MAMLAKA YA BANDARI YAWAFUNDA WAANDISHI WA HABARI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, December 21, 2022

MAMLAKA YA BANDARI YAWAFUNDA WAANDISHI WA HABARI

 

Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Bagamoyo

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, (TPA) imeandaa semina maalum kwa waandishi wa habari  kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini wanaotoka kwenye mikoa yenye bandari kwa lengo la kuwajengea uelewa wa shughuli na majukumu yanayofanywa na na mamlaka hiyo.

Akizungumza leo Desemba 21, 2022, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA , Mhandisi Juma Kijavara amesema semina hiyo ni muhimu kwani itawasaidia waandishi wa habari kuwa na uelewa mpana wa masuala yanayohusu bandari.

 “Waandishi ambao mko hapa mmetoka kwenye mikoa ambayo tuna bandari zetu, Katavi, Kigoma, Mbeya, Mwanza, Mtwara, Tanga na Dar es Salaam. Tunataka mfahamu vizuri bandari zetu ili mnapoandika basi muwe mnaandika vitu sahihi,”amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mipango TPA, Dkt. Boniphace Nobeji amesema kama Mamlaka inayo mipango ya muda mrefu , mfupi pamoja na mafanikio mbalimbali huku akifafanua majukumu ya kuundwa kwa Mamlaka ya bandari nchini kuwa ni pamoja na kusimamia na kuvumisha bandari zao ili zitambulike na shughuli wanazofanya.

Pia kuendeleza bandari kimiundombinu , kusimamia usalama wa mali za wateja, usalama wa kiafya na kwamba kisheria wanaruhusiwa kuingia ubia kwa ajili ya kuboresha bandari.Kuhusu Bandari amesema wanazo jumla ya bandari 86 hadi sasa ambazo wanazisimamia, lakini ziko bandari ambazo hazijulikani  ambazo wanaendeela kuzifuatilia kwa ajili ya kuzitambua kisha kuzirasimisha.

“Pamoja na bandari zetu kubwa tunazo pia bandari ndogo ndogo lakini zipo nyingine ambazo zinatoa huduma lakini hazitambuliwi na Mamlaka, hivyo wajibu wetu ni kuzitambua ili zitoe huduma na sio lazima tuzisimamie sisi.” amesema

Kuhusu mipango mkakati ya kusimamia bandari hizo, ameeleza kuwa mpango mkakati wao huwa unaandaliwa kila baada ya miaka mitano na kwa sasa mpango uliopo ni wanne tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo.Akielezea maoni yao amesema ni kuhakikisha inakuwa Mamlaka inayotoa huduma bora kwa ukanda wa Afrika. Pia kuwa waadilifu, kufanya kazi kama timu, kuwajibika na kuwa wawazi.

“Tunayo malengo sita ukiondoa yale malengo ya msingi ambayo yanatakiwa kufanywa na kila mamlaka au taasisi ya Serikali. Tunataka kuwa na rasilimali endelevu hasa kwenye rasilimali watu na fedha."

Aidha amesema TPA imejipanga kupunguza rushwa kwa kuwa na uwazi katika shughuli zake lakini wanahimza vitendo vya kiuadilifu huku akisisitiza kuendelea kupitia bajeti zao ili kuwa na rasimali fedha.
Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Mrisho Mrisho akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali wakati wa semina ya waandhi wa vyombo mbalimbali iliyoandaliwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA).Semina hiyo imeanza jana  Desemba 20 na inatarajia kumalizika leo Desemba 21 mwak 2022.
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa kwenye semina iliyoandaliwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA) kwa waandishi wa vyombo vya habari nchini hasa wanaotoka kwenye mikoa inayotoa huduma za bandari.Mhariri wa gazeti la Jamhuri Denis Luambano(wa kwanza kulia) akiwa na waandishi wengine wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na maofisa wa TPA kuhusu shughuli zinazofanywa na  Mamlaka hiyo.Sehemu ya maofisa wa Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA) wakijadiliana jambo wakati wa semina hiyo. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad