HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 14 May 2018

BALOZI WA IRELAND ASIFU MUHIMBILI KWA KUBORESHA HUDUMA

Balozi wa Ireland nchini Paul Sherlock leo ametembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa lengo la kuona maendeleo ya miradi mbalimbali  inayofadhiliwa na Serikali  ya Ireland.

Katika ziara hiyo Balozi Sherlock ameambatana na ujumbe wa watu saba wakiwemo wabunge watatu kutoka Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali nchini Ireland. Ujumbe huo umetembelea jengo la watoto katika wodi ya watoto wenye Saratani na jengo la wazazi namba moja wodi ya watoto wachanga .

Balozi huyo akipatiwa   maelezo  kuhusu watoto wenye Saratani Mkurugenzi Mtendaji kutoka Tumaini la Maisha (TLM) Dkt. Trish Scanlan amesema TLM  wanashirikiana na MNH kuhakikisha wanaokoa  maisha ya watoto wenye saratani kwa kuwapatia matibabu  stahiki.

Akifafanua amesema ugonjwa wa Saratani  kwa watoto ambao unaongoza nchini ni Saratani ya damu, jicho , figo pamoja na saratani ya matezi.

Ameishukuru Serikali ya Ireland kupitia Balozi wake kwa kufadhili mradi wa maji safi na salama ya kunywa katika jengo la watoto, mradi ambao upo katika hatua za utekelezaji .

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Lawrence Museru amesema pamoja na kwamba Tumaini la Maisha imekua ikisaidia kuhudumia watoto hao MNH pia ipo  mstari wa mbele kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa tiba.

Naye Mkuuu wa Kitengo cha Saratani kwa watoto MNH, Dkt. Rehema Laiti amesema kwa siku MNH  hulaza watoto 60 hadi 100  wenye Saratani na pia katika Kliniki ambazo hufanyika Jumatano na Ijumaa  wanahudumia watoto wenye Saratani 30 hdi 35 kwa siku.  

Katika ziara hiyo Balozi Sherlock ameupongeza uongozi wa MNH kwa jitihada za kuboresha huduma na kuahidi kuwa Ireland  itaendeleza ushirikiano uliopo hivi sasa.
  Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Paul Sherlock akitambulisha ujumbe wa watu saba wakiwamo wabunge watatu wa Kamati ya Hesabu za Serikali ya Ireland kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru alipotembelea hospitali hiyo leo. Balozi huyo ameitembelea MNH leo ili kuona na kupatiwa maelezo ya miradi mbalimbali ya afya inayofadhiliwa na Serikali ya Ireland. Waliosimama nyuma ya Balozi huyo ni watumishi wa MNH wakiwamo wakurugenzi, wakuu wa idara na vitengo.
  Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akizungumza na ujumbe wa watu hao leo.
  Mkuu wa Kitengo cha Saratani kwa watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Rehema Laiti (kulia) akiwaeleza wabunge wa kamati hiyo jinsi wanavyowahudumia watoto wenye matatizo ya saratani waliolazwa kwenye hospitali hiyo.
 Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tumaini la Maisha, Dkt. Trish Scanlan akieleza taasisi yake inavyotoa huduma ya tiba kwa watoto wenye saratani ambao wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
  Mkuu wa Idara ya Watoto Muhimbili, Dkt. Marry Charles akizungumza na ujumbe wa watu hao kabla ya kutembelea wodi ya watoto wachanga leo.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akiwa na Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Paul Sherlock katika hospitali hiyo.
 Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Paul Sherlock akisaini kitabu cha wageni. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Masiliano kwa Umma na Huduma kwa Wateja, Aminiel Aligaesha na Mkuu wa Idara ya Watoto Muhimbili, Dkt. Marry Charles.
 Baadhi ya wajumbe wakijadiliana jambo leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
 Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Paul Sherlock (kushoto) na ujumbe wake wakiwa picha ya pamoja na watendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad