taifa Gas kwa kutoa mitungi hiyo bure na kuwaomba mama  na babalishe hao, kutumia  bidhaa za kampuni hiyo ya wazawa.

Akikabidhi mitungi hiyo ya gesi kwa mamalishe na babalishe hao, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wirabuzu Ludigija, amewataka wafanyabiashara  kufanya shughuli zao katika maeneo rasmi na kufikiwa na fursa muhimu kama hizo.

Amesema, awali  mama na baba lishe hao ilikuwa ni vigumu kuwafikia kutokana na kufanya biashara kiholela.

“Lakini leo mko hapa Kisutu Stand ya Zamani mmepata mitungi ya gesi bure, hii ndiyo faida ya kufanya biashara katika maeneo rasmi. Mtafikiwa na fursa nyingi zikiwezo za mikopo,”alisema Ludigija.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, Said Sidde, alisema matumizi ya gesi  pia yatasaidia kulinda afya za mama  na baba lishe hao ambao wengi wanathirika na moshi wa mkaa na kunio.

Diwani wa Kata ya Kisutu, Kheri Kessy, ameshauri serikali kutenga maeneo maalumu ambayo utawekwa utaratibu wa kuto kutumika kwa mkaa na kuni hasa katikati ya jiji.

Meneja Uhusiano wa  Taifa Gas, Angel Mwita, alisema wataendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kutumia nishati mbadala ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais Dk. Samia.

Mwenyekiti wa babalishe na  mamalishe  Kisutu Stendi ya Zamani,  Pendo Maiko, alimshukuru Rais Dk. Samia, Mbunge Zungu, Taifa Gas na serikali kwa ujumla kwa kuwajali na kuwawezesha mitungi hiyo.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mussa Azzan Zungu akikabidhi mtungi wa  Taifa gesi kwa mmoja wa Mama lishe wa soko la Kisutu Dar es Salaam.
Baadhi Mitungi watakayokabidhiwa Baba na Mama lishe wa soko la kisutu kutoka Taifa gesi. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad