HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 2, 2022

RAIS SAMIA KUFANYA ZIARA NCHINI CHINA

 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya Kitaifa nchini China kuanzia tarehe 2 hadi 4 Novemba kufuatia mwaliko kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping.

Ziara hiyo ni ya kwanza kufanywa na kiongozi wa juu kutoka bara la Afrika tangu Rais Xi Jinping achaguliwe tena na Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China kuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho kwa muhula wa tatu.

Vilevile, ziara hiyo itakuwa miongoni mwa ziara za mwanzo za viongozi wa kitaifa kutembelea nchini China tangu utokee mlipuko wa UVIKO-19 mwezi Desemba 2019.

Rais Samia atapokelewa rasmi tarehe 3 katika ukumbi wa Great Hall of the People ambapo atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais wa China, Xi Jinping na kushuhudia utiaji saini wa mikataba mbalimbali.

Mbali na kukutana na Xi Xinping, Rais Samia anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu wa China Li Keqiang pamoja na Spika wa Bunge la nchi hiyo Li Zhanshu.

Ziara ya Rais Samia inafanyika katika kipindi ambacho Tanzania na China zimeadhimisha miaka 58 ya mahusiano ya kidiplomasia. Viongozi hao wawili wanatarajia kuzungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano katika nyanja za siasa, uchumi, utamaduni na ushirikiano wa kimataifa.
Zuhura Yunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad