HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, September 12, 2018

WAZIRI DKT KIGWANGALLA ARUHUSIWA KUTOKA HOSPITALI

Jopo la Madaktari Bingwa wa MOI linalomhudumia Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla limemruhusu kutoka wodini baada ya kujiridhisha kwamba afya yake imetengamaa na anaweza kurejea nyumbani na atakuwa anakwenda hospitalini hapo  kama mgonjwa wa nje kwa ajili ya muendelezo wa matibabu yaliyosalia.

Jopo hilo la madaktari bingwa watano  wa kada za Mifupa, Usingizi na magonjwa ya ndani limefikia maamuzi hayo baada ya kumhudumia Dkt. Kigwangalla toka tarehe 12/08/2018 alipohamishiwa katika taasisi hiyo kwa ajili ya matibabu ya kibingwa ya mkono wake wa kushoto baada ya kupata matibabu mengine katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt.Respicious Boniface amemtakia kila kheri Dkt Kigwangalla katika kutekeleza majukumu yake ya kitaifa kwani ni muda muafaka wa kwenda kuwatumikia wananchi.
“Kwa niaba ya jumuiya ya Taasisi ya Mifupa MOI, tunakutakia kila la kheri katika kutekeleza majukumu yako ya ujenzi wa Taifa. 

Ilikuwa ni  heshima kubwa kuwa nawe hapa kwa kipindi cha takribani mwezi mmoja... Tunaamini umeridhishwa na huduma zetu na kama kuna mahali umeona mapungufu ni vyema ukatujulisha ili turekebishe” alisema Dkt Boniface. 

Dkt. Boniface amemueleza Dkt. Kigwangalla kwamba kwa kuwa yeye ni daktari itakua rahisi kubaini mabadiliko yoyote ambayo sio ya kawaida na hivyo kushauriana na madaktari wa MOI ili kupata ufumbuzi.

Kwa upande wake Dkt. Kigwangalla ameushukuru uongozi wa Taasisi ya MOI, madaktari na wauguzi ambao wamekuwa wakimhudumia katika kipindi chote alipokuwa wodini.
“Nichukue fursa hii ya kipekee kuwashukuru watoa huduma wote kuanzia pale nilipopata tatizo na hadi kufika MOI, watanzania wote ambao mmekua mkiniombea na kunitembelea hapa hospitali baada ya kupata ajali, namshukuru Mungu afya yangu inaendelea vizuri sasa na nimeruhusiwa kwenda nyumbani” alisema Dkt Kigwangalla.

Dkt. Kigwangalla alipata ajali ya gari tarehe  4/08/2018 na kupata matibabu ya awali mkoni Manyara kabla ya kuhamishiwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili na baadae katika Taasisi ya Mifupa MOI.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa MOI Dkt.Respicious Boniface (kushoto) akizungumza jambo na  Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa MOI Dkt.Respicious Boniface (kushoto) wakifurahia jambo na  Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla mara alipokuwa amekwenda kumuaga. Kulia ni Mkuu wa Wod hiyo, Happyness Mligo 
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla akiondoka hospitalini kwa furaha kubwa baada ya kuruhusiwa na madaktari.
 (PICHA ZOTE NA KHAMISI MUSSA) 



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad