HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, December 13, 2018

DK. MABODI AKABIDHI TREKTA KIJIJI CHA BUMBWISUDI

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za Pembejeo za kilimo katika maeneo mbali mbali nchini. Hayo ameyasema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla 'Mabodi katika hafla ya kukabidhi Trekta moja lililonunuliwa na Mwakilishi wa Jimbo hilo Machano Othman Said kwa ajili ya wakulima wa kijiji cha Bumbwisudi kilichopo Wilaya Magharibi "A' Unguja.

Dk.Mabodi ameeleza kuwa hatua hiyo ya kuwapatia Pembejeo za kilimo wakulima zitarahisisha shughuli za kilimo, kwani mazao yatapandwa kwa muda mwafaka na kupatikana mavuno mengi. Kupitia hafla hiyo Dk.Mabodi amewapongeza Mbunge wa Jimbo la Mfenesini Mhe.Mhe.Col.Mstaafu Masoud Khamis pamoja na Mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe. Machano Othman Said kwa utendaji wao mzuri wa kutatua kwa wakati changamoto zinazowakabili wananchi.

Aliwambia Viongozi wa Majimbo mengine kuiga utendaji huo wa viongozi wa Jimbo la Mfenesini kwani wameendelea kutekeleza kwa ufanisi Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020, kwa nia ya kutimiza ahadi walizotoa kwa wapiga kura wao katika Uchaguzi Mkuu uliopita. Aidha aliwataka wananchi wa vijiji mbali mbali vilivyomo katika Jimbo hilo na Majimbo jirani walitumie vizuri Trekta hilo ili lidumu kwa muda mrefu na kulima mashamba mengi ya wakulima.

Katika maelezo yake Dk.Mabodi alitangaza neema kwa wananchi hao kuwa CCM imejipanga kutoa Matrekta Matano kwa wakulima wa Unguja na Pemba, kwa lengo la kuwaondoshea changamoto za upungufu wa Pembejeo za kisasa za kilimo. Pia aliwambia kuwa yupo katika hatua  za mazungumzo na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar  waharakishe upatikanaji wa mbolea.

Dk.Mabodi alilaani vikali kitendo cha baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Kitundu kususia kuswalia maiti ya kada wa CCM msikitini jambo ambalo halikubaliki katika misingi ya maadili ya Dini zote pamoja na Sheria za nchi. Aliwataka wananchi kuacha tabia za kuchanganya siasa za visasi na dini kwani suala hilo ni hatari kwa ustawi wa maendeleo ya nchi na kijamii, na inaweza kuingiza nchi katika migogoro.

Katika hatua nyingine Naibu alisema viongozi wa CCM ndio waliotembea nyumba kwa nyumba kuomba kura kwa wananchi na wakaahidi kutekeleza mambo mengikupitia ilani ya uchaguzi ya CCM,inayotakiwa kutekelezwa kwa ufanisi. Pamoja na hayo alituma salamu nzito kwa baadhi ya makada na viongozi wandamizi wa CCM ambao bado wanaendelea na mienendo isiyofaa kwa mujibu wa maadili ya CCM kuwa wasipojirekebisha na kurudi katika mstari watafyekelewa mbali.

Akizungumzia namna eneo la Bumbwisudi linavyowasaidia kwa kushughuli za kilimo wananchi wa maeneo mbali mbali aliongeza kuwa jumla ya Wakulima 234 wanatoka bububu na kwenda kulima katika mabonde ya Bumbwisudi kutokana na ardhi ya eneo hilo kuwa na rutuba. Kupitia hafla hiyo alisema maendeleo yaliyofikiwa yametokana na juhudi kubwa za Waasisi wa Mapinduzi ambao walifanya mambo mema na kwa sasa yamekuwa ni kichocheo kikubwa cha maendeleo katika nyanja mbali mbali za kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Aliwasihi wananchi hao kuthamini juhudi za viongozi wa CCM wanaokesha wakibuni miradi endelevu ya kuwakwamua kiuchumi.  Sambamba na hayo Dk.Mabodi aliweka wazi kuwa siri ya mafanikio ya CCM ni kujishusha kwa wananchi kwa kutatua changamoto zinazowakabili pamoja na kubuni mipango endelevu ya kuibua fursa za kuwakwamua wananchi kiuchumi. "CCM ipo imara na itaendelea kuwa imara kwani ndio chama pekee chenye Sera na miongozo ya kikatiba iliyotaja kwa uwazi njia na misingi ya kushughulikia kero za wananchi na kujali utu,haki na ustawi wa kijamii", alisema Dk.Mabodi.

Akizungumza katika hafla hiyo Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini Mhe. Machano Othman Said alisema viongozi wa jimbo hilo ambao ni Mbunge,Mwakilishi na madiwani wametekeleza miradi ya maendeleo kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata fursa kujiajiri wenyewe.  Alisema mbali na miradi katika sekta ya kilimo pia kwa sasa wanajipanga kuanza ujenzi wa soko la kisasa pamoja na kituo cha daladala katika eneo la Kwanyanya ili wananchi wa maeneo hayo waondokane na usumbufu wa kutopatikana kwa baadhi ya huduma za kijamii.

Alisema ushirikiano wake na viongozi wengine wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali ndio chanzo cha kufanikisha mipango ya maendeleo ndani ya jimbo hilo. Naye Mbunge wa Jimbo hilo Col. mstaafu Masoud Khamis alikemea tabia za fitna majungu zinazofanywa na baadhi ya makada wenye ajenda binafsi za kuwagombanisha viongozi wa Jimbo hilo. Col. mstaafu huyo alisema kuwa kuwa hakuna mtu yeyote atakayezuia kasi utekelezaji wa Ilani ndani ya Jimbo hilo kwani mambo yote yanayotekelezwa ni kwa ajili ya chama cha Mapinduzi.
 BAADHI ya Wana CCM na wananchi waliohudhuria katika hafla ya kukabidhi Trekta moja lililonunuliwa na Mwakilishi wa Jimbo hilo Machano Othman Said kwa ajili ya wakulima wa kijiji cha Bumbwisudi kilichopo Wilaya Magharibi "A' Unguja.
 MBUNGE wa Jimbo la Mfenesini Col.mstaafu Masoud Khamis akizungumza na wana CCM pamoja na wananchi kwa ujumla hafla ya kukabidhi Trekta moja lililonunuliwa na Mwakilishi wa Jimbo hilo Machano Othman Said kwa ajili ya wakulima wa kijiji cha Bumbwisudi kilichopo Wilaya Magharibi "A' Unguja.
 MWAKILISHI wa Jimbo la Mfenesini Mhe.Machano Othman Said akizungumzia maendeleo yaliyopatikana katika Jimbo hilo hafla ya kukabidhi Trekta moja lililonunuliwa na Mwakilishi wa Jimbo hilo Machano Othman Said kwa ajili ya wakulima wa kijiji cha Bumbwisudi kilichopo Wilaya Magharibi "A' Unguja.
 MWENYEKITI wa Mkoa Mjini Magharibi Talib Ali Talib akizungumza katika hafla ya kukabidhi Trekta moja lililonunuliwa na Mwakilishi wa Jimbo hilo Machano Othman Said kwa ajili ya wakulima wa kijiji cha Bumbwisudi kilichopo Wilaya Magharibi "A' Unguja.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi akizungumza na wananchi mbali mbali waliohudhuria katika mkutano hafla ya kukabidhi Trekta moja lililonunuliwa na Mwakilishi wa Jimbo hilo Machano Othman Said kwa ajili ya wakulima wa kijiji cha Bumbwisudi kilichopo Wilaya Magharibi "A' Unguja.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad