HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 18, 2018

Baadhi ya wafanyakazi wa MSD Kanda ya Mbeya wakionesha ishara ya mshikamano baada ya kuandaa mzigo wa dawa kwa ajili ya kwenda kuzisambaza kwenye vituo vya afya mkoani Mbeya.


Na Dotto Mwaibale, Mbeya

UPATIKANAJI wa dawa na vifaa tiba na vitendanishi vya maabara mkoani Mbeya umefikia asilimia 91.5 kwa mwezi huu wa Mei, kutokana na ongezeko la bajeti ya dawa kwa mwaka fedha 2017/2018. Imeelezwa katika mwaka huo wa fedha bajeti imeongezeka kwa asilimia 20.6 kwa hospitali za wilaya na asilimia 51 kwa zahanati na vituo vya afya.


Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dkt.Yahya Msuya ameeleza hayo wakati maofisa wa Bohari ya Dawa (MSD) walipotembelea wateja wa vituo vya Afya vitatu, vya Wilaya ya Mbeya vijijini wakati wa kusambaza dawa za mgawo wa mwisho wa mwaka wa fedha wa 2017/2018. 


Dkt. Msuya alisema ongezeko la asilimia 91.5 la upatikanaji wa dawa umeimarisha huduma za afya na na kupunguza malalamiko ya wananchi kuhusu kukosekana kwa dawa.
Ofisa Mauzo wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Mbeya, Rhoda Joseph (kushoto) na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Ilembo, Sk.Bwire Biseko (kulia), wakihesabu dawa wakati wa makabidhiano yaliyofanyika kituo hapa jana wilaya ya Mbeya Vijijini. Katikati ni mwanakamati ya Afya wa Kijiji cha Ilembo.

"Hospitali ya Rufaa ya Mbeya inahudumia wagonjwa wapatao 400 kwa siku; upatikaji wa dawa kwa sasa ni wa uhakika na uwepo wa maduka ya MSD ni chachu ya kuimarika kwa huduma," alisema.


Alisisitiza kuwa utekelezaji wa agizo la serikali, la kutoa dawa za malaria bure kwa wananchi pamoja na dawa za msaada katika vituo vya afya na hospitaliti linafanyika.

Mfamasia wa Wilaya ya Mbeya, Apolinary Mwakabana alisema pamoja na upatikanaji wa dawa kuridhisha kwa asilimia 91.5, jitihada zinahitaji ili kuwa na dawa zote, kwani asilimia 9 ya dawa zinazokosekana hulazimika kuzitafuta nje ya bohari.

Ofisa Mauzo wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Mbeya, Rhoda Joseph, akimkabidhi dawa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Afya wa Kijiji cha Ilembo wakati wa zoezi la kukabidhiwa dawa hizo. Kulia ni Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Ilembo, Sk.Bwire Biseko.

Alisifu ushirikiano wa kikanda uliopo kati ya halmashauri na MSD katika huduma hususani kukiwa na mahitaji ya dharula.


Naye Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya cha Ilembo kilichopo Mbeya vijijini Sk.Bwire Biseko, alisema kwa siku kituo hicho kinahudumia wagonjwa 107 kutoka vijiji 10, vyenye wakazi zaidi ya wakazi 17,000.

Alisema uboreshaji wa huduma za afya katika upatikanaji wa dawa na vifaa tiba umeimarisha uchumi na huduma za afya kwa kuwa watu wengi hawamudu gharama za matibabu kutoka nje ya hospitali.

Ubia Enock ni kati ya wakazi ambao walijitokeza katika kamati ya afya ya Kijiji cha Ilembo kushuhudia makabidhiano ya dawa hizo ambapo alisisitiza haja ya serikali kuboresha huduma kwa watu wanaotumia bima za afya.

Baadhi ya wafanyakazi wa MSD Kanda ya Mbeya wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuandaa mzigo wa dawa kwa ajili ya kwenda kuzisambaza kwenye vituo vya afya mkoani humo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad