HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, June 19, 2020

MABULA AFURAHIA AFURAHIA MRADI WA NHC

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia moja ya ramani zilizohifadhiwa kwenye ofisi mpya ya ardhi ya mkoa wa Arusha wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa huo jana.
 Taswira ya Jengo la Ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) lilipo katika Shamba la Miti la Kilimanjaro Kaskazini wilaya ya Rombo mkoa wa Kilimanjaro.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa wilaya ya Rombo, watendaji wa sekta ya ardhi katika ofisi ya ardhi ya mkoa wa Kilimanjaro pamoja na watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) alipotembelea mradi wa ujenzi wa jengo la TFS katika shamba la Miti la Kilimanjaro Kaskazini lililopo wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akizungumza alipotembelea mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) katika shamba la Miti la Kilimanjaro Kaskazini lililopo wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.
 Mkuu wa wilaya ya Rombo mkoa wa Kilimanjaro Agnes Hokororo akizungumza wakati Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipotembelea mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) katika shamba la Miti la Kilimanjaro Kaskazini lililopo wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.

Na Munir Shemweta, WANMM KILIMANJARO
NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kuweza kukamilisha ujenzi wa miradi ya jengo la ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Hai lililopo Bomang’ombe na ofisi pamoja na nyumba za Watumishi wa Wakala wa huduma za Misitu (TFS ) zilizopo kwenye shamba la Miti la Kilimanjaro Kaskazini maarufu Rongai wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.

Dkt Mabula alitoa pongezi hizo jana alipotembelea miradi ya ujenzi wa majengo ya ofisi na nyumba hizo akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa pamoja na kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi kwenye mkoa wa Kilimanjaro.

Alisema, Shirika la Nyumba la Taifa kwa sasa linapaswa kupongezwa kutokana na juhudi kubwa inayofanya katika kutekeleza miradi yake ya ujenzi wa majengo ya ofisi na nyumba katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Hai na zile za Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) ambapo alieleza kuwa ofisi hizo zimejemgwa katika viwango vinavyotakiwa.

Naibu Waziri Mabula alisema, hivi sasa NHC imeaminiwa na Serikali kwa kupatiwa miradi mbalimbali ya ujenzi ikiwemo ujenzi wa majengo ya ofisi na nyumba za Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (TFS) nchi nzima sambamba na ujenzi wa hospitali za Rufaa za mikoa ya Mara na Mtwara.

‘’Tunapaswa kumshukuru Mhe Rais John Pombe Magufuli kwa kuamua kutoa fedha za ujenzi wa majengo ya ofisi na nyumba za Wakala wa huduma za Misitu kwenye mikoa mbalimbali, Raisi anataka watumishi wafanye kazi katika mazingira mazuri’’ alisema Dkt Mabula.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri, Shirika hilo la Nyumba la Taifa kwa sasa imeaminiwa na serikali hivyo linapaswa kuhakikisha miradi yote inayokabidhiwa inakamilika kwa wakati sambamba na ujenzi wake kukidhi viwango na ubora unaotakiwa ili kujenga imani kwa wananchi na serikali kwa ujumla.

Akielezea utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi na nyumba za watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Kilimanjaro Juma Kiaramba alisema mradi huo ambao mpaka sasa umetumia TZSh 639,494,580.18 ulianza Septemba mwaka jana na tayari kazi za ndani kwa majengo yote 4 umekamilika kwa asilimia mia moja na kusisitiza kuwa Shirika lake linatarajia kukamilisha zilizobaki za nje katika kipindi cha muda mfupi ujao.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Shamba la Miti la Kilimanjaro Kaskazini Joel Naasi alimueleza Naibu Waziri Mabula kuwa TFS kupitia shamba la Miti la Kilimanjaro Kaskazini Wakala umefanikiwa kukusanya maduhuli kiasi cha fedha 3,688,849,489.68 hadi kufikia Mei mwaka huu wa fedha.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezitaka ofisi za halmashauri na wilaya nchini kuzitumia ofisi za ardhi za mikoa zilizoanzishwa hivi karibuni katika kushughulikia masuala ya ardhi ili kuleta ufanisi katika sekta ya ardhi.

Akizungumza na Watendaji wa sekta ya ardhi wa ofisi ya ardhi mkoa wa Arusha pamoja na wale wa halmashauri za mkoa huo ikiwemo jiji la Arusha, Dkt Mabula alisema uamuzi wa kuanzisha ofsi za ardhi za mikoa ni kutaka kuondoa kero za ardhi sambamba na kusogeza huduma za sekta hiyo karibu na wananchi.

Alisema, ofisi za wilaya na halmashauri katika mikoa zinapaswa kuwatumia wataalamu waliopo ofisi za ardhi za mikoa katika kushughulikia masuala ya upimaji, uthamini na mipango miji ili kuwa na miji iliyopangika na wakati huo wananchi kumilikishwa maeneo yao.


Akielezea suala la upungufu wa watumishi wa sekta ya ardhi kwa baadhi ya halmashauri, Naibu Waziri Mabula alisema kwa sasa wizara yake iko katika mchakato wa kuwapanga upya watumishi wa sekta hiyo baada ya kukamilika zoezi la kupeleka watumishi wa ofisi za ardhi za katika ofisi za mikoa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad