HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, December 1, 2018

MRADI WA MAJITAKA MWANZA WAIBUKA KINARA

Mradi wa Majitaka unaotekelezwa kwenye maeneo ya miinuko Jijini Mwanza unaofahamika kama "Simplified Sewerage" umekuwa miongoni mwa miradi miwili bora zaidi kuwahi kutekelezwa Barani Afrika chini ya ufadhili wa African Infrastructure Trust Fund (EU-AITF). Hayo yameelezwa mwishoni mwa Mwezi Novemba, 2018 wakati wa Mkutano wa kujadili miradi inayofadhiliwa na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) kupitia mfuko huo wa EU-AITF.

Katika mkutano huo ilielezwa kwamba tangu mfuko huo uanzishwe mnamo mwaka 2007 ni miradi miwili pekee ambayo imefuzu na kuwa miradi bora zaidi kuwahi kutekelezwa ambayo ni Mradi wa Majitaka wa Simplified Sewerage wa Jijini Mwanza, nchini Tanzania na mwingine ni mradi wa Nishati ya Umeme wa Benin & Togo.

Akizungumzia mradi wa Majitaka wa Jijini Mwanza, Mshauri wa masuala ya Kiufundi wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya, Raoul Pedrazzani alielezea hali ilivyokuwa hapo awali kabla ya kujengwa kwa mradi mpya wa majitaka kwenye maeneo ya milimani jijini humo. Pedrazzani alisema kuwa kijiografia maeneo mengi ya Jiji la Mwanza ni milima/miinuko na kabla ya mradi huo wa majitaka wakaazi wa maeneo ya milimani hawakuwa na mfumo mzuri wa uondoaji wa majitaka hali ambayo iliwasababishia adha mbalimbali ikiwemo uchafuzi wa mazingira na maradhi.

Alisema suluhisho ilikuwa ni kubuni mradi ambao utarahisisha utoaji wa majitaka kutoka kwenye makazi hayo kwenda yanakostahili. Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Anthony Sanga alithibitisha kupokea ujumbe wa pongezi juu ya ushindi huo.

Mhandisi Sanga aliipongeza Bodi ya Wakurugenzi ya MWAUWASA kwa usimamizi mahiri wa shughuli zinazotekelezwa na Mamlaka na pia aliwapongeza watumishi wote wa MWAUWASA kwa utekelezaji na usimamizi mzuri wa miradi husika. “Mungu ni Mwema, tunamuomba Aendelee kutusaidia. Hakika kwa pamoja tunaweza,” alisema Mhandisi Sanga.

Aliongeza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha huduma ya majitaka inapanuka zaidi ili wananchi walio wengi waweze kufikiwa. Maeneo ya miinuko ambayo tayari yamefikiwa na mfumo huo wa Simplified Sewerage ni Kilimahewa, Mabatini na Igogo na huku lengo likiwa ni kupanua wigo na kufikia maeneo mengi zaidi.
 Waziri wa Maji Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) akikagua ubunifu uliotumika katika ujenzi wa mradi wa majitaka, Mabatini mtaa wa Unguja wilaya ya Nyamagana. Mradi huo umejengwa kwenye maeneo ya miinuko na umesaidia kuondosha uchavuzi wa mazingira na magonjwa ikiwamo Kipindupindu.
 Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Anthony Sanga (mbele) akiwaongoza wajumbe wa Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Maji Mjini Moshi (MUWSA) eneo la Mabatini Jijini Mwanza walipotembelea kujifunza mfumo wa majitaka Oktoba, 2018. Ni mradi wa kipekee kuwahi kutekelezwa nchini.
 Moja ya eneo lililonufaika na mfumo wa majitaka ujulikanao kama ‘Simplified Sewerage’. Pichani ni Mtaa wa Unguja, Kata ya Mabatini Jijini Mwanza ambao ni miongoni mwa maeneo yaliyonufaika na mradi wa majitaka wa simplified sewerage kupitia ufadhili wa African Infrastructure Trust Fund (EU-AITF).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad