WANANCHI WA VIJIJI VYA IDENDE NA UNENAMWA KUPATA MAJI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, December 21, 2022

WANANCHI WA VIJIJI VYA IDENDE NA UNENAMWA KUPATA MAJI

 


Na Muhidin Amri,
Makete

KERO ya maji safi na salama inayowakabili zaidi ya wakazi 1,704 wa kijiji vya Idende na Unenamwa kata ya Bulongwa wilaya ya Makete,inakwenda kumalizika baada ya wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kuwa katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa Idende-Unenamwa.

Mradi huo unatekelezwa na wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa),na unajengwa na mkandarasi kampuni ya M/S Ndika Engineers Ltd kwa gharama ya Sh.milioni 758 fedha kutoka serikali kuu na hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 80.


Meneja wa Ruwasa wilaya ya Makete Mhandisi Innocent Lyamuya amesema hayo jana, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa viongozi wa serikali ya kijiji cha Idende na viongozi wa kata Bulongwa waliotembelea ili kuona hali ya utekelezaji wake.

Lyamuya alieleza kuwa,kati ya Sh.milioni 758 zilizopangwa kutekeleza
wa mradi Idende,hadi sasa Ruwasa  wilaya ya Makete imepokea Sh.milioni 229 tu ambazo  zimetumika kulipa mkandarasi.


Kwa mujibu wa Lyamuya,mradi huo utakapokamilika hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika  vijiji hivyo itaongezeka kutoka asilimia 91 ya sasa hadi kufikia asilimia 100.

Aliongeza kuwa,mradi utakamilika  kati ya mwezi Mei na Juni mwakani na utakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa  vijiji hivyo viwili  ambao watakwenda kupata huduma ya maji safi na salama kwa masaa 24.

Lyamuya amesema,Ruwasa inaendelea kutekeleza miradi mipya sita ambayo iko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji wake  na baadhi ya miradi hiyo imeshaanza kutoa huduma kwa wananchi.

Aidha amesema,kwa mwaka wa fedha 2022/2023 wanatarajia kujenga miradi mipya 8 kati ya hiyo miradi 4 itajengwa na wakandarasi ambayo ni Kidope-Madiani,Usalimwani- Mfumbi,Ujuni -Mkenya,Ipepo na kata ya Ipelele.


Alitaja miradi  mingine itakayojengwa na wataalam wa Ruwasa ni mradi wa maji Utanziwa,mradi katika kituo cha afya Bulongwa,upanuzi wa mradi  wa maji  kijiji cha Tandala na  ukarabati wa miradi ya zamani katika tarafa ya Lupalilo ili kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kujenga,kufanya upanuzi na kukarabati miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Makete ambayo itakapo kamilika itamaliza kabisa changamoto ya huduma ya  maji katika wilaya hiyo.

Diwani wa kata ya Bulongwa Benaya Luvanda,ameishukuru serikali ya awamu ya sita kutoa fedha za ujenzi wa miradi ya maji katika kata ya Bulongwa yenye wakazi takribani 3,000 ambao wameanza kunufaika na miradi hiyo.

Amewapongeza wataalam wa Ruwasa wilaya ya Makete na mkoa wa Njombe, kwa  kazi nzuri ya ujenzi wa mradi huo ambao umetekeleza kwa vitendo dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake ya kumtua mama ndoo kichwani.

Amewaasa wananchi wa Bulongwa,kutunza miradi na kulinda miundombinu ya maji  inayoendelea kujengwa kwa fedha nyingi za serikali ili miradi hiyo iwe endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

Mkazi wa kijiji cha Idende wilayani Makete Magreth Mwalongo alisema,katika kijiji hicho changamoto kubwa ilikuwa  maji safi na salama ambapo  walilazimika  kutumia kati ya masaa 2 hadi 3 kwenda kutafuta maji kwenye mito na vyanzo vingine vya asili.

Ameiomba wizara ya maji,kuipatia fedha za kutosha Ruwasa  iweze kuendelea kujenga miradi ya maji na kupanua huduma zake kwa asilimia 100 ili wananchi wapate muda wa kujikita zaidi kwenye  kazi zao za uzalishaji mali.
Meneja wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilaya ya Makete mkoani Njombe Mhandisi Inocent Lyamuya kulia na Diwani wa kata ya Bulongwa Benaya Luvanda kushoto,wakimtwisha ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Idende wilayani Makete Magreth Mwalongo.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Makete mkoani Njombe Mhandisi Innocent Lyamuya katikati akiwa na viongozi wa kijiji cha Idende na kata ya Bulongwa baada ya kutembelea miradi ya maji inayotekelezwa na Ruwasa katika kijiji cha Idende wilayani humo.
Moja kati ya matenki ya kuhifadhi maji yaliyojengwa katika wilaya ya Mekete mkoani Njombe na wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kwa ajili ya kuhudumia wananchi.
 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad