HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 20 December 2017

TMRC YAWEZESHA UPASUAJI WA MOYO KWA WATOTO WANNE

 Kampuni ya Tanzania Mortgage Refinance Limited (TMRC), imetoa msaada wa kiasi cha Shilingi milioni Nane (Shilingi 8,000,000) kwa ajili ya upasuaji wa moyo kwa watoto wanne jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi mfano wa hundi hiyo ya Shilingi milioni Nane kwa Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (JKCI), Profesa Mohamed Janabi, Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa TMRC, Oscar Mgaya, alisema kuwa wameamua Kuitikia wito huu wa kuwasaidia watoto hao ambao hawana uwezo na bila msaada huo pengine wasingeweza kupata huduma hiyo na maisha yao yangekua hatarini.
"Tumeamua kusaidia tiba kwa hawa watoto baada ya kuona tangazo kwenye kituo cha televisheni cha Clouds. Hivyo basi, tukaona umuhimu wa kufanikisha malipo kwa ajili ya upasuaji wa watoto hawa wanne," Bw. Mgaya alisema.
Aidha, Mtendaji Mkuu huyo, alisema taasisi yake hiyo ambayo inatoa mikopo ya ujenzi au ununuzi wa nyumba kupitia mabenki na taasisi nyingine za fedha kuwa, waliamua kutoa kiasi cha Shilingi milioni mbili (Shilingi 2,000,000) kwa upasuaji wa kila mtoto kwa kuwa ni taifa la kesho.  Hii ni sehemu ya kutekeleza wajibu wetu katika jamii (corporate social responsibility).   
"Tumeamua kutoa kiasi kidogo  kwa watoto hawa wadogo ambao miongoni mwao wana ndoto za kuwa wataalamu wa benki, madaktari, marubani n.k. Hivyo, taasisi yetu imeona umuhimu wa kufanya ndoto za hawa watoto kutimia kwa kuwawezesha kupata tiba," alisema.
Bw. Mgaya ametoa rai kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia wenye uhitaji wa tiba hii ya moyo hasa kwa wale wenye maisha duni ambapo uhitaji unaelezewa kuwa ni mkubwa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (JKCI), Profesa Mohamed Janabi, alisema kwamba taasis yake imejipanga kuhakikisha kuwa inaendelea kupunguza idadi ya wagonjwa wanaoenda kutibiwa nje ya nchi, kutokana na magonjwa ya moyo na badala yake kutibiwa nchini kwa gharama nafuu.
"Licha ya kuwasaidia watanzania kupunguza gharama kwa matibabu ya moyo hapa nchini badala ya nje ya nchi, pia hii imepunguza sana gharama ambazo serikali imekuwa ikizitumia kila mwaka kutibu maradhi kama hayo nje ya nchi," Prof Janabi alisema.
Tangu taasisi yetu ianze kutoa tiba hii mwaka 2008, tumeweza kupunguza kwa kiwango kikubwa idadi ya watanzania wanaotibiwa nje ya nchi. Hata hivyo, ameishukuru TMRC, kwa msaada wa fedha kwa ajili ya tiba kwa watoto hao wanne na kuziomba taasisi nyingine kuiga mfano.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad