HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, February 19, 2019

TIMU YA MAKATIBU WAKUU YATEMBELEA VIJIJI NA VITONGOJI VILIVYOMO NDANI YA HIFADHI

Timu ya Makatibu wakuu wa Wizara za kisekta zinazohusika na urasimishaji vijiji na vitongoji vilivyoanzishwa na kusajiliwa ndani ya Hifadhi imeanza ziara yake ya kutembelea vijiji na vitongoji  vilivyomo ndani ya maeneo ya Hifadhi ili kujionea na kutoa ushauri wa namna bora ya kurasimisha vijiji hivyo bila kuathiri uhifadhi endelevu. Wizara hizo ni Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Maji, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Ofisi ya Rais Tamisemi.

Hatua hii inafuatia agizo lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa Wizara za Kisekta kuangalia namna bora ya kurasimisha vijiji na vitongoji vilivyoanzishwa na kusajiliwa ndani ya Hifadhi. Kufuatia agizo lililotolewa na Rais Magufuli, Katibu Mkuu Kiongozi aliwaagiza Makatibu wakuu wa Wizara za Kisekta, kuunda kamati kwa ajili ya kuchambua kwa kina maeneo ya vijiji na vitongoji vilivyomo ndani ya Hifadhi ikiwa ni katika kutekeleza agizo la Rais Magufuli.

Akizungumza na Waandishi wa Habari walipotembelea Pori la Akiba la Swagaswaga, Mwenyekiti wa Timu hiyo ya Makatibu Wakuu, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Makazi Bibi Dorothy Mwanyika, amesema mapendekezo yatakayotolewa na timu ya Makatibu Wakuu hao, yatasaidia katika utekelezaji mzuri wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuhusu urasimishaji wa vijiji hivyo na vitomgoji vilivyomo ndani ya Hifadhi huku suala zima la uhifadhi endelevu likizingatiwa.

Bibi Dorothy amesema, ziara hii ni ya kwanza ikifuatiwa na ziara katika mkoa wa Arusha na Njombe. Amesema, timu ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta wanaendelea na Ziara kama hiyo katika mikoa mingine na tayari wametembelea mikoa ya Morogoro na Kigoma. Wakiwa katika Pori la Akiba la Swagaswaga, timu hiyo ya Makatibu Wakuu ilijionea kuwa baadhi ya vijiji viko katika maeneo ya vyanzo vya maji na mapito ya wanyama. 

Akifafanua zaidi kuhusu umuhimu wa ziara hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda amewaeleza Waandishi wa Habari kuwa, ziara katika vijiji hivyo na vitongaji vilivyoko ndani ya Hifadhi zitaiwezesha timu hiyo ya makatibu wakuu kujionea hali halisi ya vijiji hivyo ikiwemo mipaka, hali halisi ya Hifadhi kwa sasa na maeneo muhimu ya Hifadhi ambayo yanapaswa kulindwa kwa faida ya nchi na hivyo kuwa kwenye nafasi nzuri ya kutoa ushauri utakaosaidia katika utekelezaji wa agizo la  Rais  Dkt. John Pombe Magufuli      
Akizungumza na timu hiyo ya Makatibu Wakuu wa Wizara saba za Kisekta zinazohusika na urasimishaji vijiji na vitongoji vilivyoanzishwa na kusajiliwa ndani ya Hifadhi, Mkuu wa Wilaya ya Chemba Bwana Simon Odunga ameishauri kamati hiyo kuangalia namna bora ya kuhifadhi maeneo oevu na vyanzo vya maji vilivyoko kwenye Pori la Akiba la Swagaswaga kwani vyanzo hivyo ndivyo vinavyopeleka maji kwenye mto Mtera.

Bwana Odunga ameongeza kuwa tunahitaji kulinda vyanzo vya maji ili kuepusha nchi kuwa jangwa na kuwa, pamoja na kuangalia mahitaji ya wananchi wetu kama alivyoelekeza Rais lakini  tukumbuke Rais alisisitiza kuwa bado tunahitaji kuhifadhi.  Odunga ameongeza kuwa tunahitaji kuangalia suala zima la Uhifadhi wa Maliasili zetu kwa manufaa ya Taifa na vizazi vijavyo huku tukizingatia mahitaji ya wananchi kwa maendeleo endelevu. Awali, akizungumza kuhusu umuhimu wa Pori la Akiba la Swagaswaga kiuchumi na kiikolojia, Meneja wa Pori la Swagaswaga Bwana Alex Choya amesema, eneo hili ni muhimu kwa mazalia ( breeding Site) ya wanyamapori walio hatarini kutoweka kama vile Korongo na Tandala wadogo na malisho (Feeding) na Mtawanyiko ( Dispersal area) kwa wanyamapori.

Bwana Choya ameongeza kuwa, Pori hili ni kiungo muhimu kiikolojia kati ya Hifadhi ya Tarangire (upande wa Kaskazini), Msitu wa Hifadhi wa Jamii Mgori na Mapori ya Akiba ya Rungwa/ Kizigo/ Muhesi ( upande wa kusini magharibi) mwa Tanzania. Ameongeza kuwa Pori hili linachangia mapato asilimia 25 ya ada ya wanyamapori wanaowindwa kupitia uwindaji wa Kitalii kwa Halmashauri za Wilaya za Kondoa na Chemba. Meneja huyo wa Swagaswaga, amesisitiza kuwa Pori la Akiba Swagaswaga ni chanzo muhimu cha mto Bubu ambao hutiririsha maji yake kuelekea Bwawa la ufuaji umeme la Mtera. 

Pori la Akiba la Swagaswaga lina Rasilimali mbali mbali zikiwemo za Wanyamapori, misitu na uoto wa asili uliotawaliwa na miti ya miombo, mimea ya aina mbalimbali, vichaka vifupi pamoja na miinuko na milima midogo yenye miamba, majabali na mapango makubwa. Wanyamapori waliopo katika Pori la Akiba Swagaswaga ni pamoja na Tandala (Greater and Lesser Kudu), Tembo, Korongo (Roan antelope), Nyati, Pundamilia, Swalapala, Pofu, Chui, Twiga, Simba, Kongoni, Pongo, Ngiri, Nguruwe pori, Nsya, Nyani, Tumbili na Mbuzi mawe.

Pori hili pia, lina utajiri mkubwa wa michoro ya miambani (Rock Art Paintings) ambayo ni kivutio cha Utalii na kuna jumla ya maeneo hamsini na mbili (52) yenye michoro ya miambani (Rock Painting Sites). Aidha, Pori la Akiba Swagaswaga pia lina umuhimu wake kihistoria kwani lina njia iliyokuwa ikitumika kusafirisha watumwa (Pario msomali/veterinary stock route) kutoka mikoa ya kigoma, Tabora hadi Handeni – Tanga. Pori la Swagaswaga lilipandishwa hadhi na kuwa Pori la Akiba kwa tangazo la Serikali Na. 72 la tarehe 21/02/1997 likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 871 na mzingo wa kilomita 183.184.  Pori la Akiba Swagaswaga ni Hifadhi pekee ya Wanyamapori iliyoko karibu na jiji la Dodoma na linazungukwa na vijiji 17 vilivyopo katika Mkoa wa Dodoma na Singida.
 Mkuu wa Wilaya ya Chemba Bwana  Simon Odunga akitoa maelezo kwa timu ya Makatibu Wakuu kuhusiana na mipaka ya vijiji  vilivyoko kwenye Pori la Akiba  Swagaswaga 
 Timu ya Makatibu Wakuu wakishuhudia Mifugo ikinywa maji kwenye mto Bubu ambao  hutiririsha maji yake kuelekea Bwawa la ufuaji umeme la Mtera. 
  Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Profesa Adolf Mkenda, Akisikiliza kwa makini maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Meneja wa Pori la Akiba Swagaswaga Bw. Alex Choya  ( Hayumo Pichani)  kuhusu umuhimu wa Pori la Akiba Swagaswaga. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi  Prof. Elisante  Ole Gabriel na Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Chemba Bwana Simon Odunga.
 Mkuu wa Wilaya ya Chemba Bwana Simon Odunga akiwaelezea jambo Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Prof. Elisante Ole Gabriel walipotembelea Pori la Akiba Swagaswaga kuhusiana na Suala la urasimishaji wa vjiji vilivyomo ndani ya Hifadhi. 
Timu ya Makatibu Wakuu wakishuhudia Mifugo ikinywa maji kwenye mto Bubu ambao  hutiririsha maji yake kuelekea Bwawa la ufuaji umeme la Mtera.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad