BURIANI MCHUNGAJI SABINA LUMWE - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, January 12, 2023

BURIANI MCHUNGAJI SABINA LUMWE

 

Adeladius Makwega-Buigiri

Siku hiyo alifika ofisini afisa elimu maalumu anayefahamika kama Stephern Shemdoe na Halmashauri ya Lushoto ilimpa jukumu la kusimamia shule zenye wanafunzi wanaohitaji msaada maalumu ambazo zilikuwa za kuhesabika.

Wakati huo agizo la serikali ya awamu ya tano lilikuwa ni kuweka mikataba maalumu na shule zile zinazomilikiwa na taasisi za binafsi zenye kutoa huduma kwa watoto wenye mahitaji maalumu. Mwalimu Shemdoe alimjulisha mwanakwetu kuwa wilaya nzima ya Lushoto ina shule moja tu yenye sifa hiyo inayomilikiwa na Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ambapo kazi ya kuwatafuta watoto wenye mahitaji maalumu ilikuwa ikifanywa kwa ushirika wa dhehebu hilo na serikali ya wilaya. Maana utamaduni uliokuwepo familia nyingi ziliwaficha watoto wa namna hiyo hivyo kuwapata watoto wenye sifa hiyo kwa darasa la kwanza ilikuwa kazi kubwa.

Mikataba hiyo baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na taasisi hizo ilisaidia walimu na watumishi wengine wenye ajira ya serikali kupangwa hapo na shule hizo kupata ruzuku ya uendeshaji wake kulingana na idadi ya wanafunzi waliowapokea. Kinyume chake shule hizo zilijiendesha kwa kutegemea wafadhili au sadaka za washirika wao za kila jumapili kanisani ambazo ni chache na hazina uhakika maana mambo ni mengi.

Zoezi hilo lilimkutanisha mwanakwetu na baadhi ya viongozi wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki akiwamo Baba Askofu Stephern Munga, Mchungaji Mwinuka na mwanasheria wao. Mwanakwetu aliwaambia kuwa sintoweza kusaini mkataba na taasisi nisiyoifahamu naomba niitembelee shule hii kwanza.

Hapo Shule ya Msingi Irente mwanakwetu alikaribishwa na watoto wenye mahitaji maalumu wenye albinism, wenye uone hafifu na wengineo na mbele yake hapo wakaimba nyimbo kadhaa ikiwamo Tanzania Tanzania, Mungu Ibariki Tanzania na
nyingine nyingi.

Baadaye mkataba huo ulisainiwa na upande wa Serikali ukiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga wakati huo Bi Zena Said(Sasa ni Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar), mwanakwetu, Afisa Elimu wa Wilaya ya Lushoto wakati huo Mwalimu Adam Shemnga na upande wa Dayosisi hiyo.

Eneo la Irente lilikuwa na miti mingi mkubwa ya asili na ya kupandwa, ngombe kadhaa wa maziwa na wa kufungwa walizunguka katika eneo tambalale na kando ya eneo hilo tambalale palikuwa na kanisa moja dogo ambalo mwanakwetu aliambiwa kuwa ndilo linalotoa huduma za kiroho kwa jamii ya Irente na shule hii.

Ndani ya kanisa hilo mwanakwetu alitambulishwa kwa mchungaji Sabina Lumwe akiwa mama mmoja wa makamu. Hapo mwanakwetu alizungumza mambo kadhaa na baadaye mchungaji Sabina kumuonesha kitabu chake alichokiandika kilichopewa jina “My Marriage Are Not Start Yet.”


Baada ya safari hiyo mwanakwetu walishirikiana na mchungaji huyu katika mambo kadhaa ya kimaendeleo ambapo yapo yaliyokamilika na yapo ambayo hayakukamilika huku nia ya kuyafanya ilikuwapo kwa pande zote mbili.

Baadaye mwanakwetu aliondoka Lushoto na hata Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ikapata Askofu Mpya Baba Askofu Msafiri Mbilu, huku mchungaji Sabina Lumwe aliendelea na kazi yake hiyo katika kanisa hilo lililo umbali mchache na Jengo la Halimashauri ya Wilaya ya Lushoto. Mwaka wa 2023 ulianza vizuri na juma la kwanza kuelekea la pili la mwezi wa Januari mwanakwetu alipewa taarifa ya msiba wa
Mchungaji Sabina Lumwe hiyo ikiwa ni kazi ya Mungu na mara zote haina makosa.

Januari 10, 2023 Baba Askofu Msafiri Mbilu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki aliongoza Ibada ya mazishi ya Mchungaji Sabina Lumwe huku akibainisha wazi kuwa Mchungaji Sabina ni miongoni mwa Wachungaji watatu wanawake wa mwanzo wa kanisa lao kupewa daraja hilo na huku Mchungaji Sabina akiwa mwanamke wa kwanza kusomea teolojia katika dayosisi yao mwishoni mwa miaka sabini.

“Mchungaji Sabina alikuwa miongoni mwa wachungaji waliojitolea maisha yao kwa ajili ya wengine, alifanya hivyo kwa kuwa hayo ndiyo maisha yake aliyoyachagua kwa ajili ya yatima, wasio jiweza na alikuwa na maono ya kuwaungasha wanawake.” Askofu Mbilu alisisitiza.

Ibada hiyo ya mazishi ambayo mwanakwetu aliifuatilia alishuhudia Baba Askofu Mbilu akizionesha kazi mbalimbali zilizofanywa na mama huyu huku waombolezaji kadhaa wakiwamo wachungaji aliowahi kufanya nao kazi wakishuhudia.

Mchungaji Sabina Lumwe alizaliwa Julai 21, 1960 Kijiji cha Lutindi , Korogwe Mkoa wa Tanga, akiwa mtoto wa pili wa familia ya Baba Mwageni Mtunguja na Mama Julia Mtunguja. Mwezi mmoja baadaye yaani Agosti 1960 alibatiza na miaka 15 baadaye yaani 1975 alipata Kipaimara huko huko Lutindi Parish. Shule ya Msingi alisoma Lutindi hadi la saba na alijiunga na Shule ya Sekondari ya Wasichana na Kibosho na kuhitimu mwaka 1979.

Alipoitimu tu kidato cha nne aliunganisha mafunzo teolojia katika Chuo cha Makumira kwa ngazi ya astashahada na alihitumu mwaka 1983. Alipomaliza masomo yake alipangiwa majukumu katika usharika wa Lushoto na kwa kuwa wakati huo Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania lilikuwa halijaruhusu wanawake wawe wachungaji alifanya kazi kama mchungaji msaidizi. Mchungaji Sabina Lumwe hadi anafariki amemuacha mgane, watoto na wajukuu watatu.

Mwanakwetu anatoa pole kwa Baba Askofu Mbilu kwa kumpoteza Mchungaji wake, pole kwa wana Dayosisi ya Kaskazini Mashariki wote na pole kwa familia nzima ya Mchungaji Lumwe wa Lutindi na Lushoto Mjini.“N’tambo ntana Mchungaji Sabina Lumwe-Buriani Mchungaji Sabina Lumwe.”
Bwana ametoa, Bwana ametwaa, Jina lake lihimidiwe, amina.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad