HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, December 4, 2018

OFISI YA RAIS-UTUMISHI YAWATAKA WAAJIRI NCHINI KUWAPATIA HUDUMA STAHIKI WATUMISHI WA UMMA WENYE ULEMAVU

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imetoa wito kwa waajiri nchini, kuwapatia huduma stahiki watumishi wa umma wenye ulemavu kwa mujibu wa Mwongozo wa Huduma kwa Watumishi wa Umma wenye Ulemavu wa mwaka 2008 kwa lengo la kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Dorothy Mwaluko wakati wa kikao kazi  cha Watumishi wa Ofisi ya Rais, Utumishi cha kuadhimisha Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi hiyo jijini Dodoma.
Bi. Mwaluko amesema, walemavu kama walivyo binadamu wengine, wana wajibu wa kutoa mchango katika maendeleo ya taifa, hivyo ni wajibu wa waajiri wote nchini kuwapatia huduma zinazostahili ili waweze kutimiza wajibu wao.
Bi. Mwaluko amefafanua kuwa, watumishi wa umma wenye ulemavu hawana tofauti na watumishi wengine isipokuwa wana mahitaji yao ya msingi ambayo usipowapatia yanakwamisha utendaji kazi wao, hivyo waajiri hawana budi kuzingatia mahitaji ya kundi hilo ambalo baadhi ya waajiri hulisahau.
Kwa upande wake, Mratibu wa Dawati la Watumishi wenye Ulemavu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Elibariki Funga Kahungya amesema, Ofisi kama msimamizi wa Mwongozo wa Huduma kwa Watumishi wa Umma wenye Ulemavu wa mwaka 2008, inawawezesha watumishi sita waliopo wenye ulemavu kupata huduma muhimu kama mwongozo unavyoelekeza ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Bw. Kahungya amezitaja huduma zinazotolewa kuwa ni pamoja na chombo cha usafiri (bajaji), mafuta ya vyombo vya usafiri kila wiki, vifaa vya kuwezesha kusikia, mafuta ya ngozi na posho ya lishe na dawa kwa mtumishi mwenye ulemavu usioonekana.
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imeungana na wadau wengine duniani kuadhimisha Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Desemba 03 ya kila mwaka. Kauli Mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Niwawezeshe  Wenye Ulemavu na Kuwajumuisha kwa Usawa”.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Dorothy Mwaluko akifungua kikao kazi  cha Watumishi wa Ofisi ya Rais, Utumishi cha kuadhimisha Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi hiyo jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Dorothy Mwaluko akimkabidhi Mkurugenzi wa Sera, Ofisi ya Rais, Utumishi, Bi Agnes Meena, Mwongozo wa Huduma kwa Watumishi wa Umma wenye Ulemavu wa mwaka 2008  ili aweze kufanya ufuatiliaji na usimamizi wa mwongozo huo katika taasisi za umma nchini.
Afisa Tawala Mkuu, Ofisi ya Rais, Utumishi,  Bi. Mwanaamani Mtoo akiwasilisha mada kuhusu ujumuishwaji wa masuala ya watu wenye ulemavu katika utumishi wa umma wakati wa kikao kazi  cha Watumishi wa Ofisi ya Rais, Utumishi cha kuadhimisha Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi hiyo jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Dorothy Mwaluko akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Ofisi ya Rais, Utumishi baada ya kufunga kikao kazi cha kuadhimisha Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi hiyo jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad