HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, January 24, 2019

Muhimbili kusuka upya mfumo wa kliniki

Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) umesema unaangalia jinsi ya kuboresha mfumo wa kliniki ili wagonjwa wahudumiwe kwa wakati baada ya kufika katika hospitali hiyo kupata huduma za matibabu. Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru wakati akizungumza na madaktari bingwa wa Muhimbili kuhusu namna bora kuboresha huduma za matibabu katika hospitali hiyo.

Hospitali hiyo inahudumia wagonjwa wa nje 1,500 kwa siku. Pia, kuna wagonjwa 1,200 hadi 1,300 wamelazwa wodini wakati wote. Aidha wagonjwa wa nje walio wengi wanapenda kuja asubuhi hata kama kliniki zao zinaanza mchana. Prof. Museru amesema hatua hii ina lengo la kuboresha huduma katika kliniki hizo ni  kuondoa msongamano wakati mgonjwa au wagonjwa wakisubiri kuona madaktari bingwa wa hospitali hiyo.

“Wakuu wa idara kupitia kwa madaktari mtuletee mapendekezo ambayo tutaangalia jinsi ya kujenga mazingira bora ambayo wagonjwa watatumia muda mfupi kumuona daktari. Tunataka mgonjwa asikae muda mrefu kwenye foleni,”amesema Prof. Museru. Pia, Prof. Museru amewaahidi wataalam hao kwamba Uongozi wa Hospitali chini ya Bodi ya Wadhamini utaendelea kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na kutoa huduma bora kwa wananchi mbalimbali wanaofika hospitali hapo kupata matibabu.

“Naomba tuendelee kutumia vizuri na kikamilifu miundombinu iliyopo ili kuongeza tija na wananchi wametuamini ndiyo maana wengi wamekuwa na matumaini makubwa sana na huduma tunazotoa” alisema Prof. Museru. Prof. Museru amewashukuru sana watoa huduma na wafanyakazi wote kwa ujumla wao kwa namna ambavyo wanajituma na kufanya kazi kwa bidii hali iliyoifanya Hospitali kufanya mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma bora za afya hapa nchini hususani katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Akizungumzia upatikanaji wa dawa katika hospitali hiyo, mkurugenzi huyo amesema licha ya dawa kupatikana kwa zaidi ya asilimia 95 hospitali yake  inaendelea kuimarisha utoaji wa dawa kwa wagonjwa ili kuhakikisha kila mgonjwa anayetibiwa anapata dawa kwa wakati. Katika mkutano huo madaktari walijadili njia za kuimarisha utoaji wa huduma bora za matibabu kwa wagonjwa mbalimbali samabamba na kukubaliana kufanya kazi kwa juhudi ili kufikia malengo yaliowekwa na hospitali hiyo ya kutoa huduma bora za ubingwa wa juu nchini.

Hospitali ya Taifa Muhimbili ina wafanyakazi 2,705, kati yao madaktari ni 328, ambapo madaktari bingwa ni 186 na 142 ni madaktari wa kawaida. Aidha, Hospitali ina wauguzi 946 na waliobaki ni wafanyakazi wa kada nyingine.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akizungumza na madaktari bingwa wa hospitali hiyo jinsi ya kuboresha mfumo wa kliniki ili wagonjwa wahudumiwe kwa wakati.
 Baadhi ya madaktari bingwa wa Muhimbili na wataalam wengine wa hospitali hiyo wakiwa kwenye mkutano huo leo.
 Mkuu wa Idara ya utunzaji wa Kumbukumbu wa Muhimbili, Geofrey Semu akichangia mada jinsi ya kuboresha mfumo wa kliniki katika mkutano huo leo.
  Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof. Museru (wa tatu kushoto) akimsikiliza Geofrey Semu wakati akichangia mada kwenye mkutano huo. Wengine baadhi ya wakurugenzi katika kurugenzi za hospitali hiyo.
  Daktari Bingwa wa Afya ya Kinywa na Meno, Dkt. Deo Kilasara akizungumza kwenye mkutano huo leo.
 Baadhi ya madaktari bingwa wakifuatilia michango ya mada mbalimbali kwenye mkutano huo.
 Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura na Ajali, Dkt. Patrick Shao akichangia mada jinsi ya kuboresha mfumo wa kliniki katika hospitali hiyo.
 Daktari Bingwa wa Kina mama, Dkt. Geofrey Marandu akichangia mada kwenye mkutano huo leo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad