KAMPUNI YA MABASI YA KILIMANJARO YAAMRIWA KULIPA FIDIA YA MILIONI 300 KWA KUSABABISHA KIFO CHA MWANAFUNZI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, December 21, 2022

KAMPUNI YA MABASI YA KILIMANJARO YAAMRIWA KULIPA FIDIA YA MILIONI 300 KWA KUSABABISHA KIFO CHA MWANAFUNZI

 MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeiamuru Kampuni ya Mabasi ya Kilimanjaro kulipa fidia ya Sh milioni 300  baada ya moja ya basi lake kuhusika kwenye ajali na kusababisha kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha tano Immaculate Kisena (16).

 Hukumu hiyo iliyoandaliwa na Jaji Leyla Mgonya aliyekuwa akisikiliza kesi imesomwa jana Desemba 21,2022 na 

 Msajili wa Mahakama Kuu, Joseph Luambano bila wadaiwa watatu ambao ni Kilimanjaro Truck Company Limited, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Rolinda Sawaya na Mjahidi Mohamed  aliyekuwa dereva wa basi hilo kutokuwepo mahakamani baada ya kukimbia kesi hiyo wakati walipotakiwa kufanya usuluhishi.

Akisoma hukumu hiyo  Luambano amesema mahakama imetoa ushindi kwa mdai hivyo wadaiwa kwa pamoja wanatakiwa kulipa fidia ya Sh milioni 300 kwa mdai baada ya kusababisha kifo, majeruhi na uharibifu wa gari na kwamba  watakapochelewesha malipo hayo watatakiwa kulipa riba ya asilimia saba kila siku  kwa mwaka mpaka kiasi hicho cha fedha kitakapolipwa

Aidha ameongeza kuwa wadaiwa pia watatakiwa kulipa gharama zote za kesi hiyo kwa mdai na kusema haki ya rufaa ipo wazi.

Akizungumza baada ya hukumu hiyo kutolewa, mdai ambaye ni baba mzazi wa marehemu, Immaculate, Leonard Kisena ameeleza kuwa, Desemba 24, mwaka jana akiwa na watoto wake wawili na mpwa wake walikuwa safarini kuelekea mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya na walipofika eneo la Kamala Bagamoyo saa 10:15 alfajiri basi la Kilimanjaro liliacha njia na kuwagonga na kusababisha kifo cha Immaculate hapo hapo.

Amesema, alifungua kesi hiyo ya madai namba 47, 2022  baada ya kupata ushindi katika Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani ambayo ilimtia  hatiani dereva (Mjahidi) katika kesi ya jinai kwa kukiri kuendesha gari hilo lenye namba za usajili T 278 ALQ aina ya Scania  bila kuwa na bima na kusababisha kifo, majeruhi Omenis Kabora na uharibifu wa gari aina ya Toyota Land cruiser lenye namba za usajili T 323 CWB .

Katika hukumu hiyo ya Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo, hakimu Mkazi Mfawidhi, Mwanakombo Mmanya aliamuru mshitakiwa  (Mjahidi) kulipa faini ya Sh 110,000 kwa mashtaka manne yaliyokuwa yanamkabili au kutumikia kifungo cha miezi sita jela.

Pia katika kesi hii ya Madai Kisena amewakilishwa na Wakili Dkt. Aloys Rugazia ambaye mbali na mambo mengine aliiomba mahakama kulipwa fidia ya Sh milioni 400  kutokana na  gharama mbalimbali walizotumia na kuwasilisha mahakamani nyaraka kuonesha gharama halisi za mazishi, uchunguzi wa mwili wa marehemu katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Rabinsia, gharama za matibabu kwa majeruhi na gari lililoharibika.

Pia waliomba fidia ya gharama za kumpoteza Immaculate katika ajali hiyo.

Akizungumza baada ya hukumu hiyo, wakili Rugazia amedai wakati wa maombi hayo Wakili wa wadaiwa, Michael Ngalo aliweka pingamizi mahakamani akidai kuwa Kampuni ya Kilimanjaro haimtambui dereva wala ajali iliyotokea.

Wakili Rugazia alidai mahakama iliwapa nafasi mdai na mdaiwa kuingia kwenye usuluhishi lakini hawakutokea licha ya mahakama kuwapa onyo mara tatu la kufika katika Kituo cha Usuluhishi.

Amedai baada ya wadaiwa kushindwa kutii wito wa mahakama, jalada la kesi hiyo lilirudishwa kwa Jaji Mgonya ambaye alitupilia mbali mapingamizi ya wadaiwa na kuamuru kesi isikilizwe kwa upande mmoja.

"Mteja wangu ameridhika na uamuzi wa mahakama kwamba ni wa haki licha ya kwamba bado ana majonzi ya kuondokewa na binti yake kwa kuwa alikuwa na watoto wawili na sasa yupo mmoja na  mkewe amepatwa na ugonjwa wa kudumu baada ya kupata mshtuko," amedai Wakili Rugazia.

Kwa upande wa mdai (Kisena), ameishukuru mahakama kwani imetenda haki, kama ilivyokuwa katika kesi ya trafiki Bagamoyo, "sisi kama familia tunaendelea kusikitishwa na kitendo cha wamiliki wa basi hilo kutokuwa na ubinadamu na uhai wa mtu kwa sababu tangu ajali ilipotokea hawakuwahi kuona mtu yoyote katika kampuni aliyefika nyumbani kwake au hata kupiga simu kutoa pole na wala hawakujishughulisha na sisi kwa namna yoyote ile, yaani ilikuwa kama hakuna kitu kilichotokea," amesema Kisena.

Amesema hakuwa hata na wazo la kufungua kesi hiyo ya madai lakini kitendo cha wadaiwa kutokuwa na ubinadamu na kuonyesha kutokujali kilimuuma sana na kumpelekea kufungua kesi ya madai kwani baada ya ajali ile wadaiwa walichokifanya ni kuondoa gari lao kituo cha polisi na kuendelea na biashara.
Wakili Dkt. Aloys Rugazia akizungumza na waandishi wa habari baada ya kusomwa kwa hukumu ya kesi ya madai ambapo Kampuni ya mabasi ya Kilimanjaro imeamriwa kulipa faini ya sh. Milioni 300 kwa basi lake moja lililohusika kwenye ajali na kusababisha kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha tano na madhara mengine. 
Leornad Kisena, baba wa marehemu aimmaculat, akiishukuru mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa kutoa uamuzi wa haki. Mahakama hiyo imeamuru Kampuni ya mabasi ya Kilimanjaro imeamriwa kulipa faini ya sh. Milioni 300 kwa basi lake moja lililohusika kwenye ajali na kusababisha kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha tano na madhara mengine.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad