DC SIMANJIRO AIPONGEZA GLISTEN KWA UFAULU MZURI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, December 23, 2022

DC SIMANJIRO AIPONGEZA GLISTEN KWA UFAULU MZURI

 

 Na Mwandishi wetu, Mirerani

MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dkt Suleiman Serera, amewapongeza wanafunzi, walimu, wazazi na mmiliki wa shule ya awali na msingi Glisten ya Mji mdogo wa Mirerani kwa ufaulu mzuri wa darasa la saba.

Shule ya awali na msingi Glisten imefaulisha wanafunzi wote 27 waliofanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu, kwa wastani wa A huku wanafunzi 10 wakichaguliwa kwenye shule za vipaji.

Dkt Serera akizungumza kwenye mahafali ya darasa la saba ya shule ya Glisten inayomilikiwa na Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Justin Nyari, amesema kufanya vizuri kwa shule hiyo ni sifa kwa Wilaya hiyo na Mkoa wa Manyara.

“Hongereni kwa ufaulu mzuri kwenye mwaka huu kwa wanafunzi wa darasa la saba kwani mmeonyesha juhudi kubwa na heshima kubwa kwa shule hii iliyopo kwenye wilaya ya Simanjiro,” amesema Dkt Serera.

Amewataka wazazi sasa kuacha kuwapeleka watoto nje ya nchi kusaka elimu kwani kuna baadhi ya shule kama hiyo ina walimu wazuri wenye kutoa elimu bora hivyo kuacha kasumba hiyo mara moja.

Serera amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan inajali sana elimu kwa vijana wetu hivyo basi ili kumuunga mkono wakati ufike kuacha kupeleka nje vijana kwa kuwa elimu inayotolewa hapa nchini ni bora zaidi.

Mmiliki wa Shule hiyo, Justin Nyari amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kukubali kuwa mgeni rasmi na pia yeye kama mmiliki wa shule hiyo na walimu kwa ujumla hawataweza kubweteka na ufaulu huo kwani ndiyo kwanza wataongeza jitihada zaidi.

Nyari amesema sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Serikali katika sekta ya elimu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan wanazizingatia na ndiyo maana kwa kiasi kikubwa wanafanya vyema katika kufaulisha wanafunzi.
 
Mmoja wa wazazi wa shule hiyo, Awadhi Masoud amemtaka mmiliki wa shule na walimu kuongeza jitihada zaidi za kutoa elimu bora kwa wanafunzi kwani kushika nafasi ya kwanza kiwilaya na Mkoa ni chachu ya wao kujipanga zaidi miaka yote ijayo.

 Amesema mwaka jana shule ilishika nafasi ya kwanza katika kumi bora kiwilaya na kimkoa na namba 15 kitaifa na mwaka huu imeshika nafasi ya kwanza kitaifa na kimkoa na 10 bora kitaifa imefanya vyema hivyo moto usiwe moto wa mabuwa uwe moto wa gesi wa kila miaka yote ijayo na siyo vinginevyo.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad