Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
MKURUGENZI Mtendaji wa Watumishi Housing Investmet Dk.Fredy Msemwa amesema wawekezaji 3,800 wamejiandikisha kuwekeza kwenye Mfuko wa FAIDA FUND na hivyo kufanikiwa kukusanya Sh.bilioni 13.5 katika kipindi kifupi.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Dk.Msemwa amesema pamoja na mambo mengine kiwango cha uwekezaji katika mfuko huo kimeendelea kukua siku hadi siku, hivyo kuongeza mafanikio makubwa ya mfuko huo.
“Mpaka tunafunga mauzo ya mwanzo Desemba 31,2022 tumefanikiwa kukusanya kiwango kikubwa na hivyo kuvuka malengo ambayo tulikuwa tumeyaweka.Mafanikio haya yanatokana na watu wengi kutumia teknolojia rahisi na matumizi ya simu, mitandao ya kompyuta ambayo imesaidia kuufikia mfuko huo kwa wepesi na hivyo kufanikisha makusanyo hayo.”
Ameongeza kwamba watu wengi wameufikia mfuko wa FAIDA FUND na kufanya uwekezaji ambao umewezesha kukusanywa fedha Sh.bilioni 12.95 hadi kufikia Desemba 31,2022 na kwa sasa kiasi hicho kimeongezeka mpaka kufika Januari 11, 2023 wamekusanya Sh.bilioni 13.5 na kuongeza kiasi cha fedha kimeendelea kukua siku hadi siku.
Pia thamani ya kipande awali ilikuwa 100 na sasa imeongezeka kwa shilingi 100.54 huku akifafanua hayo yamewezekana kutokana na matumizi ya mfumo rahisi wa malipo Serikali ambao umewaletea faida kubwa ikiwemo ya utambuzi wa miamala kufanyika kwa kasi kubwa.
Pia amesema faida nyingine mfuko huo unawezesha fedha zinazowekezwa kuwa salama ambapo tayari fedha hizo zimeingizwa kwenye uwekezaji wa dhamana za Serikali za muda mrefu mwaka 2022/2025. “Wawekezaji pia wamepata faida katika Mfuko huo kutokana na gharama zake kuwa ndogo kwani wanalipa kidogo kwa ajili ya mtandao na zinazobaki zinaingizwa serikalini.”
Sehemu ya watumishi wa Watumishi Housing Investmet wakiwa kwenye Mkutano huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment