Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akihutubia
hadhara ya kikosi kazi cha watu 260 alichokiunda kwa ajili ya operesheni
Sangara 2018 na Wakuu wa Mikoa mitano inayozunguka Ziwa vicktoria
wakati wa mkutano wa kufanya tathimini ya Operesheni hiyo. Picha
na John Mapepele.
Viongozi wakuu wa Wizara ya Mifugo na
Uvuvi waliokaa wakiwa katika picha ya pamoja na makamanda wakuu
wa Operesheni Sangara 2018 (waliosimama) wakati wa mkutano wa kufanya
tathimini ya Operesheni hiyo. Picha na John Mapepele
Viongozi wakuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliokaa wakiwa katika
picha ya pamoja na sekretarieti ya Operesheni Sangara 2018 (waliosimama)
wakati wa mkutano wa kufanya tathimini ya Operesheni hiyo.
Na John Mapepele, Mwanza
WAKUU wa mikoa inayozunguka Ziwa Victoria wamekosoa vikali tabia ya
baadhi ya wanasiasa kuipaka matope dhamira njema ya Serikali ya
kupambana na uvuvi haramu ulioshamiri katika ziwa hilo na kutaka
viongozi wa aina hiyo kutangaza masilahi yao kwenye eneo la uvuvi kabla
ya kuwashambulia viongozi wanaosimamia zoezi hilo kwa misingi ya
kisheria.
Wakizungumza kwenye kikao cha tathmini ya operesheni sangara awamu ya
pili iliyowahusisha Wakuu wa Mikoa,Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa
Mikoa, Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Makamanda wa Polisi wa
mikoa na Wakuu wa Idara ya Usalama wa Taifa wa mikoa yote inayozunguka
Ziwa Victoria jijini Mwanza jana viongozi hao wametaka hatua zaidi
zichukuliwe ili kunusuru rasilimali hizo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka alielezea kuchukizwa na tabia
inayoanza kuota mizizi ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kuipaka matope
dhamira nzuri ya Serikali ya kukabiliana na uvuvi haramu na kutaka
viongozi wa aina hiyo watangaze masilahi yao kabla ya kuanza
kuwashambulia viongozi wanaosimamia operesheni hiyo inayotekelezwa kwa
mujibu wa sheria .
“Viongozi wanaopinga operesheni ya kupambana na uvuvi haramu ni muhimu
watangaze kwanza masilahi yao kuhusu eneo la uvuvi ili wasiendelee
kuchafua taswira za viongozi wanaosimamia wizara hii”alisema Mtaka.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela alisema kumekuwepo na dhana
zinazojengeka kwamba viongozi wa mikoa inayozunguka Ziwa Victoria
hawaungi mkono mapambano ya kukabiliana na uvuvi haramu operesheni jambo
ambalo alisema ni upotoshaji mkubwa na kwamba Serikali ya mkoa iko
mstari wa mbele na kuwabana watendaji wa ngazi zote watakaobanika
kufadhili uvuvi haramu.
Alisema ni muhimu operesheni hiyo iwe endelevu na kubainisha kuwa suala
la uvuvi haramu haliwezi kumalizika kama hakuna dhamira ya dhati
miongoni mwa wasimamizi wa sheria na kwamba uongozi wa mkoa huo
hautakubali kuendelea kuwa na watumishi wazembe wataoshindwa kusimamia
suala hilo.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina alitangaza
kuanza kwa awamu ya tatu ya Operesheni Sangara yenye lengo la kupambana
na uvuvi haramu katika Ziwa Victoria sambamba na kutangaza operesheni
katika maziwa yote na kuagiza viongozi wakuu wa mikoa na wilaya
kuwachukulia hatua kali viongozi wa chini wanaobanika kujihusisha na
kufadhili uvuvi haramu.
Pia alitangaza kuunda kanda mpya ya udhibiti na usimamizi rasilimali za
uvuvi katika wilaya za Ukerewe na Sengerema huku akiunda ofisi mpya ya
Kanda jijini Mwanza itakayokuwa inaratibu shughuli zote katika kanda
hizo saba ili kuongeza usimamizi madhubuti wa rasilimali hizo.
Aidha Mpina aliongeza kuwa katika awamu ya tatu ya operesheni hiyo
itahusisha pia Mahakama zinazotembea ili kuweza kutoa hukumu huko huko
ziwani hali itayowezesha kuondokana kabisa na uvuvi haramu.
Aidha aliwataka watu wote wanaopinga operesheni ya uvuvi haramu wasome
takwimu ili kujua ukubwa wa tatizo katika Ziwa Victoria ambapo jumla ya
watuhumiwa 3,284 wamekamatwa kujihusisha na uvuvi haramu huku samaki
wasioruhusiwa kilo 326,751 , mabondo kilo 5,142 zilikamatwa zikitoroshwa
kwenda nje ya nchi na nyavu haramu 566,497 nazo zilikamatwa na
kuteketezwa. Pia magari 257, mitumbwi 1278 , pikipiki 269 na injini za
mitumbwi 564 vilikamatwa vikihusishwa na makosa ya uvuvi haramu.
Alisema katika baadhi ya maeneo ya Bushengere wilayani Ukerewe wazazi
wamewaonya watoto wao kutotumika na mafisadi kwenye uvuvi haramu kwani
wakikamatwa wao ndio wanaopata tabu na kutelekezwa ambapo wameweka
azimio la kukataa kutumika tena kwenye jambo hilo.
Alisema kutokana na operesheni hizo zinazoendelea za kupambana na uvuvi
haramu hadi kufikia mwezi Disemba mwaka huu watu wote wanaopinga na hata
kuwaombea mabaya viongozi wa operesheni watapata aibu kubwa kwani idadi
ya samaki itaongezeka huku akitoa wito kwa viongozi wa ngazi zote wenye
mapenzi mema na nchi kuunga mkono vita hiyo kwa manufaa ya Taifa.
Katibu Mkuu Uvuvi, Dk. Yohana Budeba alisema wizara hiyo imejipanga
kikamilifu kuhakikisha sekta ya uvuvi inatoa mchango mkubwa katika pato
la Taifa na kwamba operesheni hiyo itaendelea hadi pale uvuvi haramu
utakapokoma.
Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera alisema wamekuwa wakipokea
malalamiko mengi kuhusu operesheni hiyo lakini kila walipofuatilia
kupata ushahidi wa malalamiko hayo waliukosa jambo ambalo wamebaini kuwa
ni njama za makusudi za kutaka kuhujumu nia njema ya Serikali ya
kupambana na kutokomeza uvuvi haramu.
Kamanda Mkuu wa operesheni hiyo kutoka Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Hassan
Shelukindo alisema katika operesheni hiyo jumla ya watuhumiwa 22
wakiwemo wenyeviti wa vijiji na vitongoji na viongozi wa BMU wamefungwa
jela huku wengine 17 mashauri yao yakiwa yanaendelea Mahakamani kwa
makosa ya kujihusisha na uvuvi haramu.
Shelukindo alisema pia watumishi 6 walikuwa kwenye operesheni hiyo
waliondolewa kwa makosa mbalimbali ikiwemo ukiukwaji wa maadili ya kazi
ambapo watumishi hao watachukuliwa hatua za kinidhamu na taasisi zao
huku jumla ya sh. bilioni 7.5 zikikusanywa kutokana na faini
pamoja mauzo ya mabondo,samaki na kayabo.
No comments:
Post a Comment