Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
Imeelezwa kuwa takwimu za kuandika na kutunza wosia nchini ni ndogo licha ya kundi kubwa la Wazee kuwajibika zaidi katika uandishi na utunzaji wake.
Kundi kubwa la Wazee limetajwa kuwajibika zaidi katika kuandika na kutunza wosia pindi wawapo hai ili kuepusha migogoro ambayo inaweza kutokea katika familia wakati wa ugawaji wa mali kwenye familia hizo pindi wao wakiwa wamefariki dunia.
Akizungumza na Michuzi Blog katika Banda la RITA kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Wakili wa Serikali Peter Mbogoro amesema idadi kubwa ya Wazee inafika RITA kuandika wosia tofauti na idadi ya vijana licha ya kuwa jukumu la kuandika na kutunza Wosia ni la kila mtu aliyetimiza miaka kumi na nane na mwenye akili timamu.
“Wosia ni maneno ambayo yatakusimamia wewe wakati ambao haupo duniani na pia maneno hayo yataepusha migogoro katika familia endapo familia hiyo husika itafuata maelekezo ya wosia huo ulioachwa na marehemu”, amesema Wakili Mbogoro.
Wakili Mbogoro amesema wosia unasaidia katika ugawaji wa mali za marehemu wakati amefariki dunia, pia amesema wosia unaweza kutoa maelekezo ya mazishi pindi ambapo mtu huyo amefariki dunia, huku akisisitiza kuwa wosia una msaada mkubwa hasa katika kuepusha migogoro ambayo inaweza kutokea mtu anapofariki.
Hata hivyo, Wakili Mbogoro amebainisha taratibu za kupata Cheti cha Kuzaliwa na Cheti cha Kifo. Amesema ili kupata cheti cha kuzaliwa mwombaji anapaswa kuwa na Tangazo la Kizazi toka kituo cha tiba alichozaliwa mtoto, kadi ya kliniki ya mtoto, cheti cha ubatizo, kadi ya mpiga kura/kadi ya uraia, pasi ya kusafiria, cheti cha kumaliza elimu ya msingi na elimu ya sekondari (leaving certificate).
Upatikanaji wa Cheti cha Kifo, Wakili Mbogoro amesema lazima kuwepo kibali cha mazishi endapo marehemu atakuwa amefariki hospitali, endapo marehemu atakuwa amefariki nyumbani, inatakiwa muhtasari wa kikao cha Familia utakaomtambulisha Msimamizi wa Mirathi ambaye atatakiwa kuja na barua ya utambulisho kutoka kwa mtendaji kata Mahali alipofia marehemu.
.jpeg)
No comments:
Post a Comment