HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 2, 2018

NECTA YAFUTA MATOKEO YA MTIHANI WA DARASA LA SABA KWA BAADHI YA SHULE ZA MSINGI NCHINI

*Ni baada ya kubaini kufanya udanganyifu, yatangaza kurudiwa kwa mtihani

Na Ripota Wetu,Globu ya jamii
HATIMAYE Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) limetangaza kuyafuta matokeo ya mitihani ya darasa la saba kwa shule za msingi zote zilizopo ndani ya Halmashauri ya Chemba mkoani Dodoma,  pamoja na baadhi ya shule zilizopo katika halmashauri ya Ubungo, Kinondoni,Kondoa na Mwanza.

Kwa mujibu wa Necta imeamua kufuta matokeo ya shule hizo baada ya kubaini kuvuja kwa mtihani huo katika shule hizo na kwamba hilo ni jambo ambalo ni kinyume na sheria na kanuni za mitihani nchini kwetu.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Taifa (NECTA) Charles Msonde ametangaza uamuzi huo leo jijini Dar es Salaam ambapo amesema wamefikia uamuzi huo baada ya kuvunjwa kwa kanuni za mitihani baraza hilo limeamua kufuta matokeo ya mtihani huo wa kumaliza elimu ya msingi katika shule  za msingi za halmashauri hizo.

"Hivyo watahiniwa wote watarudia tena mtihani huo Oktoba 8 na 9 mwaka huu kwa halmashauri zote ambazo halmashauri zao uchaguzi umefutwa baada ya kubaini umevuja," amesema Dk.Msonde.

Ametaja shule ambazo zimefutiwa matokeo ya mtihani imo Shule ya Msingi Hazina na New Hazina zilizopo Magomeni wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Pia Shule ya Aniny Nndumi na Fountain of Joy zilizopo Ubungo, Shule ya Msingi Kondoa Integrity  iliyopo Halmashauri ya Kondoa, pamoja na Shule ya Msingi Kisiwani,  Alliance na New Alliance zilizopo Mwanza.

Dk.Msonde amesema pia  baraza hilo limefuta vituo vya mitihani kwa shule nane ambazo zilihusika katika uvujishaji wa mitihani hiyo sambamba na kupendekeza kuondolewa kwenye nafasi za ajira kwa baadhi ya maofisa elimu kata na wilaya waliohusika kwenye udanganyifu huo.

Amefafanua Necta wameidhinisha vituo mbadala vya mtihani vitakavyotumiwa na watahiniwa katika mtihani wa marudio utakaoufanya Ocktoba 8 na 9 wiki ijayo.

" Shule ya Msingi  Hazina na New Hazina wanafunzi wake wa darasa la saba watafanya mtihani huo katika shule ya Msingi Osterbay.

" Shule ya Fountain of Joy na Aniny Nndumi za Ubungo zitafanya mtihani katika shule ya Msingi Mbezi.Shule ya Msingi Kisiwani ya jijini Mwanza wanafunzi wake watafanya mtihani huo kwenye shule ya Msingi Kakebe.

"Shule ya Alliance na New Alliance watahiniwa watafanya mtihani katika shule ya Msingi Mahina na Shule ya Msingi ya Kondoa Integrity wanafunzi watafanya mtihani kwenye shule ya Msingi Bicha, " amefafanua.

Dk.Msonde akifafanua jinsi udanganyifu ulivyofanyika, amesema Septemba 6 mwaka huu mara baada ya mtihani wa somo la Sayansi kukamilika Ofisa wa Necta mfuatiliaji alibaini katika Shule ya Hazina uwepo wa kipande cha karatasi chenye maswali  kwenye chumba kilichokuwa karibu na kile kilichokuwa kikihifadhi mitihani.

Amesema uchunguzi ulifanywa na Kamati ya Mtihani ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na Necta ulibaini mmiliki wa Shule za Hazina kwa kushirikiana walimu wa shule hizo walitafuta mitihani na kuipata siku moja kabla ya tarehe ya kuanza mtihani na waliwaonesha wanafunzi wote wa shule hizo za Hazina.

Dk. Msonde amesema walimu wa Shule ya Hazina walibainisha kuwa walitumiwa mitihani ya masomo yote kutoka kwa walimu wa Shule ya Msingi Alliance iliyopo Mwanza lakini pia simu za walimu hao zilibainika kutumiwa mitihani ya masomo yote.

Amewataja walimu waliohusika kuvujisha mtihani huo katika shule hizo ni Mwalimu Heche Nasri,  Bahanzika  Mohamed,  Mambo Bakari,  Idd Lawrence,  Jacob Ochieng na Musa Juma, pia yupo Justus James,  Kenedy Malogo wa Shule ya Msingi Aniny Nndumi pamoja na Benson Beita na Benson Awolo  wa Shule ya Msingi Alliance.
 Ameongeza kuwa walimu wa Shule ya Alliance walipokamatwa na kuchunguzwa walikutwa na mitihani hiyo kwenye simu zao na walibainisha wazi kuwa waliupata kutoka kwa walimu wa Shule ya Anny Nndumi ya Ubungo.

Pia walimu wa Nndumi alikiri Katumiwa mitihani hiyo ambapo alibainisha na yeye alitumiwa na Mwalimu wa Shule ya Fountain of Joy ya Ubungo.

"Ukitazama  mlolongo huu utaona jinsi ambavyo cheni ilivyokuwa kubwa.Hivyo tunaendelea kufanya uchunguzi katika shule zote na kisha tutachukua hatua kwa wale ambao watakaobainika kuhusika na  udanganyifu huo.

Wakati huo huo Dk.Msonde amesema Halmashauri ya Chemba uongozi wa idara ya elimu ya Halmashauri ya Chemba walipanga kufanya udanganyifu kupitia kwa waratibu Elimu Kata, walimu wakuu na wasimamizi kwa lengo la kuinua kiwango cha ufaulu wa halmashauri hiyo.

Ameeleza kuwa wahusika walioshiriki udanganyifu huo amesema aliyehusika ni Kaimu Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Chemba  Modest Tarimo,  Ofisa Taaluma Msingi wa halamshauri hiyo,  Ally Akida, Mratibu Elimu Kata ya Farkwa Mwalimu Deo Philip, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Farkwa.

Pamoja na mambo mengine imeelezwa kuvuja kwa mitihani hiyo kumesababisha kuingiza nchi kwenye gharama nyingine ya kurudia mtihani na ni aibu kwa nchi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad