Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WAFUGAJI Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wametakiwa kutunza ardhi kwa ajili ya manufaa ya watoto miaka ijayo hivyo wasijihusishe na kuiuza kwani hiyo ndiyo dhamana yao.
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kupitia Wilaya ya Simanjiro, Lenganasa Soipey ameyasema hayo kwenye harambee na uzinduzi wa kwaya ya Sayuni KKKT mtaa wa Oloshonyokie Naisinyai na kufanikisha kupatikana sh. Milioni 12.5.
Lenganasa amesema jamii ya wafugaji wasiwe na tamaa ya kuuza ardhi kwa watu wengine kwani eneo walilonalo ni dogo na ndiyo urithi wa watoto wao hivyo wasiuze.
“Msidhubutu kuuza ardhi yenu kwa shilingi, hii ardhi ina thamani kubwa mno muitunze kwa ajili ya watoto wenu kwani watakuja kunufaika nayo miaka ijayo,” amesema Lenganasa.
Hata hivyo, katika harambee na uzinduzi wa kwaya hiyo zilipatikana sh. Milioni 12.5 ambapo fedha taslimu ni sh. Milioni 9.7 ahadi zilikuwa sh. milioni 2.6 na dume moja la ng’ombe.
Lenganasa na mke wake walitoa mchango wa sh. Milioni 2.6 kwa ajili ya kuiunga mkono kwaya hiyo ya Sayuni ya KKKT Mtaa wa Oloshonyokie Kata ya Naisinyai.
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kupitia Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha, Siria Saibuli ambaye yeye binafsi amechangia sh. Milioni 2 kwenye harambee hiyo, ameisihi jamii kuendelea kumchangia Mungu.
“Unapotoa sadaka kwa Mungu ni kama umemkopesha hivyo tuendelee kuwa na moyo wa kutoa ili tufanikiwe kwenye mipango yetu ya maendeleo ya ufugaji, kilimo na madini,” amesema Siria.
No comments:
Post a Comment