HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, January 29, 2019

Mauaji ya Watoto Njombe, Imani za kishirikina, visasi vyatajwa

Hali ya majonzi, vilio na simanzi ilitawala wakati wa mazishi ya  miili ya watoto watatu wa familia moja waliouawa kikatili ikiwa takribani mwezi mmoja sasa tangu  matukio ya kupotea na kuuawa kwa watoto katika Wilaya ya Njombe.

Akizungumza katika mazishi ya watoto hao watatu;Godliver Mwenda(11), Gasper Nziku(8) na Geribet Nziku(5), Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema Serikali inalaani mauaji hayo na imejipanga kuhakikisha inadhibiti na kutokomeza mtandao huo unaojihusisha na mauaji hayo ya kikatili kwa watoto

“Tukio hili halitopita bure bure na tunataka iwe fundisho kwa watu wengine wote wenye roho za kinyama waliotekeleza mauaji haya na tayari baadhi ya watuhumiwa wa mauaji haya tayari washakamatwa kwa kupitia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama likwemo jeshi la polisi,” alisema Masauni

“….nataka nitoe ujumbe huu kwa nchi nzima kwamba mtu yoyote ambae  anajishughulisha na mauaji dhidi ya binadamu ikiwemo watoto wadogo kama hawa tunamuhakikishia tutamkamata na serikali haitolala katika hili” aliongeza Masauni

Akizungumza wakati wa mazishi hayo Baba wa marehemu hao,Danford Nziku ameiomba Serikali kuimarisha ulinzi maeneo mbalimbali katika kijiji hicho huku akisisitiza kutafutwa kwa watuhumiwa waliohusika na mauaji ya watoto wake

“Watoto wangu wameondoka wakiwa bado na umri mdogo sana, ndoto zao sasa zimezimwa ghafla baada ya kufanyiwa ukatili,na wao sio wa kwanza kufanyiwa matukio hayo ndani ya mwezi huu, naiomba serikali yangu kuimalisha ulinzi katika maeneo haya,sasa naishi kwa hofu hapa nyumbani na mke wangu” alisema Baba wa marehemu hao.

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake mkazi wa Kijiji cha Ikando wilayani Njombe, amesema matukio hayo yametokea sana kipindi cha nyuma  huku akiiomba serikali kupiga vita ramli chonganishi, kupitia uhalali wa waganga wa kienyeji waliopo wilayani hapo.

“Vifo hivi vinasikitisha nadhani serikali iandae utaratibu wa kuhakiki hawa wataalamu wetu wa kienyeji, wamekua chanzo cha malumbano mengi hapa kijijini, watu wamekua wakituhumiana mambo ya uchawi hali inayopelekea kuwepo kwa visasi kati yao ambavyo hupelekea vifo kama hivi,” alisema mwananchi huyo

Akizungumza juu ya mauaji hayo  Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kibena, Barnabas Baraka amesema vifo vya watoto hao vimetokana na kushambuliwa na vitu vizito na vyenye kali maeneo ya kichwani huku mmoja kati ya maiti hizo akiwa amekatwa sikio la kulia.
 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na wananchi waliohudhuria mazishi ya watoto watatu wa familia moja waliouawa kikatili katika kijiji cha Ikando Kata ya Kichiwa, wilayani Njombe, ambapo aliahidi Serikali kukomesha mauaji hayo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akiweka mchanga katika moja ya makaburi ya watoto watatu wa familia moja waliouawa kikatili katika kijiji cha Ikando  Kata ya Kichiwa, wilayani Njombe.
 Moja ya jeneza lililobeba mwili wa mmoja wa watoto wa familia moja waliouawa kikatili katika kijiji cha Ikando  Kata ya Kichiwa, wilayani Njombe, likiingizwa kaburini wakati wa mazishi hayo.
 Ndugu wa familia iliyopoteza watoto watatu wakiweka kaburini nguo za mmoja wa watoto hao ikiwa ni utekelezaji wa mila na desturi ambapo marehemu huzikwa na nguo zake zote.Mazishi hayo yamefanyika katika Kijiji cha Ikando Kata ya Kichiwa, wilayani Njombe.
Waombolezaji wakiwa wamebeba majeneza ya  watoto watatu; Godliver Mwenda, Gasper Nziku na Geribet Nziku wa familia moja waliouawa kikatili katika kijiji cha Ikando  Kata ya Kichiwa, wilayani Njombe.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad