Friday, October 18, 2019

ZAHANATI YA DUCE WABORESHA HUDUMA YA AFYA KWA MAMA NA MTOTO

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es  Salaam (DUCE) kimezindua jengo jipya la Afya ya uzazi na mtoto katika zahanati ya Chuo hicho leo Jijini Dar es Salaam.

Jengo hilo limezinduliwa na Mwakilishi  wa Mkuu wa Wilaya Temeke, Aimbora Aminiel Nnko litakalokuwa na uwezo wa kutoa huduma bora za Afya ya uzazi na mtoto.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo hilo, Aimbora amesema DUCE wamefanya jambo kubwa sana kwani afya ndiyo msingi mkubwa wa maendeleo katika taifa letu.

Aimbora amesema, zahanati ya DUCE imekuwa inatoa huduma nzuri sana kwa jamii inayowazunguka na hata yeye ni mmoja wa watu wanaofika kupata huduma hapo.

Amesema, kutanua wigo kwa kuweka huduma ya Afya ya uzazi na Mtoto itawasaidia kuanzia watumishi wa Chuo, wanafunzi na hata wananchi wanaokaa kwenye mazingira yanayowazunguka.

"Mmefanya jambo kubwa kutanua wigo wa huduma kwani ni jambo kubwa na la muhimu, kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya tunawapongeza sana na mmesema mnataka kuongeza hadhi ya Zahanati ninaamini hilo litafanikiwa kwa juhudi kubwa mnazofanya,"amesema Aimbora.

"Niwapongeze zaidi kwa kuunga mkono juhudi za Rais Dkt John Pombe Magufuli za kutekeleza na kujenga Zahanati ili wananchi wapate huduma nzuri, pia madaktari na waaguzi mnafanya kazi kubwa ya kutoa huduma bora ya Afya,"

Naye Mkuu wa Chuo Kishiriki RASI Prof Bernadeta Killian amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2018 hadi Juni 2019, zahanati ya DUCE imeweza kuwahudumia wagonjwa 15,138 wakiwemo wanafunzu, watumishi na wakaazi wanaozunguka maeneo hayo.

Amesema, kutokana na kukosekana kwa huduma ya afya ya uzazi na mtoto kwa wana DUCE na wanajamii wanaoishi jirani imewasukuma kujenga jengi hilo ili kuwezesha huduma inapatikana na kuongeza wigo na kipato kwa chuo.

"Jumla ya Milion 59 zimetumika kukamilisha jengo, Milion 41.7 zimetumika kukamilisha ujenzi wa jengo hilo na Milioni 17.3 kwa ajili ya kununulia thamani na zote zimetokana na mapato ya ndani ya chuo, "amesema Rasi Bernadeta.

"Chuo kina mikakati endelevu ya kuiboresha Zahanati ili iweze kutoa huduma bora zaidi ksa wanajumuiya ya DUCE na wananchi kwa ujumla na mikakati hiyo ikiwa ni kupandisha hadhi Zahanati kuwa kituo cha Afya, kuanzisha kamati ya Afya ya Chuo, kuifanya zahanati kuwa kliniki ya huduma za kibingwa na kutangaza huduma kwa watu wengi zaidi," 

Katika jengo hilo, Kumepatikana chumba kimoja cha Daktari kitakachotumika kutolea huduma za matibabu kwa wagonjwa wote, na itasaidia kupunguza changamoto ya vyumba.

Pia, kutakuwa na huduma ya ufuatiliaji wa ukuaji bora na wenye afya kwa watoto chini ya miaka mitano sambamba na utoaji wa chanjo kwa watoto hao hali kadhakika kutakuwepo na utoaji wa huduma rafiki kwa vijana.
Mkuu wa Chuo Kishiriki (DUCE) RASI Prof Bernadeta Killian akisoma hotuba kwa mgeni rasmi yw uzinduzi wa jengo jipya la Afya ya uzazi na mtoto katika zahanati ya Chuo hicho leo Jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi  wa Mkuu wa Wilaya Temeke, Aimbora Aminiel Nnko akitoa pongezi kwa Chuo Kishiriki DUCE kwa hatua kubwa waliyoifanya ya kujenga jengo jipya litakalokuwa na uwezo wa kutoa huduma bora za Afya ya uzazi na mtoto.
Mwakilishi  wa Mkuu wa Wilaya Temeke, Aimbora Aminiel Nnko akizindua jengo jipya la afya ya Mama na Mtoto litakalotoa huduma kwa watumishi wa Chuo Kishirikishi DUCE, wanafunzi na wakazi wa maeneo hayo.
Mwakilishi  wa Mkuu wa Wilaya Temeke, Aimbora Aminiel Nnko akipata maelezo kutoka kwa Mganga Mkuu wa Zahanati ya DUCE Dr Saning'o Sangeti baada ya kuzindua jengo jipya la Afya ya uzazi na mtoto katika zahanati ya Chuo hicho leo Jijini Dar es Salaam.
Naibu Rasi (Utawala)  Dkt  Method Semiono akitoa neno la Shukrani kwa Mwakilishi wa Mkuu ws Wilaya baada ya kuzindua jengo jipya la Afya ya uzazi na mtoto katika zahanati ya Chuo hicho leo Jijini Dar es Salaam.
Picha ya pamoja baada ya uzinduzi wa Jengo jipya la Afya ya uzazi na mtoto katika zahanati ya Chuo hicho leo Jijini Dar es Salaam.





No comments:

Post a Comment