Thursday, October 17, 2019

RAIS MAGUFULI KUWA MGENI RASMI UFUNGUZI WA MAONESHO YA UTALII (SITE)

Na Zainab  Nyamka, Globu ya Jamii

Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa maonesho ya Swahili International Tourism Expo (SITE) kesho Ukumbi wa Mlimani City.

Maonesho hayo yatajayoanza kesho Oktoba 18 yatamalizika Oktoba 20 mwaka huu yakitarajia kuwa na kampuni za waoneshaji 210 kutoka nchi 60, Jumla ya mawakala wa utalii na waandishi wa habari takribani 333.

Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof Aldof Mkenda amesema lengo la maonesho ya SITE ni kuwaunganisha wafanyabiashara wadogo na wa kati wa utalii Tanzania pamoja na wafanyabiashara kutoka masoko makuu ya utalii duniani.

Mkenda amesema, kwa mara ya kwanza maonesho hayo yalianza mwaka 2014, yakiandaliwa na Bodi ya Utalii Nchini (TTB) na yamekuwa yanakuwa kwa kasi kila mwaka.

Mkenda amewashukuru balozi za Tanzania nje ya nchi kwani wameweza kufanya kazi kubwa sana ya kufanya usaili wa mawakala wa utaliu pamoja na waandishi wa habari watakaoshiriki kwenye maonesho hayo kutoka nchi wanazosimamia.

"SITE imeendelea kupata mafanikio makubwa bapo ni jambo la kujivunia kama Wizara, wadau wa sekta ya utalii  na nchi kwa ujumla kuona onesho hili limeendelea kukua mwaka hadi mwaka na kuvutia washiriki wengi kutoka kila kona duniani," amesema Mkenda

Aidha, ameeleza kuwa TTB imeandaa ziara kwa ajili ya mawakala wa utalii na waandishi wa habari wa kimataifa Oktoba 21, kwenda kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vya asili ikiwemo Hifadhi ya Taifa Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro.

Maeneo mengine ni Fukwe za Tanga na mapango ya Amboni, Misitu ya Magoroto, Mlima Kilimanjaro na miradi ya utalii wa utamaduni katika Mkoa wa Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Riaha na Mji wa Iringa. Pia Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa na Mikumi, Visiwa vya Zanzibar na Mafia.

Pia, katika maonesho hayo kutakuwa na semina  zitakazoendeshwa na wataalamu waliobobea kwenye masuala ya utalii kukiwa na mada mbalimbali.

No comments:

Post a Comment