BIBI TITI ALIHAMASISHA KISWAHILI KUTUMIKA BUNGENI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, December 15, 2022

BIBI TITI ALIHAMASISHA KISWAHILI KUTUMIKA BUNGENI

 

Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

Wakati Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, mkoa wa Pwani ikiandaa tamasha la kumbukizi ya marehemu Bibi Titi Mohammed katika Wilaya hiyo, jamii imeaswa kuenzi Waasisi wa taifa la Tanzania ambao walikuwa mstari wa mbele kwenye kupigania maslahi ya taifa hilo.

Akizungumza kuelekea tamasha hilo, Mbunge wa Jimbo la Rufiji ambaye pia ni Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mhe. Mohammed Mchengerwa amesema ili tuweze kupiga hatua katika maendeleo, vizazi vya sasa vinapaswa kujifunza mambo mbalimbali yaliyofanywa na Waasisi wa taifa hili katika kuhimiza maendeleo.

“Tunamkumbuka marehemu Bibi Titi tangu afariki dunia, lakini tunaona jinsi alivyokuwa mstari wa mbele sanjari na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kupigania maslahi ya taifa. Marehemu Bibi Titi alikuwa Kiongozi shupavu na alikuwa anatamani kila mmoja kwenye taifa hili kuwa na uhuru”, amesema Mhe. Mchengerwa.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema marehemu Bibi Titi alihamasisha Wanawake wengi waingie kwenye masuala ya Siasa na kuwa mstari katika kupigania haki na usawa katika masuala hayo kwenye Jamii kama alivyofanya nchini Kenya kutoa hamasa ya ukombozi kwa Wanawake kusaidia kukomboa taifa hilo jirani.

“Nakumbuka kuna neno alisema na kumhamasisha Mwalimu Nyerere kuhimiza Bunge la Tanzania kuzungumza lugha ya Kiswahili, alikuwa anataka  Barabara fulani iwekwe Taa, hapo ndipo zilipoanza harakati za kuzungumzwa Kiswahili bungeni”, ameeleza Mhe. Mchengerwa.

Mhe. Mchengerwa amesema: “Hata barabara ya ‘Kilwa Road’ ilijengwa chini ya uongozi wa Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi ambaye alisema ujenzi wake ni mahsusi kumuenzi marehemu Bibi Mohammed ambaye alikuwa mmoja wa Waasisi wa taifa la Tanzania”.

Hata hivyo, Mhe. Mchengerwa ametoa wito kuendelea kuwaenzi Waasisi wa taifa la Tanzania ambao walikuwa mstari wa mbele katika kupigania maslahi ya nchi, ameviasa vizazi vijavyo kukumbushwa historia za Waasisi hao ikiwa sanjari na kuandikwa historia zao sehemu mbalimbali.

Kumbukizi ya marehemu Bibi Titi Mohammed inafanyika katika viwanja vya Ujamaa, Rufiji mkoani Pwani, na itahudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wazee wa zamani, Maprofesa, Madaktari na Wananchi mbalimbali pamoja na Mtoto wa Marehemu, Bi. Halima.

Mbunge wa Jimbo la Rufiji, Mhe. Mohammed Mchengerwa (wa kushoto) akisalimiana na baadhi ya Wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya kuwasili kwenye Ofisi yake binafsi, kuelekea katika tamasha la Kumbukizi ya marehemu Bibi Titi Mohammed.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad