HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, February 17, 2019

GEREZA LA KWITANGA LIPATIWE KIWANDA CHA KISASA-MAJALIWA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara ihakikishe gereza la Kwitanga mkoani Kigoma linapata kiwanda bora na cha kisasa cha kukamulia mafuta ya mawese kitakachoonesha dhamira ya Serikali ya kufufua zao la michikichi nchini.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na jitihada zilizofanywa na Jeshi la Magereza katika kuboresha shamba lake la michikichi pamoja na mabadiliko waliyoyafanya kwenye kiwanda chao cha kuzalisha mafuta.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Februari 17) wakati alipotembelea Gereza la Kwitanga kwa ajili ya kukagua shamba la michikichi na kuzindua trekta na kufungua sero moja iliyojengwa gerezani hapo.
Amesema amefurahishwa baada ya kukuta mashine mpya ya kukamulia mafuta ya mawese inafungwa kwenye kiwanda cha gereza hilo ambayo itakuwa inatumia mota tofauti za zamani wapolikuwa wanatumia mashine ya kusukumwa na mikono.

Kadhalika Waziri Mkuu ameliagiza Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) waimarishe teknolojia ya kukamua mafuta kwenye kiwanda hicho ili kiweze kuzalisha kwa tija.

Katika kuhakikisha gereza hilo linakuwa la mfano kwenye kilimo cha zao la michikichi, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inunue gari lenye winchi litakalorahisisha uvunaji wa chikichi.

Waziri Mkuu amesema njia inayotumiwa kwa sasa ya kupanda juu ya mchikichi wakati wa mavuno si salama kwa mvunaji, hivyo ni vema wakatumia magari hayo yenye winchi kwa ajili ya kurahisisha shughuli ya uvunaji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kigoma, Leonard Burushi amesema wamefanikiwa kuongeza uzalishaji wa mafuta kutoka pipa 63.4 kwa mwaka 2016/2017 na kufikia pipa 97 kwa mwaka 2018/2019 na zoezi la uvunaji bado linaendelea.

Amesema mafanikio hayo yametokana na maagizo yalitolewa na Waziri Mkuu alipotembelea gereza hilo Julai, 2018, ambapo pamoja na mambo mengine aliwaagiza waboreshe eneo la kukamulia mafuta ili waongeze uzalishaji.

Kiongozi huyo wa Magereza mkoa wa Kigoma amesema eneo la ekari 20 limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha kukamua mafuta ya mawese, maghala ya kutunzia mafuta machafu na upanuzi wa kiwanda baadae.

Amesema maelekezo mengine yaliyotolewa na Waziri Mkuu ni pamoja na Magereza ya Kwitanga na Ilagala yaongeze eneo la mashamba yake kwa ajili ya kupanda michikichi mipya ambalo limetekelezwa. Amesema tayari gereza la Ilagala limeandaa jumla ya ekari 150 zenye uwezo wa kupandwa michikichi aina ya tanera 8,550 na Kwitanga ekari 400 ambazo zitapandwa miche 22,800 ya michikichi aina ya tanera.
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akisalimiana na Kamishina wa  Magereza Nchini, Fhaustine Kasike wakati alipowasili kwenye Gereza la Kwitanga mkoani Kigoma  akiwa katika ziara ya kufufua zao la michikichi mkoani humo Februari 17, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipanda mchikichi ikiwa ni ishara ya kuzindua mpango wa kupanua mashamba ya michikichi katika Gereza la Kwitanga mkoani Kigoma, Februari 17, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua Sero katika Gereza la Kwitanga  Mkoani Kigoma, Februari 17, 2019. Gereza hilo ni maarufu kwa kilimo cha michikichi.  Kulia ni mkewe Mama Mary na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenrali Mstaafu, Emmanuel Maganga. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akitazama mashine ya kukamua mafuta ya mawese wakati alipotembelea Gereza la Kwitanga mkoani Kigoma ambalo ni maarufu kwa kilimo cha michikichi, Februari  17, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mama Mary wakitoka baada ya kuzindua  sero  katika Gereza la Kwitanga, maarufu kwa kilimo cha michikichi, Mkoani Kigoma, Februari 17, 2019. Walikuwa katika ziara yenye lengo la kufufua zao la michikichi mkoani humo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua matrekta mawili aina ya Ursus yenye thamani ya shilingi milioni 145 yatakayosaidia kuinua kilimo cha michikichi katika Gereza la Kwitanga mkoani Kigoma Februari 17, 2019.  Wengine kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamadi Masauni, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya, Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasha Trekta aina ya Ursus wakati alipozindua matrekta mawili yatakayosaidia kuinua kilimo cha michikichi katika Gereza la Kwitanga mkoani Kigoma, Februari 17, 2019.(Picha na Ofisi a Waziri Mkuu)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad