BODI MPYA SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA LATEMBELEA MIRADI YAKE MIKUBWA JIJINI ARUSHA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, January 16, 2023

BODI MPYA SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA LATEMBELEA MIRADI YAKE MIKUBWA JIJINI ARUSHA

 

 Na Pamela Mollel - Arusha 

Bodi mpya ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) imefanya ziara ya kutembelea miradi yake mikubwa katika mkoa wa Arusha kwa lengo la kuona maendeleo yake kwa ujumla.

Akizungumza na vyombo  vya habari katika ziara hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Bw. Nehemiah Mchechu alisema Bodi mpya iliyoteuliwa hivi karibuni imepata fursa ya kutembelea miradi ya shirika hilo iliyopo katika eneo la Useriver na Mateves

Alisema Arusha inaongoza kuwa na miradi mikubwa ya shirika ikiwemo mradi wa Safari City ambao ni kitovu cha mji unaojitegemea wenye jumla ya ekari 587

Aidha, aliongeza kuwa kinachofurahisha katika mradi huu uliopo eneo la Burka Mateves ndani ya jiji la  Arusha ni namna unavyoendelea kujengeka.

"Mpaka sasa Taasisi ambazo zinaendelea na ujenzi ni Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (AUWSA)ambao wamejenga jengo la Makao Makuu ya Ofisi zao, Baraza la Taifa la Elimu ya ufundi na ufundi stadi (NACTVE)

Aliongeza kuwa Taasisi nyingine zilizonunua maeneo ni pamoja na LATRA,OSHA,FIRE,POLICE pamoja na EWURA 

Mbali na kuwepo kwa mradi wa viwanja Mkurugenzi huyo alisema mpango wao kwa sasa ni kuangalia baadhi ya nyumba za zamani zinazomilikiwa na Shirika ambazo zitajengwa upya ili kuwezesha watu wengi kumiliki nyumba.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt.Sophia Kongela alisema mikakati ya Bodi ni kutembelea miradi ya shirika  na kuweka mpango mkakati wa kufufua baadhi ya miradi iliyokufa 

"Tumetembelea miradi yetu na kuona maendeleo yake kwa ujumla ili kuchochea uuzwaji wa viwanja. alisema Kongela

Aidha, mwenyekiti wa Bodi pamoja na Bodi ya Shirika  wameipongeza wkala wa barabara za miji na vijiji  (TARURA) kwa kuanza  ujenzi wa daraja linalounganisha eneo la mradi na barabara ya mzunguko ya Afrika mashariki.

Mwenyekiti alisema kuwa kitendo cha TARURA kuanza ujenzi wa daraja hilo muhimu kutawaezesha wananchi waliowekeza kwenye mradi  huo kuendeleza maeneo yao kwa urahisi zaidi.

Kwa upande wake Meneja wa Mkoa wa Arusha Bennet Masika wakati akitoa taarifa fupi kwa bodi alisema kuwa mradi wa safari city una jumla ya viwanja 1913 kwa ajili ya uendelezaji wa nyumba za makazi,majengo ya biashara,huduma za jamii kama Shule,Vyuo,Hospitali,Sehemu za ibada na sehemu za kimichezo

Alisema kuwa katika viwanja hivyo Shirika limetenga Viwanja 1601 kwa ajili ya kuviuza sawa na asilimia 84 na viwanja 313 vimehifadhiwa kwa ajili ya uendelezaji wa baadae.

"Kwa kipindi cha miaka sita kuanzia Juni 2016 hadi sasa shirika limeweza kuuza jumla ya viwanja 1022 sawa na asilimia 63.8 ya viwanja vyote

Aliwataka wadau mbalimbali kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwa bado maeneo yapo na bei ya kiwanja kwa mita moja ya mraba ni shilingi 21,000 kwa maeneo ya makazi na biashara mita moja ya mraba ni TZS 27,000. Akasema kuwa  maeneo ya makazi mteja atalipia kwa miezi 36 makazi na biashara miezi 60.  

Pamoja na mradi wa safari City na Usariver, Bodi hiyo iliweza kutembelea miradi ya ubia kati ya NHC na wawekezaji binafsi ambayo imesimama kwa muda mrefu na wameipongeza  Menejimenti kwa kuanza  kuchukuwa hatua za miradi hiyo kuendelezwa na Shirika lenyewe.

Mwenyekiti wa Bodi mpya ya  Shirika la nyumba la Taifa NHC Dkt Sophia Kongela akizungumza na vyombo vya habari mara  baada ya kumaliza ziara ya kutembelea miradi mikubwa ya shirika hilo katika eneo la mradi wa SafariCity jijini Arusha
Meneja wa NHC Mkoa wa Arusha Bennet Masika kushoto akionesha mchoro wa ramani inayoonesha Mradi wa SafariCity kulia  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Nehemiah Mchechu katika eneo la Mateves jijini ArushaMkurugenzi Mkuu Shirika la Nyumba la Taifa Nehemiah Mchechu akizungumza na vyombo vya habari juu ya ziara hiyo


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad