Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.
Philip Mpango ametoa wito kwa Mahakama na mfumo wa utoaji haki kwa
ujumla kuongeza juhudi katika kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo suala
la Rushwa katika vyombo vya utoaji haki pamoja na suala la upelelezi
kuchukua muda mrefu.
Makamu wa Rais amesema hayo mara baada ya Matembezi ya Uzinduzi wa
Wiki ya Sheria yaliofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere (Nyerere
Square) Jijini Dodoma leo tarehe 22 Januari 2023. Amesema yamekuwepo
malalamiko katika maeneo ya minada ya mifugo inayokamatwa kwenye
hifadhi kuzuiwa au wahusika kutozwa faini ndogo, fedha za kigeni
zilizokamatwa mipakani kupotea mikononi mwa mahakama na hukumu
kupindishwa ili kumpa ushindi mwenye fedha.
Aidha Makamu wa Rais ametoa rai kushughulikiwa kwa malalamiko ya
gharama kubwa za uendeshaji wa kesi na kulipia gharama za mawakili,
hukumu kuandikwa kwa lugha ya kiingereza, watuhumiwa kukaa mahabusu
muda mrefu kusubiri uchunguzi kukamilika pamoja na ukosefu wa elimu ya
sheria kwa umma. Amewaasa wahusika katika mfumo wa utoaji wa haki
kuendelea kutoa elimu kwa umma na kuhakikisha huduma mbadala ya
usuluhishi inapatikana na kufikika kwa urahisi.
Katika nyingine Makamu wa Raais ametoa wito kwa Mahakama kushirikiana
vema na wadau katika kuimarisha utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi
ili kuweza kufikia malengo yake kirahisi. Amesema mawakili wa kujitegemea
wanapaswa kujielekeza katika kutoa elimu na ushauri sahihi kwa wateja wao
kuhusu namna bora ya kutatua migogoro ikiwa ni pamoja na kutumia njia
mbadala ya usuluhishi badala ya kuendelea na kesi mahakamani ambako
watalipwa gharama kubwa zaidi za kuwatetea.
Makamu wa Rais ameziasa asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali
kuendelea kutoa elimu kwa umma, misaada kwa wananchi na kujenga uelewa
kuhusu haki za msingi za kiraia na umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia
ya usuluhishi. Vilevile Makamu wa Rais ametoa wito kwa viongozi wa dini na
viongozi wa mila kote nchini kuisadia Mahakama kuzungumza na wananchi
kuhusu umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.
Dkt. Mpango ameagiza kuangaliwa upya ufanyaji kazi wa mabaraza ya ardhi
nchini kutokana na kuongezeka kwa migogoro ya ardhi inayokosa usuluhishi
wa mapema.
Makamu wa Rais ameongeza kwamba Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu imeendelea kuhakikisha Mahakama
inakuwa na miundombinu bora, watendaji wa kutosha, pamoja na mazingira
wezeshi ya kutekeleza majukumu yake ya msingi ikiwemo kuhakikisha
Mahakama inapata fedha za matumizi ya kawaida, fedha za maendeleo za
ndani na pia kukopa mikopo ya masharti nafuu ili kutekeleza miradi ya
maboresho ya Mahakama ikiwemo ujenzi wa majengo ya Vituo Jumuishi vya
Utoaji Haki (6) (Integrated Justice Centres), Mahakama za Wilaya (25),
Mahakama ya Hakimu Mkazi (1) na Mahakama za Mwanzo (6). Vilevile
amesema ili kuongeza ufanisi na kukidhi mahitaji, Mheshimiwa Rais
ameshateua jumla ya Majaji 52 (Mahakama ya Rufani 9 na Mahakama Kuu
43) na kuagiza Wizara ya Mawasiliano, TTCL pamoja na eGA kuhakikisha
kuwa Mahakama inapatiwa “Bandwidth” ya kutosha ili kuendesha shughuli
zake kwa kutumia Tehama.
Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Prof. Ibrahim Hamis
Juma ametoa wito kwa wananchi wanaohitaji kudai haki zao kuhakikisha
wanafahamu kwanza haki hizo kwa kusoma na kutafuta elimu itakayowezesha
kufahamu sheria na taratibu zinazoongoza haki inayotafutwa.
Amesema Wiki ya sheria itatumika katika kutoa elimu na kuwakumbusha
wananchi namna ya kupata haki zao kwa njia sahihi na rahisi. Amesema wiki
hiyo pia itatumika kuonesha namna mahakama inavyotumia teknolojia katika
kufanya shughuli zake. Prof Juma ameongeza kwamba kwa matumizi ya
Tehama, haki inayotolewa mahakamani itakua shidani na haki bora na
iliyowazi kwa wananchi na wale watakaofika mahakamani.
Wiki ya Sheria imeanza rasmi leo tarehe 22 Januari 2023 na inatarajiwa
kuhitimishwa tarehe 1 Februari 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibarahim Juma, Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdallah, Viongozi na Watumishi mbalimbali wa Mahakama pamoja na Viongozi na wananchi wa Mkoa wa Dodoma wakati akiongoza Matembezi ya Uzinduzi wa Wiki ya Sheria yalioanzia katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Haki (IJC) na kumalizika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere (Nyerere Square) leo tarehe 22 Januari

No comments:
Post a Comment