WAKUFUNZI MASUALA YA WENYE ULEMAVU WANOLEWA STADI ZA MAISHA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, December 13, 2022

WAKUFUNZI MASUALA YA WENYE ULEMAVU WANOLEWA STADI ZA MAISHA

 

 

 Na: Mwandishi Wetu – MWANZA
 
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imeendelea kutoa elimu ya Stadi za Maisha kwa wakufunzi na watendaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu ili kuwezesha vijana wenye Ulemavu nchini kuelewa njia sahihi za kushughulikia changamoto na mahitaji yao.
 
Akizungumza, wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo mkoani Mwanza, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana kutoka ofisi hiyo, Dkt. Mwiga Mbesi ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya vijana nchini ikiwemo kuwapatia mafunzo ya stadi za maisha yatakayo wawezesha kujitambua, kuhimili mihemko, kutatua matatizo na kufanya maamuzi.
 
“Vijana ndio nguvu kazi ya taifa na serikali inatambua mchango mkubwa walionao katika kukuza uchumi wa nchi, hivyo Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ilianzisha programu ya stadi za maisha ili kuwezesha vijana kujitambua,”
 
Ameeleza kuwa, vijana wenye Ulemavu wapo kwenye hatari zaidi ya kukabiliwa na matendo mbalimbali ya ukatili, hivyo mafunzo hayo yatajikita katika kuhakikisha elimu ya stadi za maisha inajumuishwa kwenye afua na programu za kushughulikia changamoto za vijana wenye Ulemavu.
 
Ameongeza kuwa, awali mwongozo huo wa stadi za maisha umetumika katika kuwajengea uwezo wawezeshaji wa kitaifa wa stadi za maisha 142 kwa kushirikiana na mamlaka za mikoa na serikali ambao wameweza kutoa mafunzo kwa waelimishaji rika 16,390 katika mikoa yote Tanzania bara. Waelimishaji rika hao wametoa mafunzo kwa vijana wapatao 655,600.
 
“Wakufunzi 26 mliopo katika mafunzo haya kama kila mmoja wenu atatoa elimu kwa waelimishaji rika 100 wenye ulemavu tutaweza kuwa na waelimishaji rika 2600, hivyo waelimishaji rika hao wakiweza pia kuwafikia vijana 50 kila mmoja tutakuza uelewa na elimu wa stadi za maisha kwa vijana 130,000 wenye Ulemavu,”
 
Amefafanua kuwa, Wawezeshaji wa kitaifa hivi sasa wapo 379 ikiwemo Maafisa vijana wa halmashauri (185), Maafisa Vijana wa Mkoa (26), Wakufunzi na watendaji kutoka taasisi zanazoshughulikia Watu wenye Ulemavu (26) ambapo idadi ya wawezeshaji hao watatoa mafunzo kwa waelimishaji rika na pia watatoa mafunzo kwa vijana ili ifikapo 2023 vijana wapatao 2,960,000 waweze kunufaika na mafunzo hayo.
 
Vile vile, Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa mwaka 2017 Ofisi ya Waziri Mkuu ilianza kufanya mapitio ya Mwongozo wa stadi za maisha wa mwaka 2009 lengo ikiwa ni kuhakikisha masuala mapya yaliyojitokeza katika duru za kitaifa, kikanda na kitaifa kwa ajili ya maendeleo ya vijana yanahuishwa kwenye Mwongozo.
 
Aidha, amewataka wakufunzi na watendaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu kuhakikisha elimu ya stadi za maisha inawafikia vijana wenye ulemavu ili waweze kujitambua, kuwa na uthubutu na kufanya maamuzi sahihi.
Pia, amewataka vijana kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali ikiwemo mikopo inayotolewa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na mikopo inayotolewa na halmashauri 4% kwa Vijana, 4% Wanawake na 2% kwa Watu wenye Ulemavu.
 
Naye, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma kwa Watu wenye Ulemavu, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Rasheed Maftah alieleza kuwa, mafunzo watakayopatiwa wakufunzi na watendaji kutoka kwenye taasisi zinazoshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu yatawezesha kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto zinazokabili Watu wenye Ulemavu nchini.
 
Kwa upande wa washiriki wa mafunzo hayo wameshukuru kupata elimu hiyo na wameahidi kutoa elimu hiyo kwa walengwa ili waweze kuwezesha kundi hilo kujitambua na kuona umuhimu walionao katika ujenzi wa maendeleo ya taifa.


Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana, Dkt. Mwiga Mbesi akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Stadi za Maisha kwa wakufunzi na watendaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu yaliyofanyika leo Disemba 12, 2022 koani Mwanza.

Afisa Maendeleo ya Vijana Mwandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bi. Diana Kasonga akitoa elimu wakati wa mafunzo hayo.Afisa Maendeleo ya Vijana Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Godfrey Massawe akitoa elimu wakati wa mafunzo hayo.Mwezeshaji Bw. Robert Semkiwa (aliyesimama kushoto) akifafanua jambo kuhusu stadi za maisha kwa wakufunzi na watendaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu. Kulia ni Mwezeshaji wa Stadi za Maisha kitaifa, Bi. Rhoda Kagogo (aliyesimama).Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma kwa Watu wenye Ulemavu, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Rasheed Maftah akieleza jambo wakati wa mafunzo hayo kuhusu Stadi za Maisha kwa wakufunzi na watendaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu yaliyofanyika mkoani Mwanza.

Washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia hotuba ya Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana, Dkt. Mwiga Mbesi (hayupo pichani) wakati wa hafla hiyo ya ufunguzi wa mafunzo ya Stadi za Maisha kwa wakufunzi na watendaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu yaliyofanyika mkoani Mwanza.No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad