Kukithiri kwa uvuvi
haramu hasa wa kutumia mabomu kumesababisha mawaziri wa wizara saba
kukutana ghafla ili kujadiliana namna ya kukabiliana na tatizo hilo.
Mawaziri hao ni January Makamba (Muungano na Mazingira ), Dk Charles
Tizeba (Kilimo na Mifugo na Uvuvi), Dk Hussein Mwinyi (Ulinzi na Jeshi
la Kujenga Taifa) na Mwigulu Nchemba (Mambo ya Ndani ya Nchi). Wengine
ni Profesa Jumanne Maghembe (Maliasili na Utalii) na Seleman Jafo (Naibu
Waziri wa Tamisemi) wakati Wizara ya Uchukuzi iliwakilishwa na katibu
mkuu, Dk Leonard Chamulilo.
Akizungumza na wanahabari jana baada ya
kikao hicho, Makamba alisema lengo la mkutano huo lilikuwa ni
kujadiliana namna ya kuchukua hatua za kukabiliana na uvuvi huo.
Makamba
ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho, alisema Tanzania imebarikiwa
kuwa na rasilimali za bahari na samaki, lakini zinaathiriwa na uvuvi
haramu.
“Tumejadiliana kwa kirefu na tumetafakari hatua za kuchukua ili
kukomesha tabia hii. Kikao kilikuwa cha kazi, mikakati na mbinu za
kukabiliana na watu wanaofanya uvuvi haramu,” alisema Makamba.
Hata
hivyo, hakuwa tayari kuzitaja hatua walizokubaliana na mawaziri
wenzake badala yake alisema taarifa kwa kina itatolewa siku zijazo.
Kwa
mujibu wa Makamba, baada ya miezi sita mawaziri hao watakutana na
kupeana mrejesho wa kujua hatua walizokubaliana zimefanikiwa kwa kiwango
gani.
“Shughuli hii ni vita, lazima tupambane. Nguvu ya Serikali
iliyopo hapa (mawaziri) itawashukia wahusika pasipo kujua,” alisema
Makamba.
Dk Tizeba alisema mazingira ya
bahari yanazidi kuharibika na kwamba asilimia 40 ya matumbawe ya samaki
yameathiriwa na uvuvi huo.
“Lazima tuchukue hatua madhubuti kukomesha
uvuvi haramu. Tumejipangia hatua za muda mrefu na mfupi katika hili,”
alisema.
Waziri huyo aliongeza kuwa Tanzania ndiyo nchi iliyobaki na
aibu ya kuvua samaki kwa kutumia milipuko ya mabomu, jambo linaloiletea
sifa mbaya.
Nchemba alieleza kuwa kila Mtanzania ana wajibu wa
kushirikiana na Serikali kukomesha vitendo hivyo kwa kutoa taarifa
kwenye vyombo vya dola.
“Wafichueni wote wanaofanya vitendo hivi na
motisha ipo kwa mtoa taarifa,” alisema Nchemba.


No comments:
Post a Comment