Na Amina Hezron,Mbeya.
Imeelezwa kuwa matokeo ya Utafiti wa Mradi wa Tathimini ya Maji kwa Mazingira
(EFLOWS) unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa
kushirikiana na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)
yanatarajiwa kwenda kutumika kama mfano kwenye nchi kumi za Afrika katika
ukanda wa magharibi mwa Bahari ya Hindi ambazo zinakabiliwa na changamoto
za uhifadhi kama ilivyo kwenye mto Mbarali.
Hayo yameelezwa na kiongozi wa Sekretarieti ya Azimio la Nairobi, Dixon
Waruinge wakati alipokuwa akifafanua kuhusu umuhimu wa Mradi wa EFLOWS
pamoja na lengo ya ziara yao ya tathimini toka mradi huo kuanza kwa Mkuu wa
Wilaya ya Mbarali Kanali Denis Filangali Mwila na maafisa wengine kutoka Ofisi ya
Makamu wa Raisi Mazingira.
Amesema kuwa utaalamu wa kuhifadhi maji kwenye mito haupo kwenye nchi
nyingi za Afrika ya Mashariki na hivyo ikaonekana uanzishwe mradi huo ambao
utasaidia kuongeza elimu na ufahamu juu ya taaluma hiyo.
“kazi kubwa inayofanywa na watafiti hawa hapa Tanzania siyo kazi ya Tanzania
peke yake japokuwa inafanyika Tanzania ni kazi ya nchi kumi, elimu bora
tutakayoitoa hapa ni lazima tuieneze kwa nchi nyingine ili tukaseme kuwa
inawezekana kwasababu watanzania wameweza na wametuonyesha njia na uzuri
ni kuwa Prof. Japhet Kashaigili ni mmoja ya wale wanaoeneza elimu hiyo, hivyo
tumpe nguvu hapa Tanzania elimu hiyo aipeleke nchi nyingine maana hata sasa
anahusika katika kazi kama hiyo huko Madagasca”, alisema Waruinge.
Akieleza sababu za kuchagua mto huo Mtafiti Mkuu wa Mradi EFLOWS kutoka
SUA Prof. Japhet Kashaigili amesema kuwa mto Mbarali ni mto ambao awali
ulikuwa ukitiririsha maji mwaka mzima lakini miaka ya karibuni mto huo umeanza
kukata maji hivyo kuna maswali ya kujiuliza ni nini kinapelekea hali hiyo.
“Hii hali imeleta changamoto ambayo tunajaribu kutafakari kwa sababu
tunaiangalia katika upana mkumbwa kwamba serikali ipo katika jitihada kubwa ya
uendelezaji wa miradi ya kimkakati kama nchi na moja ni Mradi wa Kufua Umeme
wa Mwalimu Nyerere ambapo bila maji mradi huu hauwezi kuwa endelevu na
mto Mbarali unachangia maji kwenye bwawa lile lakini sasa mto unakauka hasa
eneo la chini”, alieleza Prof. Kashaigili.
Prof. Kashaigili amesema miaka michache iliyopita Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan akiwa Makamu wa Rais aliunda kamati ya kitaifa ya kuangalia changamoto
hizo na yeye alikuwa ni mmoja wa wataalamu walitoa mapendekezo na maazimio
mengi ya mambo ya kufanya na hiki wanachofanya sasa ni sehemu ya kutekeleza
mapendekezo yale.
Aidha ameongeza kuwa mradi huo ni wa mfano kwakuwa wana ainisha athari
zitokanazo na shughuli za kibinadamu na jinsi ambavyo zinaathiri mtiririko wa
maji kwenye mito lakini pia wanaangalia namna ya kupunguza athari hizo kwa
kushirikiana na wadau wote walio kwenye maeneo hayo.
Amesema pamoja na utafiti wao, pia wameanzisha vitalu vya miche rafiki wa maji
ambapo miche 45,000 imeoteshwa na zoezi la kupanda linaendelea kwenye
vyanzo vya maji ambavyo vimeathirika na shughuli za kibinadamu pamoja na
kingo za mito ndani ya mita 60 kwenye maeneo mbalimbali ya Wilaya ya
Wanging’ombe lakini pia kwenye Wilaya ya Mbarali ili kurudisha uoto wa asili.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Kanali Denis Filangali Mwila
amepongeza kazi hiyo inayofanywa na watafiti hao kwa kushirikiana na Serikali
katika kusaidia kupatikana kwa ushahidi wa kisayansi unatokana na tafiti ili
kuweza kuyapa nguvu maamuzi yoyote yanayofanywa na Serikali katika bonde
hilo muhimu linalotegemewa na miradi ya kimkakati.
Aidha mkuu huyo wa Wilaya ya Mbarali amesema wao kama viongozi na Serikali
wanatambua umuhimu wa Bonde hilo kama chanzo kikubwa cha maji kuelekea
kwenye miradi mikubwa ya kufua umeme lakini pia wanatambua uhitaji wa maji
kwa wananchi katika kufanya shughuli za kilimo lakini maamuzi yoyote
yanayofanywa yazingatie maslahi mapana ya Taifa kiuchumi na sio watu
wachache ambao wanaweza patiwa maeneo mengine ya kufanya kilimo na
wakaendelea kuishi na kustawi.
“ Sisi kama Serikali ya wilaya tupo tayari kutoa ushirikiano wa hali na mali katika
kuhakikisha matokeo ya utafiti huu yanapatikana na utaalamu wake unatumika
katika kufanya maamuzi sahihi kuhusu bonde hili na mito yake na hapa
ningependa kuomba wataalamu wetu mtoe ushauri vyema, mfano swala la watu
kuondoka kwenye bonde lilikuwa wazi lakini baadae likatolewa tamko la kuwacha
walime kwa mwaka mmoja ndio waondoke lakini mimi natamani tunapoamua
kufanya maamuzi magumu tufanye maamuzi magumu kwa faida na maslahi
mapana ya taifa letu”, alifafanua Mhe. Kanali Mwila.
Aidha amesema kauli hiyo inaweza kuleta athati kubwa zaidi kwenye eneo hilo
kwani kwakuwa wanajua wameambiwa walime msimu mmoja ndio waondoke
wanaweza kuongeza maeneo ya kilimo ili wavune zaidi kupata faida kubwa lakini
matokeo yake uharibifu ukawa mkubwa kwakuwa wanajua wanaondoka.
Mradi huu wa Utafiti unatekelewa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)
na kutekelezwa katika bonde la mto Rufiji ndani ya dakio la mto Mbarali kwa
ushirikiano na Bodi ya Maji ya mto Rufiji, jumuiya za watumia maji, Wakala wa
Huduma za Misitu (TFS), Wilaya ya Mbarali na Wanging`ombe na jamii, kwa
ufadhili wa program ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa, UNEP na kutekelezwa
Kiongozi wa Sekretarieti ya Azimio la Nairobi, Dixon Waruinge akisisitiza jambo wakati wa ziara yake kutembelea maeneo ambayo yanatekeleza kazi mbalimbali za utafiti wa mradi wa EFLOWS.

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Kanali Denis Filangali Mwila akisisitiza jambo mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa EFLOWS katika Wilaya yake.

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Kanali Denis Filangali Mwila akisisitiza jambo mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa EFLOWS katika Wilaya yake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Mwl. Missana Kwangura akieleza mikakati ya Halmashauri yake katika kuunga Mkono juhudi za Mradi huo katika uhifadhi wa vyanzo vya maji na mito.

Mkurugenzi Msaidizi wa Ofisi ya Makamu wa Raisi Mazingira Bw. Thomas Bwana kitoa salamu za Mkurugenzi ofisi ya makamu wa Raisi Mazingira wakati wa kikao cha pamoja na Jumuiya ya MBUMTILU.

Watafiti wa mradi wa EFLOWS, Maafisa kutoka Ofisi ya Makamu wa Riasi Mazingira, Maafisa kutoka Sekretarieti ya Azimio la Nairobi, na Jumuiya ya watumia maji ya MBUMTILU wakijadiliana jambo wakati wakiangalia moja ya chanzo cha maji kilichoharibiwa na shughuli za binadamu na sasa kimepandwa miti rafiki wa maji kurudisha uoto wake wa asili.
No comments:
Post a Comment