HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, September 12, 2018

Serikali Haijavunja Mkataba wa Wanufaika wa Mikopo ya Elimu ya Juu - Prof. Ndalichako.

Na Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.

Serikali imesema haijavunja mkataba wowote na wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu bali makato ya asilimia 15 kutoka kwenye mshahara ghafi wa mnufaika wa mkopo huo ni ya kisheria.

Hayo yameelezwa leo Bungeni, Jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbozi, Mhe. Paschal Yohana Haonga juu ya kinachodaiwa kuwa Serikali imevunja mkataba kinyume na makubaliano kwa kuwa wakopaji walisaini mkataba wa asilimia 8 na siyo 15.

"Kilichofanyika mwaka 2016 katika marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo (SURA 178) ni kuiboresha sheria hii kwa kutaja kiwango mahsusi cha asilimia 15 kinachopaswa kukatwa kutoka mshahara ghafi wa mnufaika. Awali, kabla ya marekebisho hayo, kifungu cha 7(1) (h), kiliipa Serikali mamlaka ya kupanga kiwango cha makato na kubadilisha kiwango pale itakapoona inafaa," alifafanua Prof. Ndalichako.

Ameendelea kusema kuwa, Serikali inafahamu umuhimu wa kuwashirikisha wadau katika marekebisho ya sheria yoyote. Hivyo basi, katika mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (SURA 178) ya mwaka 2016, wadau mbalimbali walishirikishwa.

Amewataja wadau walioshirikishwa kuwa ni pamoja na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi (TUGHE na TUCTA), Chama cha Mawakili nchini (TLS) pamoja na wanafunzi kutoka Taasisi za Elimu ya Juu kama vile Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo cha Elimu ya Biashara - Dodoma (CBE) na Chuo cha Mipango (IDRP).

Aidha amesema, makato hayo ya asilimia 15 yana lengo la kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali zinarejeshwa kwa wakati iliziweze kuwasomesha Watanzania wengine wahitaji. Hivyo, kwa sasa Serikali haina mpango wa kusitisha makato hayo.

Prof. Ndalichako ametoa wito kwa wanufaika wote wa mikopo ya Elimu ya Juu kuhakikisha kuwa wanarejesha kwa wakati mikopo waliyokopeshwa na Bodi hiyo ili iweze kusaidia watoto wengine wenye uhitaji.
Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Mhe.Prof Joyce Ndalichako akijibu maswali mbalimbali ya wabunge leo Bungeni Jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad