HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, July 8, 2021

DKT KALEMANI AZINDUA ULIPAJI FIDIA BOMBA LA MAFUTA

 

Hafsa Omar-Tabora

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, amezindua rasmi Ulipaji wa Fidia kwa wananchi waliopisha mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).

Tukio hilo limefanyika, Julai 7,2021, katika kijiji cha Sojo, kata Igusule, Wilaya ya Nzega, Mkoani Tabora.

Katika hafla hiyo,pia ilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara Nishati, Kheri Mahimbali, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Batilda Buriani, Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Nishati na Madini,viongozi mbalimbali wa Wizara na Taasisi zake.

Akizungumza katika hafla hiyo, amesema zoezi la kulipa fidia kwa wale wote ambao wanastahili kupata fidia limeanza rasmi na watu wote watafidiwa kwa usahihi na kwa wakati.

“ kwasababu Serikali ni sikivu na inawajali wananchi wake wananchi wote ambao watafikiwa kwa namna yoyote ile na mradi huo wote watafidiwa kwasababu Serikali imetoa fedha za kutosha kwaajili ya malipo,” alisema Dkt. Kalemani.

Aidha, amesema gharama za fidia katika mradi mzima kutoka kyaka Mkoani kagera hadi Chongoleani Mkoani Tanga ni shilingi bilioni 28.26 za Kitanzania.

Amesema,Serikali imeamua kuzindua ulipaji wa fidia katika kijiji cha Sojo kwasababu eneo hilo lipo katikati baina ya  hoima Uganda na chongeleani Tanga na kuwataka wasimamizi wa mradi huo kujenga karakana katika eneo hilo kwakuwa karakana zinajengwa katikati ya mradi.

Ameeleza kuwa, wanufaika wa mradi huo watakuwa Watanzania wote kwa jumla lakini waliopitiwa na mradi watanufaika zaidi kwasababu fursa mbalimbali zitapatikana wakati wa ujenzi wa mradi katika maeneo yao na kuwataka wananchi hao kujitokeza kwenye kuchukua fursa mbalimbali za mradi.

Pia, amesema kutokana eneo hilo ndio linatumika kujenga kambi  wananchi wa eneo hilo watafaidika na ujenzi wa huduma za kijamii kama vile  kituo cha  afya, Shule na barabara ambazo zitajengwa mara baada ya ujenzi wa mradi kuanza.

Dkt. Kalemani, amewataka wananchi ambao watalipwa fidia zao kuanza kuondoka kwenye maeneo hayo ili ujenzi wa mradi uanze mara moja.

“ukishalipwa na pesa umepewa na ni haki yako, basi pisha mradi asije akatokea mtu akalipwa halafu akazitumia pesa zote baadae akasema pesa alizolipwa ni ndogo, kwahiyo tuheshimu malipo ya fidia na tuzitumie pesa kwaajili ya maendeleo,”alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Dkt. James Mataragio, amesema zoezi la ulipaji fidia lipo tayari kuanza kwa maeneo yote 12 ambapo timu za wawakilishi wa Serikali, wawakilishi wa Kampuni ya EACOP, Kampuni ya Uthamini (White Night) na Kampuni ya Ushirikishaji na Kusaidia Jamii (JSB) zipo katika baadhi ya Mikoa wakitekeleza shughuli za zoezi hilo.

Amesema, utwaaji wa ardhi umezingatia Sheria na Kanuni za ndani za uthamini na utwaaji wa ardhi,vilevile ili Mradi  uweze kukidhi vigezo vya kupata mikopo ya kimataifa, kumekuwepo na nyongeza ya manufaa mbalimbali kwa wananchi waliopisha mradi ikiwemo nyongeza ya fidia, kujengewa nyumba mbadala  za kisasa.

Ameongeza kuwa, mara tu baada kukamilika kwa taratibu jumla ya wananchi 391 waliopisha mradi watalipwa fidia ambapo wananchi waliopisha Mradi wapatao  44 wametoka kijiji cha Sojo ambao baadhi yao leo hii watasaini mikataba ya kulipwa.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizumgumza amezindua rasmi Ulipaji wa Fidia kwa wananchi waliopisha mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP). Julai 7,2021.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (kushoto) Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Nishati na Madini, Seif Gulamali(katikati) Naibu katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, wakiwa katika picha ya Pamoja mara baada uzinduzi wa Ulipaji wa Fidia kwa wananchi waliopisha mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), Julai 7,2021.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Dkt. James Mataragio, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Ulipaji wa Fidia kwa wananchi waliopisha mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), Julai 7,2021.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, akiwa Pamoja na viongozi mbalimbali na baadhi ya wananchi ambao wanatarajiwa kulipwa fidia.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani,akifurahiya ngoma Pamoja na viongozi mbalimbali wakati wa hafla uzinduzi wa Ulipaji wa Fidia kwa wananchi waliopisha mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), Julai 7,2021.


Picha mbalimbali katika hafla ya uzinduzi wa Ulipaji wa Fidia kwa wananchi waliopisha mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), Julai 7,2021.

 



1 comment:

  1. Awesome and interesting article. Great things you've always shared with us. Thanks. Just continue composing this type of post.

    ReplyDelete

Post Bottom Ad