HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 10, 2018

TUMIENI CHUO CHA ARDHI TABORA KUPIMA MIJI NA VIJIJI VYENU-KABUNDUGURU

Na Tiganya Vincent
HALMASHAURI  za Wilayani Mkoani Tabora zimetakiwa kutumia wataalamu na wanachuo wa Chuo cha Ardhi Tabora ili kuhakikisha vijiji na miji yao inapimwa na kupagwa kwa ajili ya kuwa katika mpango wa matumizi bora ya ardhi. Hatua hiyo itasaidia kuepusha migogoro miongoni mwa wananchi na pia kuwawezesha kutumia maeneo yao kujiletea maendeleo ikiwemo kukopa fedha katika Taasisi mbalimbali zinazotoa mikopo kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Kauli hiyo hiyo imetolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Mathias Kabundunguru wakati wa sherehe za mahafali ya 36 ya Chuo cha Ardhi Tabora.
Alisema Serikali imenunua vifaa mbalimbali vya kisasa kwa ajili ya Chuo hicho ambavyo vinawawezesha wataalamu wachche kupima eneo kubwa kwa muda mfupi na kwa gharama nafuu ukilinganisha ambavyo wangetumia Kampuni binafsi.

Kabundunguru alisema hakuna sababu ya maeneo mbalimbali katika Halmashauri za Mkoa wa Tabora na mikoa jirani kuendelea kujengeka bila mpangilio wakati Chuo kipo karibu. Alisema upimaji wa maeneo ya mijini na vijiji Mkoani humo utasaidia kuwaondoa wananchi kuishi katika maisha magumu na hatarishi kutokana na maeneo yao kutokuwa katika mpangilio.

Naibu Katibu Mkuu huyo alisema hatua hiyo inatokana na ujenzi wa makazi yasiyozingatia mipango miji na matumizi bora ya ardhi na hivyo kuwa na makazi yaliyojengwa kiholela. “Hakuna sababu ya kuwa na nyumba zilizojengwa kiholela mkoani Tabora wakati Chuo cha Ardhi kipo hapa na kina vifaa vya kisasa ambavyo vinarahisisha kazi katika upimaji” alisema

Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo ameutahadharisha uongozi wa Chuo cha Ardhi Tabora kutodiriki kukodisha vifaa hivyo katika Kampuni binafsi za upimaji ardhi kwa kuwa vifaa hivyo ni kwa jili ya matumizi ya Chuo tu. Naye Mkuu wa Chuo cha Ardhi Tabora Biseko Musiba alisema jumla ya wahitimu 536 walihitimu fani mbalimbali kwenye mahafali ya 36 mwaka huu.

Alisema miongoni wao wapo wa Stashahada ya Sanaa, Ubunifu na Uchapishaji, Astashahada ya Awali ya Urasimu Ramani, Astashahada ya Urasimu Ramani, Stashahada ya Urasimu Ramani,  Astashahada ya Awali ya Usimamizi wa Ardhi, Uthamini na Usajili na Astashahada ya Usimamizi wa Ardhi, Uthamini na Usajili.
 Brass Band ya Chuo cha Ualimu Tabora ikiongoza maandamano ya Wahitimu wa Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA) kuingia katika viwanjani kwa ajili ya Mahafali ya 36 ya Chuo hicho yalifanyika jana mjini Tabora.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Mathias Kabundunguru (aliyeweka mkono kifuani) akishiriki kuimba wimbo wa Taifa wakati wa sherehe za mahafali ya 36 ya Chuo cha Ardhi Tabora zilizofanyika jana.
 Mkuu wa Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA) Biseko Musiba(aliyesimama) akitambulisha wageni mbalimbali wakati wa mahafali ya 36 ya Chuo hicho yaliyofanyika jana mjini Tabora.
 Baadhi ya wahitimu wa Chuo cha Ardhi Tabora(ARITA) wakimsikiliza Mgeni rasmi wakati wa mahafali ya 36 ya Chuo hicho yalifanyika jana.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Ardhi Tabora(ARITA) Profesa Gabriel Kassenga akitoa salamu za Bodi wakati mahafali ya 36 ya  ARITA yaliyofanyika jana.
  Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Mathias Kabundunguru akiwahutubia wahitimu wa mahafali ya 36 ya Chuo cha Ardhi Tabora jana.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Mathias Kabundunguru (mwenye Joho la bluu waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali na wakufunzi wa Chuo cha Ardhi Tabora jana mara baada ya kumalizika kwa mahafali ya 36 Chuo cha Ardhi Tabora yaliyofanyika jana. Picha na Tiganya Vincent

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad