WATU WENYE MAMLAKA YA UONGOZI ACHENI KUOMBA RUSHWA YA NGONO- KAMANDA MAGOMI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, December 18, 2022

WATU WENYE MAMLAKA YA UONGOZI ACHENI KUOMBA RUSHWA YA NGONO- KAMANDA MAGOMI

 

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Kamanda wa jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa polisi Janeth Magomi amekemea watu wenye mamlaka ya uongozi kutumia nafasi zao kutaka  rushwa ya Ngono.

Kamanda Magomi ameyasema hayo  wakati akizindua kampeni ya kupambana na rushwa ya ngono iliyofanyika katika uwanja wa CCM Kambarage Mjini Shinyanga.

Kampeni hiyo inaendeshwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Karibu Tanzania Organization (KTO) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) huku ikiwa imebeba ujumbe wenye  kauli mbiu isemayo ‘ Kuwa Jasiri Kataa Rushwa ya Ngono’ 

Amesema wapo baadhi ya watu wanaotumia vibaya mamlaka waliyonayo katika kutoa huduma za jamii , kwa kutaka rushwa ili kutoa huduma hizo, jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo hasa katika kukabiliana na vitendo vya ukatili na mapambano dhidi ya rushwa.

Kamanda Magomi amesema  rushwa ya ngono ni moja ya tatizo linaloonekana ,kuwa sehemu ya baadhi ya watu kutumia vibaya madaraka na nafasi walizonazo , kushawishi watu ili waweze kupata huduma na haki hizo, jambo ambalo ni ukatili unaopaswa kukemewa na kila mtu, kwa kupingwa kwa nguvu zote, kwani ni kinyume cha sheria.

Amesema matumizi mabaya ya mamlaka ni kuendeleza videndo vya ukatili ambapo ametaja athari za rushwa ya ngono huku akiwasihi wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuendelea kushirikiana na serikali kupitia idara zake kama vile jeshi la Polisi pamoja na TAKUKURU ili kutokomeza vitendo vya rushwa ya ngono.

“Rushwa ya ngono ni kitendo cha mtu mwenye mamlaka au madaraka kumshawishi mtu kutoa mwili wake kingono ili aweze kupata huduma au haki lakini sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya Mwaka 2007 inakataza mtu yoyote mwenye mamlaka kutumia mamlaka aliyonayo katika kutekeleza majukumu yake kwa kudai au kulazimisha upendeleo wa kingono”.amesema Kamanda Magomi

“Watu wenye mamlaka viongozi katika ngazi  mbalimbali kwenye jamii hutumia fursa hiyo kufanyia wanawake zuruma ya kingono lakini pia katika vyuo mashuleni walimu hushawishi wanafunzi kufanyanao ili wapate maksi za juu lakini katika vyombo vya sheria mtu hutakiwa kutoa rushwa ya ngono asaidiwe ili asichukuliwe hatua dhidi ya kesi inayomkabili”.amesema kamanda Magomi

“Rushwa ya ngono ni kitendo cha ukatili, athari zake rushwa ya ngono inaua kwani ni chanzo cha kusambaza magonjwa, pili rushwa ya ngono inazalilisha na kusababisha msongo wa mawazo tatu rushwa ya ngono inanyima haki za  wenye haki na kumpa haki asiyestahili nne rushwa ya ngono inasababisha Taifa kuwa na watumishi kwenye sekta na idara zote wasiostahili”.amesema kamanda Magomi kwenye uzinduzi wa rushwa ya ngono Mkoani Shinyanga

“Kunyamazia vitendo vya rushwa ya ngono ni kukuza na kueneza tatizo na hivyo kuongeza uzalilishaji na ukatili kwa watoto wetu, mama zetu, ndugu jamaa na marafiki wito weto kwa wananchi ni kuendelea kuvunja ukimya kupaza sauti ili kwa pamoja tuweze kutokomeza vitendo hivyo”. Amesema Kamanda Magomi

Mkurugenzi wa  wa shirika lisilo la kiserikali la Karibu Tanzania Organization (KTO) Maggid Mjengwa amesema uwepo wa vitendo vya rushwa ya ngono inatokana na mmomonyoko wa maadili pamoja na tamaa za kujipatia mali katika jamii.

Mjengwa amesema mmomonyoko wa maadili unaotokana na baadhi ya watu kutaka kujipatia mali kwa njia zisizo halali, hususani kuomba au kutoa rushwa ya ngono katika kupata au kutoa huduma kwa jamii, ni sababu inayochangia uwepo wa vitendo vya ukatili na rushwa ,jambo ambalo ni kikwazo cha maendeleo ya familia na Taifa kwa ujumla.

Amesema kuendelea kwa vitendo hivyo vinasababisha kuwepo kwa athari mbalimbali katika jamii hivyo kila mwananchi  anapaswa kupambana dhidi ya vitendo hivyo ili kuepuka athari.

“Watu kukosa maadili ndiyo moja ya chanzo cha vitendo vya rushwa kuna fikira katika jamii kwamba tendo likitokea anasema hilo halinihusu mimi nilakwao kwa mfano mtu anachukua pesa kwa rushwa na daraja anajenga kwa kiwango cha chini halafu unasema hilo jambo halinihusu ni kazi ya TAKUKURU  tubadilishe fikra tuepuke athari hizo”.amesema Mkurugenzi wa KTO Mjengwa

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii Manispaa ya Shinyanga John Tesha  amesema vitendo vya rushwa vinachangia utekelezaji mbaya wa miradi mbalimbali ya maendeleo Nchini ambapo amesisitiza kwa jamii  kutoa taarifa wanapobaini viashiria ama vitendo vya rushwa.

Tesha amesema vitendo vya rushwa vinachangia kurudisha nyuma shughuli za maendeleo katika jamii kutokana na kukosa  haki na huduma bora , na hivyo kuwataka wananchi kushirikiana na mammlaka zinazohusika, kutoa taarifa pindi wanapobaini viashiria ama vitendo vya rushwa  ili kutokomeza vitendo hivyo.

“Tukiwa na jamii ambayo inakataa rushwa maana yake hiyo ni jamii inayojitambua na ni jamii ambayo itakuwa na maendeleo tuendelee kusisitiza sehemu mbalimbali za kazi pamoja na maeneo mengine ya utoaji huduma rushwa isiwepo kama kuna yoyote basi fika sehemu husika ili jambo hilo liweze kushughulikiwa kwa haraka”.

“Maendeleo hayawezi kuwa endelevu kama kutakuwa na rushwa, rushwa inafanya mradi usiwe imara kwa maana mradi utachakachuliwa lakini kama hakuna rushwa huo mradi utakuwa imara na utatoa huduma iliyotarajiwa tuwaomba wananchi tuendelee kushirikiana katika kupambana na rushwa ya ngono”.amesema Bwana Tesha

Akizungumza kwa niamba ya Mwenyekiti wa bodi ya KTO ambaye ni mkuu wa chuo cha maendeleo ya wananchi Mtawanya (FDC) kilichopo Mkoa wa Mtwara Mshana Halfan amesema shirika hilo linaendeleo na jitihada mbalimbali za kukabiliana na mapambano dhidi rushwa ya ngono.

Halfan amesema vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi vimeendelea kushirikiana na (TAKUKURU) na kutoa elimu ya kupinga rushwa ya ngono kwa kuendesha Programu mbalimbali ikiwemo Programu ya Elimu Haina Mwisho ambayo ni Programu maalumu ya kuendeleza maarifa kwa wanawake vijana waliokatishwa masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito pamoja na wale ambao hawakupata nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari, watasoma masomo ya sekondari kupitia mfumo usio rasmi, masomo ya ufundi, ujasiriamali na stadi za maisha bure.

 Kwa upande wake Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Mwamba Masanja, amesema rushwa ya ngono siyo fursa ya kujinufaisha ambapo amewataka wananchi kutoa taarifa za rushwa ya ngono ili wahusika waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa lengo ni kutokomeza vitendo vya rushwa ya ngono.

Naye Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi, Maria Mkanwa amesema chuo hicho pamoja na vyuo vingine vya maendeleo ya wananchi kwa kushirikiana na KTO wameendelea  kutoa elimu ya kupinga rushwa ya ngono pamoja na kutoa Proramu mbalimbali kwa ajili ya kuwawezesha wananchi hasa kundi la wanawake.

Uzinduzi wa Kampeni ya Kupinga Rushwa ya Ngono umefanyika Jumamosi Desemba 17,2022 katika uwanja wa CCM Kambarage Mjini Shinyanga ukiambatana na utoaji wa elimu ya Rushwa ya Ngono kwa njia mbalimbali ikiwemo michezo ya Baiskeli ambapo washindi wote waliofanya vizuri katika michezo hiyo wamepewa zawadi.

 Kampeni ya kupambana na rushwa ya ngono imeandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Karibu Tanzania Organization  (KTO) kwa kushirikiana na Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Buhangija ambapo imekwenda sanjali na kauli mbiu isemayo “KUWA JASIRI KATAA RUSHWA YA NGONO”.


 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad