Na Said Mwishehe, Michuzi TV
UNITED Bank for Africa(UBA) imesema itaendelea na mkakati wake wa kuwahamasisha watanzania wa kada mbalimbali kujiunga na benki hiyo ili kupata fursa ya mkopo wenye masharti nafuu unaofahamika kama Mkopo Kitonga ambapo Sh.bilioni 13 zimetengwa kwa ajili ya kutoa mkopo huo.
Akizungumza kwenye tukio la menejimenti ya juu ya benki hiyo pamoja na maofisa mbalimbali kukutana na wateja kufanya mazungumzo yenye lengo la kubadilishana uzoefu, Meneja wa Matawi wa UBA Tanzania Mwinyimkuu Ngalima amesema benki hiyo imetoa fursa ya mikopo kwa ajili ya wajasiriamali wa aina zote pamoja na wananchi kwa ujumla.
“UBA tunazo huduma nyingi na sasa hivi tunahuduma yetu kubwa sana kwa ajili ya wajasiriamali ya Mkopo Kitonga , ni mkopo ambao unaanzia Sh.milioni sita hadi Sh.milioni 315.Tunatoa mkopo kwa muda mfupi wa mwaka mmoja kwa kilipa kila mwezi lakini tunao mkopo wa muda mrefu ambao mkopaji anachukua kwa mfumo wa Over draft,”amesema.
Amefafanua mkopo huo umewekwa rahisi kwani mtu anaweza kuchukua mkopo kwa kuweka dhamana ya vifaa mbalimbali vya uzalishaji kama vile matrekta, jenereta pamoja na makatapila.Pia kwa wajasirimali nao wanaweza kuweka kitu chochote kama dhamana ya mkopo aliochukua.“Kwa hiyo ni mkopo unaolenga makundi yote ya wajasiriamali , hata washereheshaji (MC) wanayo nafasi ya kukopa kwenye benki yetu,riba yetu ni nafuu.”
Aidha Ngalima amesema kigezo kikubwa wanachoangalia ni mteja aweze kufanya biashara na wao angalau kipindi cha miezi mitatu na kwamba huduma ya Mkopo Kitonga ilizinduliwa Septemba 30 na wakaaanza Oktoba , hivyo kwa sasa wako katika kipindi cha uangalizi kwa wale wateja wao ambao walianza Septemba.“Bajeti ambayo tumeweka kwenye eneo hili ni Sh.bilioni 13 na lengo letu ni kuona wajasiriamali wengi wanachangamkia hii fursa.”
Kuhusu kufungua akaunti kwenye benki hiyo, amesema wamerahisisha kwani wanayo program maalum ya LEO ambayo mtu anaweza kufungua akaunti, aidha akiwa kwenye platform yake ya Whatsapp au Facebook Messenger.
“Mteja akianza kwa kuandika neno Hi basi anaendelea na tararibu za kufungua akaunti yake na kuanza kutumia wakati huo huo. Ni huduma nyepesi na tunataka mtu akiwa hata kwenye Instagram au Google awe na uwezo wa kufungua akaunti ya UBA.”
Akizungumzia matawi ya benki hiyo amesema wameendeelea kuongeza matawi katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi na hivi karibuni wanatarajia kuzindua tawi mkoani Arusha na baadae watakwenda mikoa mingine pamoja na Zanzibar.
“Dar es Salaam tunayo matawi manne na nje ya Dar es Salaam tunayo matawi manne.Sasa hivi tunakaribia kufungua tawi letu Arusha.Faida ya benki yetu tunapatikana nchi 24 ndani ya Afrika kwa hiyo huduma unayoipata hapa unaweza kuipata katika nchi yoyote utakayokwenda maana tutaendelea kukutambua wewe ni mwana UBA,”amesema Ngalima.
Ametumia nafasi hiyo kueleza UBA inawajali watu wa hali zote lakini hata ufunguaji wa akaunti unagharama nafuu ukilinganisha na benki nyingine huku akisisitiza kufungua akaunti UBA hakuna gharama yoyote.
“Tunaendelea kupanua wigo wa utoaji huduma, tunaendelea kuongeza mawakala kwa ajili ya benki yetu kwa ajili ya kupata huduma ya benki hiyo sehemu yoyote.Tuko nchini Tanzania tangu mwaka 2009 na tunandelea kukua kwa mfano sasa hivi tuko Dodoma , Mwanza na Rufiji.Sasa hivi tunataka kwenda maeneo mengine.”

Mkurugenzi Mkuu wa UBA Group (United Bank for Africa) (katikati), ndg. Oliver Alawuba, akisalimiana na mmoja wa wateja wa benki hiyo, katika hafla ya chakula cha usiku. Wa kwanza kulia, ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya UBA Tanzania, Gbenga Makinde.


No comments:
Post a Comment