Waziri Jafo, Benki Ya Exim na Wadau Wa Habari Waadhimisha Mapinduzi Ya Zanzibar Kwa Upandaji wa Miti Dodoma - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, January 13, 2023

Waziri Jafo, Benki Ya Exim na Wadau Wa Habari Waadhimisha Mapinduzi Ya Zanzibar Kwa Upandaji wa Miti Dodoma

 

Waziri Jafo, Benki Ya Exim na Wadau Wa Habari Waadhimisha Mapinduzi Ya Zanzibar Kwa Upandaji wa Miti Dodoma.

Dodoma: Januari 11, 2023; Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo ameungana na Benki ya Exim Tanzania na wadau wa habari mkoani Dodoma katika zoezi la upandaji miti kwenye soko la Machinga Complex jijini humo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar sambamba na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Mkakati huo wa upandaji miti kwenye soko hilo ambao umedhaminiwa na Benki ya Exim na kuratibiwa na Taasisi ya Habari Development Association ni sehemu ya mpango wa upandaji miti 6000 katika maeneo mbalimbali jijini humo ikiwemo pia eneo la Hospitali ya Mirembe na Shule ya Msingi Uhuru ya jijini humo.

Akizungumza mara tu baada ya kuongoza zoezi la upandaji miti kwenye soko hilo, Waziri Jafo alisema Wizara yake kwa kushirikiana na wadau hao imejipanga kutumia vema Maadhimisho ya Miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendesha jitihada mbalimbali za utunzaji mazingira hususani kwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali nchini.

“Tukiwa kwenye mkakati huu muhimu tunaguswa zaidi kuona kwamba wenzetu Benki ya Exim wameamua kuungana na serikali ili kufanikisha zoezi hili muhimu ambalo ni sehemu ya Maadhimisho ya miaka 59 tangu kufanyika kwa Mapinduzi Zanzibar…tunawashukuru sana Benki ya Exim kwa kuwa ‘wanaupiga mwingi’ katika jitihada mbalimbali za utunzaji mazingira hususani katika jijini hili la Dodoma’’ alisema.

Kwa mujibu wa Waziri Jafo, taifa kwasasa linapitia changamoto nyingi zinazotokana na athari ya mabadiliko ya tabia nchi na hivyo kusababisha upungufu wa mvua kwa karibu nusu ya kiwango kilichozoeleka. Hali hii imesaababisha upungufu wa uzalishaji wa chakula, upatikanaji wa huduma ya maji, ukosefu wa umeme wa uhakika na hivyo kusababisha mporomoko wa uchumi.

“Hata hivyo serikali inaendelea na miradi mbalimbali inayolenga kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa, kuchimba mabwawa makubwa ya kuhifadhi maji sambamba na mradi wa uzalishaji umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, zote hizi zikiwa ni jitihada za kuhakikisha kama taifa hatuathiriki sana na changamoto hii,’’ alisema.

Kwa upande wake Ofisa Mkuu Idara ya Fedha (CFO) Benki ya Exim Shani Kinswaga alisema benki hiyo imekuwa ikiunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kuja na namna mbalimbali ikiwemo kupitia Program yake ya ‘Exim Go Green Initiative’ kwa kuhamasisha upandaji wa miti na utunzaji mazingira nchini kupitia matawi yake yaliyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

“Kwa upande wa ukanda huu wa kati, jiji hili la Dodoma limebahatika kuwa chaguo la Benki ya Exim katika kuendesha Programu hii. Zoezi hili la leo ni zoezi la tatu kwa benki ya Exim kushiriki katika kipindi cha miaka mitatu ndani ya mkoa huu wa Dodoma tukiwa tayari tumedhamini upandwaji wa miti zaidi ya zaidi ya 20, 000 katika maeneo mbalimbali,’’ alisema.

Kwa mujibu wa Bw Kinswaga, benki hiyo kama taasisi ya fedha nchini inaguswa pia na chanagmoto za kiuchumi zinazotokana na athari ya mabadiliko ya tabia nchini hivyo imedhamiria kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazolenga kukabiliana na changamoto hiyo.

Awali akizungumza kwenye tukio hilo, Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Habari Development Association Bernard Mwanawile alisema taasisi yake imejipanga kupanda miti milioni 1 mkoani humo huku akipongeza wadau mbalimbali wanaounga mkono mpango huo ikiwemo benki ya Exim ambayo hadi sasa imeweza kufadhili upandwaji wa miti 16,000 kupitia taasisi hiyo pekee.

Naye Meneja wa Soko la Machinga Complex Bi Veronica Tarimo aliahidi kuhakikisha kwamba soko hilo na wadau wake wote wakiwemo wafanyabiashara wadogo wanaofanya biashara zao kwenye soko hilo wataitunza vema miti hiyo sambamba na kuendelea na mkakati wao wa utunzaji mazingira katika soko hilo.

“Zaidi tu niseme kwamba kwa kuwa Benki ya Exim imeonesha nia ya kushirikiana na wamachinga nasi pia tunaiomba benki hii iweke kambi kwenye soko letu ili itoe elimu ya kifedha kwa wafanyabiashara hawa ili waweze pia kupatiwa mikopo nafuu kutoka benki ya Exim,’’ alisema.Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mh Selemani Jafo (Kulia) akishuhudia  Ofisa Mkuu Idara ya Fedha (CFO) Benki ya Exim Shani Kinswaga (wa pili kulia), Meneja Masoko na Mawasiliano wa Benki hiyo Bw Stanley Kafu (katikati) na Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Habari Development Association Bernard Mwanawile (kushoto) wakipanda miti kwenye soko la Machinga Complex jijini Dodoma mapema hii leo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar sambamba na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.  Kupitia mkakati huo, Benki ya Exim imefadhili upandaji wa miti 6000 katika maeneo mbalimbali jijini humo. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad