HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Sunday, 13 May 2018

DED MBINGA ATUMBUA WATUMISHI 10 WA IDARA YA AFYA

Na Mwandishi Wetu Mbinga
MKURUGENZI Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Gombo Samandito,amewasimamisha kazi watumishi kumi wa idara ya Afya akiwemo mganga mkuu wa halmashauri hiyo Dkt Hussen Sepoko.

Watumishi hao  kwa pamoja wamesimamishwa kazi kutokana na matumizi mabaya ya fedha   zaidi ya shilingi milioni 11, 270,000/= zilizotolewa na shirika lisilokuwa na kiserikali la Waterled  kwa ajili ya kufanikisha mpango wa kutoa elimu ya Afya kwa wananchi kinyume na utaratibu.

Kwa mujibu wa Gombo, watumishi hao walijilipa  fedha hizo  na kuongopa kwamba wanakwenda kutoa elimu ya Afya ikiwemo masaula ya Ukimwi katika vijiji mbalimbali,hata hivyo katika hali isiokuwa ya kawaida hawakwenda  vijijini licha ya kila mmoja kuchukua fedha  na  kuzitumia kinyume na taratibu.

Mbali na Dkt Sepoko,watumishi wengine ni   Andrew Kapinga, Tulizo Nziku,Sara Komba,Mary Ngonyani, Evarist Towegela tabibu mwandamizi,Agnes Adidas,Bryson Mapunda na katibu wa Afya Georg Mhina ambaye alichukua kiasi cha zaidi  ya shilingi milioni nne na kwenda kuzifanyia  matumizi mengine kinyume na utaratibu na maelekezo ya fedha hizo.

“ ni kweli nimewasimamisha kazi  watumishi kumi wa Idara ya Afya katika halmashauri yangu, hawa watumishi wakiongozwa na Dkt Sepoko walichukua fedha  zilizotolewa na Waterled kwa kisingizio cha kwenda kutoa elimu ya Afya kwa wananchi lakini hawakufanya hivyo”alisisitiza Gombo.

Alisema,alipata  taarifa kuwa watumishi hao kumi  kila mmoja alichukua  kiasi  cha fedha kulingana na cheo chake na kushindwa kwenda vijijini  kutekeleza wajibu wao, na hata alipomtuma mkaguzi wa ndani   aliyefuatilia  ubadhirifu huo katika vijiji vilivyotajwa  kupitia hati za malipo alibaini kuwa ,  watumishi hao hawakwenda  vijijini husika licha ya kuchukua fedha.

Gombo alibainisha kuwa,  taarifa ya ukaguzi  katika kipindi cha Januari hadi March inaonesha kuwa,idara ya Afya imekuwa na matumizi mabaya ya fedha za miradi jambo linalo sababisha  Idara hiyo kushindwa kufanya vizuri  kutokana na kuwepo kwa watumishi wasiokuwa waadilifu na wanao fanya kazi kwa maslahi binafsi.

Alisema, baada ya kuwasimamisha kazi hatua inayofuata ni ya kinidhamu,ambapo ataunda tume maalum  ambayo itawaita na kuwahoji kabla ya kuchukua hatua  nyingine zaidi za kiutumishi kutokana na makosa waliyofanya.

Alisema, ataendelea kuchukua hatua kali kwa watumishi wote wa halmashauri ambao wamekuwa wakishiriki katika vitendo vya wizi ili kurudisha nidhamu ya matumizi ya fedha za serikali zinazotolewa kwa ajili ya kuboresha huduma za kijamii na miradi mbalimbali ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad