MELI KUBWA YENYE WATALII ZAIDI YA 1500 KUTOKA MAREKANI IMEWASILI NCHINI TANZANIA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 10, 2022

MELI KUBWA YENYE WATALII ZAIDI YA 1500 KUTOKA MAREKANI IMEWASILI NCHINI TANZANIA

MELI kubwa yenye watalii zaidi ya 1,500 kutoka Marekani imetia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam huku ikielezwa kwamba itakuwepo kwenye bandari hiyo kwa siku mbili na kisha itakwenda visiwani Zanzibari.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Amoss Nnko amesema  meli ya kitalii ya Zaandam mali ya Kampuni ya Holland America Line imewasili nchini asubuhi ya leo ikiwa na watalii 1060 ikiwa ni sehemu za safari za kitalii za meli hiyo.

Amesema meli hiyo ina wafanyakazi na wahudumu zaidi ya 500 na kwamba  ilianza safari yake siku 71 nchini Marekani katika jimbo la Florida na baada ya kuwasili Tanzania itaelekea Shelisheli.
 
"Baada ya kutiananga kwenye bandari ya Dar es Salaam itakaa hapa nchini kwa siku nne ambapo Tanzania Bara itakaa siku mbili na Zanzibar itakaa siku mbili.Ujio wa meli hii unachochea jitihada za kukuza utalii nchini na ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa katika kutangaza vivutio vilivyopo Tanzania,"amesema Nnko 

Aidha amesema watalii hao kutoka Marekani wametembea katika nchi kadhaa na sasa ni zamu ya Tanzania ambapo pamoja na kwenda katika hifadhi ya Selous, watatembelea mji wa kihistoria Bagamoyo na kuzunguka jiji la Dar es Salaam.

Wakati huo huo Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mathew Antony amesema ni mafanikio kwa bandari hiyo kuendelea kupokea meli kubwa ikiwa ni matokeo ya uboreshaji wa miundombinu.

Amefafanua kwamba imezoeleka bandari ya Dar es Salaam huwa inahudumia  meli za mizigo pekee, lakini ukweli hata hizi za watalii wanazihudumia na
 wanaomba wadau wengine kupeleka meli zao kwani miundombinu ni mizuri na wanaendelea kuboresha.

Kwa upande wake mmoja wa watalii hao Roseline Richard ameeleza kwamba ilikuwa ndoto yake kubwa kutembelea barani Afrika na hatimaye amefika Tanzania nchi inayosifiwa kwa ukarimu."Hakika ilikuwa ndoto yangu ya miaka mingi sasa imetimia na nimekuja Tanzania kwenye nchi nzuri inayosifika kwa watu wake kuwa wakarimu."

Meli ikiwasili katika Bandari ya Dar es Salaam. (PICHA ZOTE NA  EMMANUEL MASSAKA WA MICHUZI TV)
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Amoss Nnko akimkabidhi zawadi mtalii aliekuja na meli kubwa iliyokuja na watalii zaidi ya 1,500 kutoka Marekani leo kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Amoss Nnko akiteta jambo na watalii leo kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mathew Antony.
Kaimu Kamishina Msaidizi TANAPA,Hassan Nguluma.


PICHA ZOTE NA EMMANUEL MASSAKA WA MICHUZI TV

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad