HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, January 24, 2019

CHANGAMOTO HALMASHAURI YA BAHI ZAMSONONESHA NAIBU WAZIRI WA ARDHI

Na Munir Shemweta, BAHI
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula amekutana na changamoto kubwa zinazoikabili halmashauri ya wilaya ya Bahi mkoani Dodoma kiasi cha kushindwa kuwabana maafisa ardhi katika halmashauri hiyo.

Akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya Serikali kupitia sekta ya ardhi katika halmashauri mbalimbali nchini jana, Dk Mabula aliikuta halmashauri ya Wilaya ya Bahi ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ufinyu wa bajeti na  uhaba wa magari.

Hali hiyo imesababisha halmashauri hiyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kama vile kukusanya maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi, kuwapelekea wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi hati za madai, kupima na kupanga viwanja pamoja na kwenda kutatua migogoro ya ardhi.

‘’Sekta ya ardhi ni idara nyeti sana ambayo inaweza kuingizia seriali mapato mengi lakini kama haitawezeshwa kufanya kazi ipasavyo kwa kupatiwa rasilimali fedha na vifaa kama magari basi itashindwa kutekeleza majukumu yake na hivyo kuifanya serikali kukosa mapato kupitia sekta hiyo.’’ Alisema Dk Mabula

Mkuu wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Chediel Mrutu alimwambia Naibu Waziri Mabula kuwa, idara yake hajawahi kupatiwa fedha za mgao wa ndani na bajeti yake kwa mwaka ni milioni mbili na laki tano na kubainisha kuwa kiasi hicho wakati mwingine  hakipatikani chote. Kwa mujibu wa Mrutu idara yake haina gari la kuwawezesha kufanya shughuli za ardhi ambazo wakati mwingine hutakiwa kwenda umbali mrefu kushughulikia masuala ya ardhi.

Kufuatia hali hiyo Dkt. Mabula alitaka kufahamu kiasi cha fedha za mgao inazopata idara nyingine kwenye halmashauri hiyo kufuatia katika ziara zake kubaini idara ya ardhi kutengwa na kupewa kiasi kidogo cha fedha ukilinganisha na halmashauri nyingine ambapo kwa upande wa Bahi hakuna tofauti jambo lililomfanya kuishiwa nguvu na kusema halmashauri hiyo inahitaji kusaidiwa.

Dk Mabula alisema kiasi cha milioni mbili na laki tano inazopata halmashauri kwa mwaka haiwezi kufanya kitu kwa idara kama ya ardhi yenye majukumu mengi jambo lililoifanya kukusanya milioni saba tu hadi kufikia desemba mwaka jana huku ikiwekewa malengo ya milioni 47.

Alisema kwa hali waliyo nayo halmashauri ya Wilaya ya Bahi haiwezi kufikia asilimia hamsini ya malengo ya serikali na kuagiza ofisi ya Kamishana Msaidizi Kanda kuangalia namna itakavyoweza kuisaidia idara ya ardhi angalau iweze kutatua baadhi ya changamoto.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Bahi leo Mavika alisema halmashauri yake inakabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji mapato ambapo alisema kwa sasa inajitahidi  kuhakikisha kiasi kidogo kinachopatikana kinagawanywa kwenye idara zote za halmashauri huku idara ya ardhi ikipewa kipaumbele kutokana na umuhimu wake na kuongeza kuwa halmashauri hiyo kwa sasa ina magari mawili tu jambo linalowawia vigumu kutekeleza majukumu ya kila siku.

Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mwanahamisi Munkunda alisema ili halmashauri yake iweze kutoka ilipo mikakati madhubuti inahitajika ili kuondokana na hali hiyo ambayo imekuwa ikiwakatisha tama watumishi kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu ipasavyo kutokana na changamoto zinazowakabili.
 Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Bahi mkoani Dodoma alipofanya ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Bahi Mwanahamisi Munkunda, na wa tatu kushoto ni Mkurugenzi wa Halamashauri ya Wilaya ya Bahi leo Mavika.
 Mkuu wa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma Mwanahamisi Munkunda akizungumza wakati wa ziara ya Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi.
 Mkuu wa Idara ya Ardhi katika halmashauri ya Wilaya ya Bahi mkoa wa Dodoma Chediel Mrutu akitoa maelezo kuhusiana na sekta ya ardhi  wakati wa ziara ya Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi.
Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akizungumza wakati akikagua mfumo katika ofisi za ardhi halmashauri ya wilaya ya Bahi mkoani Dodoma alipofanya ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad