HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, May 17, 2018

TRA YAKAMATA BIDHAA MBALIMBALI KUPITIA NJIA ZA MAGENDO ZIKIWA NA THAMANI YA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 20

Na Veronica Kazimoto

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekamata malori mawili yenye bidhaa mbalimbali eneo la Loliondo Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha kupitia njia ya magendo yakitokea nchini Kenya zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 20.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha, Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere amesema kuwa, malori hayo yenye namba T 985 AJP na T 840 ABF yalikamatwa usiku wa tarehe 10 Mei, 2018 na kusisitiza kuwa wafanyabiashara wenye bidhaa hizo wamevunja sheria kwa kuwa hawakulipa kodi stahiki kama inavyotakiwa.

Kichere amefafanua kuwa, wafanyabiashara wenye bidhaa hizi zilizokamatwa, wamevunja kifungu cha sheria namba 82 na 200  cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015 na Sheria ya Forodha ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2004. Hivyo kwa Sheria hizi, wafanyabiashara hawa wanatakiwa kulipa kodi pamoja na faini ya shilingi milioni 39 na magari yao kutaifishwa.

"Kwa ujumla bidhaa hizi zote zina thamani ya shilingi 20,037,330.15 ambayo kodi ya bidhaa hizi ni shillingi 28,524,758.11 na adhabu au faini ya bidhaa hizi ni shilingi 10,768,665.08. Hivyo jumla ya mapato yanayotakiwa kulipwa Serikalini ni shilingi 39,293,423.19," alieleza Kichere.

Amezitaja bidhaa zilizokamatwa kuwa ni pamoja na mifuko 362 ya sukari yenye uzito wa kilo 50 kila mmoja, maboksi 40 ya mafuta ya kula yanayoitwa Karibu, maboksi matatu ya mafuta ya kula yanayoitwa Daria, magaloni 100 ya mafuta ya kula yanayoitwa Nyata na maboksi matatu ya viungo vya mboga  

Kufuatia tukio hilo, Kamishna Mkuu Kichere amewakumbusha wafanyabiashara wote kuzingatia taratibu za uingizaji bidhaa nchini ili kuepuka hasara kwenye biashara zao na kuongeza kuwa, TRA haitavumilia ukiukwaji wowote utakaofanywa na wafanyabiashara kwa kutozingatia sheria na taratibu hizo.
`

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad