HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, February 4, 2019

NAIBU WAZIRI NDITIYE AKABIDHI KOMPYUTA SHULE ZA SEKONDARI MPANDA

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amekabidhi kompyuta 25 kwa shule za sekondari Mpanda mkoani Katavi kwa lengo la kukuza kiwango cha ufaulu na kuongeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) shuleni kwa kuwawezesha waalimu kutumia kufundishia na wanafunzi kujifunzia
Nditiye amewataka waalimu na wanafunzi wa shule hizo kuhakikisha kuwa kompyuta zilizotolewa zinatumika kwa nia njema kutoa elimu kwa watoto wetu kwa kuwa sasa dunia ni kijiji. 

Amefafanua kuwa lengo ni tupate wanafunzi mahiri kwa kompyuta hizo kutumika na wanafunzi wengine kwenye shule mbali mbali kwa kuziunganisha kompyuta hizo kwenye mtandao ili mwalimu mmoja aweze kufundisha wanafunzi wengi wengine wa shule nyingine
“Kumbukeni hapo zamani wanafunzi wa mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma ilikuwa inatoa wanafunzi wenye ufaulu mzuri, hivyo tuwarithishe wanafunzi wetu,” amesisitiza Nditiye
Kompyuta hizo zimetolewa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambao una dhamana ya kuhakikisha wananchi waishio vijijini na maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara wana wasiliana kwa kuzipatia kampuni za simu za mkononi ruzuku ya kujenga minara ili kufikisha huduma za mawasiliano maeneo mbali mbali nchini

Nditiye amekabidhi kompyuta 25 zenye thamani ya shilingi milioni 46 kwa Mbunge wa Mpanda Mjini, Mhe. Sebastian Kapufi kwa niaba ya waalimu na wanafunzi wa shule za sekondari zilizopo mjini humo kwa kuwa aliiomba Serikali kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu  ili shule hizo ziweze kupatiwa kompyuta hizo.

“Nimeanza kumsumbua Nditiye zaidi ya mwaka mmoja na nusu kuomba kompyuta, unaweza kuona kompyuta ni chombo chepesi ila sio hivyo kwa kuwa ni chombo muhimu na kitatunza siri,” amesema Kapufi
Pia, ameongeza kuwa tunalotekeleza hapa ni upendo na na litaenda kufuta ujinga wa watoto wetu kwenye shule za sekondari kwa kutumia kompyuta hizi. Vile vile ameishukuru Serikali kwa ahadi ya mafunzo ya kompyuta ambayo yatatolewa kwa waalimu wa shule ili kuwawezesha namna ya kutumia na kufanyia matengenezo madogo madogo kompyuta hizo ambapo ameahidi kuwa atakwenda yeye mwenyewe binafsi kukabidhi kompyuta hizo kwa kila shule

 Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji kutoka UCSAF Mhandisi Albert Richard amesema kuwa UCSAF imekuwa ikitoa kompyuta hizo kwenye shule mbali mbali nchini kupitia mradi wa kuunganisha shule ujulikanao kama “School Connectivity”. Richard amesema kuwa ni imani yao kuwa kompyuta hizo zitatumika kwa malengo yaliyopangwa kwa nia ya kuwasaidia wanafunzi kusoma na waalimu kufundishia. Ameongeza kuwa UCSAF itatoa mafunzo kwa waalimu wa shule za sekondari za Mpanda ya namna ya kutumia kompyuta hizo kufundushia pamoja na waalimu wao wenyewe kuweza kuzifanyia matengenezo madogo madogo kompyuta hizo pale zinapoharibika.

Akizungumza kwa niaba ya waalimu wa shule za sekondari za Mpanda, Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Mpanda, Enelia Lutungulu amesema kuwa shule za msingi na sekondari zina uhitaji mkubwa sana wa kompyuta kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia na TEHAMA ambapo kazi nyingi zinahitaji mawasiliano kwa kutumia kompyuta
“Shule hizi zina uhitaji mkubwa wa kompyuta kwa kuwa baadhi ya shule kompyuta zinazotumika ni za waalimu binafsi na hivyo kuleta ugumu wa utendaji wa kazi wa kila siku ukizingatia upokeaji na utoaji wa taarifa ni wa kila mara,” amefafanua Lutungulu.

Ameongeza kuwa kompyuta hizo zitakuwa kichocheo cha kuongeza na kurahisisha ufanisi wa kazi katika shughuli mbali mbali zikiwemo za uchapishaji wa mitihani ndani ya shule, ukusanyaji na uhifadhi wa data za kielimu katika shule, utoaji rahisi na wa haraka wa taarifa kwa kutumia TEHAMA, kupokea miongozo na maagizo mbali mbali ya kikazi kwa kutumia mawasiliano ya barua pepe, kwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ikiwemo TEHAMA na mawasiliano katika kazi za kila siku. Makabidhiano ya kompyuta hizo yamehudhuriwa na wakuu wa shule za sekondari, viongozi na wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi na Wilaya ya Mpanda na viongozi wa Chama cha Mapinduzi wa Wilaya hiyo

Akiwasilisha taarifa ya mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Abdallah Malela amemuomba Nditiye kuipatia mkoa huo ofisi ya TTCL ya ngazi ya mkoa tofauti na hali ilivyo sasa ambapo ipo ofisi ya TTCL ya ngazi ya wilaya. Pia, ameongeza kuwa mkoa upatiwe usafiri wa ndege kwa kuwa ina kiwanja kizuri na kuna wateja wa kutosha

Nditiye amepokea changamoto hizo na kuielekeza Bodi ya TTCL na menejimenti yake kufungua ofisi ya Shirika hilo lenye hadhi ya mkoa ndani ya kipindi cha mwezi mmoja. Pia, ameuhakikishia uongozi wa mkoa na wananchi wa Katavi kuwa Serikali inaleta gari la zimamoto kwenye uwanja huo na huduma za usafirishaji utaanza kutolewa kwa wananchi na wadau wa mkoa huo. Pia, Nditiye alitembelea na kukagua kiwanja hicho cha ndege na kuona hali ya kiwanja na miundombinu yake.
 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (katikati) akikabidhi kompyuta kwa Mbunge wa Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi (wa pili kulia) kwa ajili ya shule za sekondari mjini humo. Wakishuhudia, wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Mhandisi Albert Richard na Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Abdallah Malela (wa pili kushoto)
 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akifafanua jambo kwa viongozi wa Mkoa wa Katavi, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda na waalimu wa sekondari (hawapo pichani) kuhusu ukuaji na maendeleo wa sekta ya Mawasiliano nchini. Kulia kwake ni Mbunge wa Mpanda Mjini, Mhe. Sebastian Kapufi na kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Abdallah Malela.
 Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Mhandisi Albert Richard akitoa maelezo ya kompyuta walizotoa kwa shule za sekondari za Mpanda. Walioketi wakimsikiliza, wa kwanza kushoto ni Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye na  katikati ni Mbunge wa Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi.
 Afisa Elimu wa Shule za Sekondari wa Manispaa ya Mpanda, Enelia Lutungulu akisoma risala ya shukrani kwa Serikali kwa niaba ya waalimu na wanafunzi wa shule kwa kuzipatia shule hizo kompyuta 25. Walioketi wakimsikiliza wa kwanza kushoto ni Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye na  katikati ni Mbunge wa Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi.
 Waalimu wa shule za sekondari, viongozi na watendaji wa mkoa wa Katavi na Manispaa ya Mpanda wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (hayupo pichani) wakati akiwahutubia kabla ya kukabidhi kompyuta kwa ajili ya shule za sekondari za Mpanda.
 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akisisitiza jambo kwa Afisa Usalama Msaidizi wa Uwanja wa Ndege wa Katavi, Fredrick Valentine(wa kwanza kulia) wakati akikagua miundombinu na hali ya uwanja huo akiwa ziarani mkoani humo. Mbunge wa Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi (wa tatu kulia) akifuatilia kwa makini mazungumzo hayo.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (aliyesimama mbele amefunga mikono) akiwa kwenye picha ya pamoja na waalimu wa shule za sekondari, viongozi na watendaji wa mkoa wa Katavi na Manispaa ya Mpanda. Wan ne kulia ni Mbunge wa Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi na wa tano kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Abdallah Malela

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad