VIJIJI SITA WILAYANI MBALALI VYAPELEKEWA MRADI MKUBWA WA MAJI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, December 29, 2022

VIJIJI SITA WILAYANI MBALALI VYAPELEKEWA MRADI MKUBWA WA MAJI

 

Na Muhidin Amri Mbalali

ZAIDI ya vijiji sita katika wilaya Mbalali mkoani Mbeya,vinatarajiwa kunufaika na huduma ya maji kufuatia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijiji(Ruwasa),kuanza kutekeleza mradi wa maji Ruduga-Mawindi utakaohudumia  takribani watu 18,341 wa vijiji hivyo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo,mara baada ya kutembelea chombo cha watoa huduma ya maji ngazi ya jamii (CBWSO)cha Luduga- Mawindi wilayani humo.

Kivegalo amevitaja vijiji  vitakavyonufaika kupitia mradi huo ni Ipwani,Manienga,Matemela,Itipingi,Mkandami na Kangaga ambacho wakazi wake wameanza kupata huduma ya maji katika awamu ya kwanza ya mradi huo.

“tangu mwezi wa sita mwaka jana wakazi wa Kangaga wameanza kupata huduma ya maji safi na salama,na kwa upande wa serikali  kupitia Ruwasa imefikia hatua nzuri katika kuhakikisha vijiji vitano vilivyobaki vinapata maji haraka iwezekanavyo”alisema  Mhandisi Kivegalo.


Kivegalo,amekipongeza chombo cha watoa huduma ya maji ngazi ya jamii cha Luduga-Mawindi kwa kuonyesha uwezo katika usimamizi na uendeshaji wa mradi huo.

Alisema,malengo ya chombo hicho kukusanya Sh.milioni 1 kwa mwezi,lakini  kwa sasa wanakusanya Sh.800,000, jambo ambalo linaloleta matumaini  makubwa kwa Ruwasa.


Mhandisi Kivegalo,ameipongeza kampuni ya GNMS Contructors Co. Ltd ya Iringa inayotekeleza mradi huo kwa kuonyesha uwezo na jitihada kubwa katika utekelezaji wake na hivyo kuanza kuleta manufaa na matumaini makubwa kwa wananchi.

Kwa upande wake Msimamizi wa CBWSO hiyo Frank Sanga alisema, katika kipindi cha uendeshaji wa skimu ya maji wamefanikiwa kuwafungia dira za maji wateja 200.

Alitaja mafanikio mengine ni ufuatiliaji wa matengenezo ya mara kwa mara katika bomba kuu,huku akieleza mipango waliyonayo ikiwamo kuongeza vitendea kazi na idadi ya wateja kutoka 200 hadi 600.

Sanga alieleza kuwa,wastani wa mahitaji ya maji kwa wakazi wote katika eneo la huduma la CBWSO ni mita za ujazo 13,824 kwa mwezi,wakati uzalishaji wa chombo ni mita za ujazo 90,720 hivyo hakuna upungufu wa huduma ya maji.

Aidha alisema,upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi waishio katika eneo linalohudumiwa na chombo(CBWSO)ni wastani wa asilimia 17 ambapo wakazi wapatao 3,066 kati ya wakazi wote 18,431 wanapata huduma ya maji safi na salama.

Naye mwakilishi wa wanawake wa kijiji cha Kangaga Flora Kweya,ameishukuru wizara ya  maji kupitia Ruwasa kwa kuwapelekea mradi huo ambao utakapo kamilika utawezesha kumaliza  kero ya maji safi na salama iliyokuwepo kwa muda mrefu.

Hata hivyo,ameiomba Ruwasa kupeleka miundombinu ya mradi huo kwenye maeneo mengine ambayo hadi sasa hayako kwenye mpango wa kupata huduma ya maji ili wananchi wa maeneo hayo nao waweze kupata  huduma hiyo.Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Mhandisi Clement Kivegalo kulia,akizungumza na viongozi wa chombo cha watoa huduma ya maji ngazi ya jamii(CBWSO)cha Luduga-Mawindi wilaya ya Mbalali mkoani Mbeya wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi ya maji mkoani humo.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad