WANANCHI WA KIJIJI CHA IKELU MAKAMBAKO WAMSHUKURU RAIS SAMIA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 26, 2022

WANANCHI WA KIJIJI CHA IKELU MAKAMBAKO WAMSHUKURU RAIS SAMIA

 


Na Muhidin Amri,
Makambako

WANANCHI wa kijiji cha Ikelu kata ya  Utengule Halmashauri ya mji Makambako mkoani Njombe,wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ahadi ya kuwajengea mradi  wa maji ambao  umemaliza kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema,kero ya maji safi na salama imewatesa kwa muda mrefu  kabla na baada ya kupata Uhuru hali iliyosababisha baadhi yao kushindwa kushiriki vyema kazi za maendeleo na ujenzi wa Taifa.

Wamesema,mradi huo ni ukombozi mkubwa kwa jamii ya wana Ikelu kwani  umemaliza mateso ya kutembea kati ya km mbili  hadi tatu kwenda kutafuta maji kwenye mito iliyopo kando kando ya kijiji hicho.

Mwenyekiti wa kijiji cha Ikelu Batson Nyagawa alisema,kijiji  hicho hakijawahi kupata maji ya bomba tangu kilipoanzishwa miaka ya 70,badala yake wananchi walitumia maji ya mito na visima  hivyo kuleta madhara makubwa kwa wananchi ikiwamo vifo  vilivyotokana na matumizi ya maji  ambayo hayakuwa safi  na salama kwa matumizi ya binadamu.

Amesema,ujenzi wa mradi huo umesaidia kupunguza baadhi ya magonjwa yanayotokana na  matumizi ya maji yasio safi na salama na kuokoa ndoa nyingi ikilinganishwa na siku za nyuma,kwani baadhi ya wanaume hawakuwa na imani na wake zao hasa wanapotumia muda mwingi kurudi nymbani kutoka kutafuta maji mtoni.

Kwa mujibu wa Nyagawa,tangu mradi ulipokamilika  kwa sasa hakuna wananchi hasa wanawake wanaotumia muda mwingi  kutafuta maji badala yake wanapata huduma hiyo kupitia vituo vya kuchotea maji vilivyojengwa kwenye makazi yao.

Diwani wa kata ya Utengule Stephano Mgoba,amewapongeza wataalam  wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) wilaya na mkoa wa Njombe,kwa usimamizi mzuri wa mradi huo na miradi mingine ambayo imemaliza changamoto ya upatikanaji wa maji katika vijiji mbalimbali vya kata ya Utengule.

Amesema,katika kijiji cha Ikelu suala la maji ya bomba wananchi walisikia kupitia vyombo vya habari,lakini  tangu serikali  ya awamu ya sita ilipoingia madarakani mwaka mmoja uliopita imefanikiwa kujenga mradi mkubwa na kumaliza kero ya maji  iliyokuwepo kwa muda mrefu.

Aidha amesema,ukosefu wa maji safi na salama katika kata hiyo ulipelekea hata wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kutopata chakula cha mchana,kukosa muda wa masomo darasani na baadhi yao kwenda shule wakiwa wachafu.

Kwa upande wake kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Njombe Bakari Kitogota alisema,mradi huo ulianza kutekelezwa miaka miwili iliyopita kwa kutumia mkandarasi kampuni ya M/S Business Network Ltd kwa gharama ya  Sh.bilioni 2.9 fedha  kutoka mfuko wa Taifa wa maji(NWF).

Kitogota amesema,hadi sasa mkandarasi amelipwa Sh.bilioni 1,942,578,330.20 na  fedha anazodai ni Sh.milioni 102,240,964.80 ambazo zitalipwa baada ya kumalizika kwa muda wa matazamio ya mradi  ambapo wakazi 3,796  wa kijiji cha Ikelu wanapata huduma ya maji safi na salama kwa masaa 24.

Naye katibu wa chombo cha watoa huduma ya maji  ngazi ya jamii(CBWSO) kijiji cha Ikelu Pascal Mlimila amesema,tayari kaya 130 sawa na asilimia 80 zimeingiza maji kwenye nyumba zao na zinapata huduma ya maji safi na salama.

Amesema,tangu chombo hicho kilipoanza kutoa huduma huduma ya maji hadi sasa wamefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh.milioni 5,960,200,hata hivyo changamoto kubwa  baadhi ya kaya hazijafikiwa na mtandao wa maji ya bomba.
Tenki lenye uwezo wa kuhifadhi takribani lita 150 za maji linalohudumia vijiji viwili vya Usetele na Mahongole Halmashauri ya Mji Makambako likiwa limekamilika.
Kaimu Meneja wa Ruwasa wilaya ya Iringa Mhandisi Bakari Kitogota katikati aliyevaa sweta,akiwaonyesha baadhi ya  wakazi na viongozi wa serikali ya kijiji cha Mahongole baadhi ya miundombinu  kwenye mradi wa maji unaohudumia zaidi ya wakazi 4411 wa vijiji vya Usetule na Mahongole Halmashauri ya Mji Makambako mkoani Njombe.
Diwani wa kata ya Utengule Halmashauri ya Mji Makambako wilayani Njombe Mheshimiwa Stephano Mgoba kulia,akimpongeza meneja wa Ruwasa mkoa wa Njombe Mhandisi Sadik Sakka kutokana na kazi nzuri ya utekelezaji wa miradi ya maji katika  vijiji mbalimbali vya kata hiyo,katikati kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Njombe Bakari Kitogota

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad