HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, December 5, 2018

BORA TUKAWIE LAKINI TUJIRIDHISHE NA MIKATABA – WAZIRI KALEMANI

Na Veronica Simba – Mtwara
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amesema Serikali itatumia muda mwingi kadri itakavyoona inafaa ili kujiridhisha na manufaa ambayo Taifa litapata kabla ya kusaini mikataba mbalimbali ya sekta ya nishati, hususan ya mafuta na gesi. Aliyasema hayo Mtwara jana, Desemba 4 wakati akizungumza na uongozi wa Kampuni ya kigeni ya mwekezaji Maurel & Prom kutoka Ufaransa, wanaotafiti na kuchimba gesi eneo la Mnazi Bay.

Waziri Kalemani alitoa msimamo huo wa Serikali baada ya kupokea taarifa ya utendaji kazi wa kampuni hiyo iliyowasilishwa na Makamu Mkurugenzi Mkuu, Elias Kilembe, ambayo pamoja na mambo mengine, waliomba Serikali iharakishe mchakato wa utiaji saini mikataba ya uwekezaji zaidi katika sekta husika, ambayo walikwisha kuwasilisha. Akifafanua, Waziri Kalemani alisema, Serikali haikusudii kumchelewesha mwekezaji bali kinachofanyika ni kujiridhisha hatua kwa hatua, namna Taifa litakavyonufaika.

“Tutatumia muda wa kutosha kujiridhisha, hata kama ni miaka 40, lakini lazima mikataba iwe na manufaa. Huo ndiyo msimamo wa Serikali.” “Sisi tunapenda wawekezaji, tunataka waendelee kuwekeza ili tupate manufaa ya gesi na mafuta, lakini tusiibiwe,” alisisitiza.

Aidha, katika ziara hiyo, Waziri Kalemani aliutaka uongozi wa Kampuni husika kuchukua hatua stahiki, za makusudi na haraka katika kudhibiti changamoto ya maji ya baharí kusogea karibu zaidi na kisima cha gesi cha Mnazi Bay, hivyo kuwepo hofu ya maji hayo kuingia kwenye kisima husika.

Vilevile, Waziri alipongeza ukamilishwaji wa mfumo wa kuunganisha visima vyote vya gesi vya Mnazi Bay, hali ambayo alieleza itasaidia katika kuimarisha ukaguzi na udhibiti. “Naagiza, kuanzia sasa kila gesi inayotoka katika visima vilivyopo, ipite kwenye mfumo huu mpya ili ituwezeshe kujua ni kiasi gani imetoka na kiasi gani kilipwe.”

Akikagua Mtambo wa kuchakata gesi wa Madimba, ulio chini ya Shirika la umma la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Waziri alipongeza kazi nzuri inayofanywa na Shirika hilo na kuwataka waongeze bidii zaidi katika usimamiaji wa rasilimali hizo adhimu za mafuta na gesi kwa manufaa ya watanzania.

Katika ziara hiyo, Waziri pia alikagua utekelezaji wa miradi ya umeme iliyo chini ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika Mtaa wa Ufukoni na Mbae Mashariki, Manispaa ya Mtwara; ambapo aliwaagiza viongozi wa Shirika hilo katika maeneo hayo, kuhakikisha wananchi wote waliolipia umeme wanaunganishiwa huduma hiyo ifikapo Desemba 20 mwaka huu.

Aidha, alitoa maagizo kwa Mameneja wote wa TANESCO nchi nzima kuwa tarehe ya mwisho kuwaunganishia wananchi waliolipia umeme ni Desemba 31 mwaka huu, vinginevyo watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
 Wananchi wa Mtaa wa Ufukoni, Manispaa ya Mtwara wakishangilia mara baada ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kulia) kuwasha umeme katika nyumba ya mmoja wa wananchi wa eneo hilo pamoja na kuzungumza nao akiwa katika ziara ya kazi Desemba 4, 2018.
 Taswira ya sehemu ya mtambo wa kuchakata gesi asilia wa Madimba kama ilivyonaswa wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani Desemba 4, 2018.
 Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati-mbele) na Ujumbe wake, akikagua Mtambo wa kuchakata gesi asilia wa Madimba mkoani Mtwara, akiwa katika ziara ya kazi Desemba 4, 2018.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mwenye shati ya bluu-katikati) na Ujumbe wake, wakikagua sehemu ya mitambo ya kuchakata gesi Mnazi Bay, Mtwara alipokuwa katika ziara ya kazi, Desemba 4, 2018.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad