HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 15 May 2018

SADC WATOA MAFUNZO KWA MAAFISA WA SERIKALI

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Balozi Innocent E. Shiyo akifungua  Warsha ya Mafunzo ya Mfumo wa Ufuatialiaji na Tathmini wa SADC (SADC Results Based Online Monitoring and Evaluation System) kwa niaba ya Katibu Mkuu Prof. Aldof Mkenda, kulia kwake ni Meneja Mradi kutoka GIZ Bw. Robson Chakwama na wa mwisho ni  mmoja wa Wakufunzi wa Warsha hiyo kutoka SADC Bi. Lerato Moleko 

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Wizara kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani chini ya Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) na Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), yametolewa kwa Maafisa wa Serikali na Taasisi za Umma, tarehe 15 - 17 Mei,2018 katika ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere, Jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Washiriki wakifuatilia mafunzo hayo
Sehemu ya Maafisa kutoka Wizarani wakifuatilia mafunzo hayo.
Mkutano ukiendelea
Picha ya pamoja baada ya mkutano
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAARIFA KUHUSU WARSHA YA MAFUNZO JUU YA MFUMO WA UFUATILIAJI NA TATHMINI WA SADC KWA MAAFISA WA SERIKALI NA TAASISI ZA UMMA
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana  na Serikali ya Ujerumani chini ya Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) na Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imeandaa Warsha ya Mafunzo ya Mfumo wa Ufuatialiaji na Tathmini wa SADC (SADC Results Based Online Monitoring and Evaluation System) kwa maafisa wa Serikali na taasisi za umma. Warsha hii inafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam kuanzia tarehe 15 hadi 17 Mei, 2018.

Lengo la warsha hii ni kuwezesha wizara na taasisi mbalimbali za Serikali kufahamu utendaji kazi wa mfumo huu wa SADC ambao unalenga kukusanya taarifa za utekelezaji wa itifaki na programu mbalimbali za maendeleo za SADC ambazo zinatekelezwa ndani ya nchi na kikanda kwa ujumla. 

Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini wa SADC uliridhiwa na Kikao cha Baraza la Mawaziri wa SADC kilichofanyika katika Falme ya Eswatini (Swaziland) mwezi Machi, 2017. Pamoja na mambo mengine, mfumo huu utawezesha pia nchi wanachama kufanya tathmini ya kina ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Kanda uliofanyiwa maboresho wa mwaka 2015-2020 (Revised Regional Indicative Strategic Plan, 2005 – 2020). Mpango huu ndio mkakati mkuu (blueprint) unaosimamia programu zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii zinazotekelezwa SADC. 

Warsha hii itatuwezesha kufuatilia kwa karibu zaidi maendeleo ya utekelezaji wa itifaki na programu mbalimbali za SADC katika sekta zao na kutoa tathmini, na kubainisha fursa zinazopatikana kupitia uanachama wetu. Hadi sasa nchi za Lesotho, Mauritius, Falme ya Eswatini (Swaziland), Zambia na Zimbabwe tayari wameshapata mafunzo ya mfumo huu. Tanzania itakuwa ni nchi ya sita. 
 
Tanzania kama mwanachama hai na mwanzilishi wa Jumuiya hii, hadi kufikia Machi, 2018 imesaini jumla ya Itifaki 28 kati ya itifaki 31. Kati ya Itifaki zilizowekwa saini, jumla ya Itifaki 23 zimesharidhiwa na itifaki 5 ziko katika hatua mbalimbali za kuridhiwa. 

Aidha, kuna Itifaki nyingine tatu ambazo Tanzania bado haijaweka saini ambazo ni itifaki ya Ajira na Kazi 2014; Itifaki ya Utunzaji wa Mazingira kwa Maendeleo Endelevu 2014 na itifaki ya kulinda aina Mpya ya Mimea, 2017. Itafaki hizi zinatarajiwa kusainiwa wakati wa Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali utakaofanyika mwezi Agosti, 2018 Windhoek, Namibia.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 15 Mei ,2018

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad