HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 13 December 2017

WADAU WA TAKWIMU WAKUTANA KUJADILI NA KUTATHMINI UTEKELEZAJI WA MALENGO YA MAENDELEO ENDELEVU NA MPANGO WA PILI WA MAENDELEO WA TAIFA

Na Emmanuel Ghula
WADAU wa Takwimu nchini wamekutana ili kujadili upatikanaji wa Takwimu za msingi na uzalishaji wa takwimu na mapungufu yaliyopo katika kupima na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.

Akizungumza wakati akifungua warsha ya siku mbili ya wadau hao, Naibu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango, Wizara ya Fedha na Mipango Mhandisi Happiness Mgalula amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Maendeleo pamoja na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)  wameandaa warsha hiyo ili kujadili namna bora ya upatikanaji wa takwimu zitakazosaidia kufanikisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

“Leo tumekutana hapa kwa pamoja ili kujadili namna bora ya upatikanaji wa takwimu kwa ajili ya kupima na kutathmini utekelezaji wa viashiria vya Malengo ya Maendeleo Endelevu na Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa katika sekta ya Ukuaji Uchumi, Ajira na Ushindani wa Kiuchumi,” amesema Mhandisi Mgalula.

Amesema Serikali itaendelea kuratibu upatikanaji wa takwimu rasmi nchini kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu pamoja na wadau wengine ili kufanikisha utekelezaji wa seti za malengo ya ulimwengu katika muda maalumu na ambayo mkazo wake ni kuondoa aina zote za umaskini pamoja na njaa. 

Amesema Serikali imepiga hatua kubwa katika kuweka mikakati ya utekelezaji wa Malengo ya Mandeleo Endelevu (SDGs) tangu mwaka 2015 ikiwa ni pamoja na kufanya mikutano mikubwa miwili ya Kitaifa kwa ajili ya kuwajengea wananchi uelewa mzuri kuhusu SDGs na utekelezaji wake. 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Irenius Ruyobya amesema NBS itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhak  takwimu rasmi zinapatikana kwa wakati ili ziweze kutumika na Serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo katika kupanga na kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Aidha, Ruyobya amesema washiriki watajadili namna bora zaidi ambayo wadau wanaweza kushiriki katika kuchangia mapungufu ya upatikanaji na uzalishaji wa takwimu pamoja na ubunifu na ujuzi wa teknologia katika uzalishaji na upatikanaji wa takwimu.
 Naibu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango, Wizara ya Fedha na Mipango Mhandisi Happiness Mgalula akizungumza wakati akifungua warsha ya siku mbili ya wadau wa takwimu waliokutana kuanzia leo jijini Dr es Salaam katika ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere.
 Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Irenius Ruyobya akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari wakati wa hafla ya ufunguzi wa warsha ya siku mbili ya wadau wa takwimu waliokutana leo jijini Dr es Salaam katika ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere.
Baadhi ya wadau wa takwimu waliokutana leo jijini Dar es Salaam katika warsha ya siku mbili ili kujadili namna bora ya upatikanaji wa takwimu kwa ajili ya kupima na kutathmini utekelezaji wa viashiria vya Malengo ya Maendeleo Endelevu na Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad