HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 4, 2017

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI, JAPHET HASUNGA ATOA MIEZI MITATU WANANCHI WALIPWE FIDIA WAPISHE ENEO LA HIFADHI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kushoto) akizungumza na watumishi wa Pori la Akiba Mpanga Kipengele alipotembelea makao makuu ya pori hilo jana katika Wilaya ya Wangin'ombe mkoani Njombe. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, David Kanyata na Kaimu Meneja wa pori hilo, Stanslaus Odhiambo.

Na Hamza Temba, Mbarali - Mbeya
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ametoa miezi mitatu kwa uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA kukamilisha malipo ya fidia ya shilingi milioni 771.6 kwa kaya 308 za Kitongoji cha Machimbo ili ziweze kupisha eneo la hifadhi katika Pori la Akiba la Mpanga Kipengele.

Naibu Waziri Hasunga ametoa agizo hilo jana katika mkutano wa hadhara baada kutembelea kitongoji hicho katika Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya wakati wa ziara yake ya kikazi kwa ajili ya kutatua migogoro kwenye maeneo ya hifadhi mkoani humo.

“Kaimu Mkurugenzi (TAWA) kama unavyoona wananchi hawa wapo tayari kupisha eneo hili la hifadhi, wanachosubiri ni malipo yao ya fidia, naagiza mpaka ifikapo mwezi Februari mwakani (2018) wawe wameshalipwa fidia zao, na ikiwezekana hata ndani ya mwezi Januari wawe wameshalipwa,”alisema Hasunga.

Awali akiwasilisha taarifa ya pori hilo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, David Kenyata alisema wakati pori hilo linaanzishwa mwaka 2002 kwa Tangazo la Serikali Na. 483 wananchi wa kitongoji hicho na vitongoji vingine walikuwa ndani ya eneo hilo la hifadhi.

Alisema mazungumzo yalishafanywa kupitia vikao halali vya uongozi wa viijiji na halmashauri ambapo wananchi hao waliridhia kulipwa fidia ili kuachia maeneo hayo ya hifadhi.

Alisema sababu kubwa ya kuanzishwa kwa pori hilo ni pamoja na kuhifadhi vyanzo vya maji yanayotiririka kwenda mto Ruaha na kwenye mabwawa ya kidatu na mtera yanayotumika kuzalisha umeme nchini.

Akizungumzia malipo ya fidia kwa vijiji na vitongoji vilivyopo ndani ya hifadhi hiyo alisema kijiji kimoja kilishalipwa mwaka 2015 jumla ya shlingi milioni 500 na vijiji vilivyosalia vitalipwa kwa awamu ambapo kwa mwaka wa fedha 2017/2018 fedha zimetengwa kwa ajilia ya kulipa wananchi wa kitongaoji cha Machimbo ambao tayari walishafanyiwa uthamini mwaka 2015.

Awali akizungumza na watumishi wa Pori hilo katika ofisi zao zilizopo Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe, Naibu Waziri Hasunga aliwataka watumishi hao kuongeza nguvu na ubunifu kwenye kuzuia mifugo isiiingie hifadhini badala ya kusubiri iingie ndipo waikamate na kuitoza faini au kuitaifisha.

“Nyie ni watalaamu, tumieni mbinu na ubunifu wenu wote muhakikishe mnazuia mifugo isiingie hifadhini, sitaki kusikia mmekamata au mmetaifisha mifugo hifadhini, hiyo siyo sifa, sifa ni kuzuia isiingie kabisa, na nitawapima kwa hilo,” alisema Hasunga.

Aidha aliwataka watumishi hao kuimarisha uhifadhi shirikishi, kujiepusha na vitendo vya rushwa, kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kuongeza ubunifu utakaowezesha ongezeko la mapato ya Serikali.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo aliwatembelea wananchi wanaojishughulisha na kilimo cha umwagiliaji katika Skimu ya Igomelo ambao awali waligomea zoezi la uwekwaji wa vigingi vya mpaka kwenye eneo lao na Pori la Akiba la Mpanga Kipengele kwa hofu ya kupoteza maeneo hayo.

Hata hivyo baada ya kuwaelimisha kuwa lengo la zoezi hilo ni kuiwezesha Serikali kufanya uamuzi wa mwisho wa kumaliza migogoro ya ardhi iliyodumu kwa muda mrefu baina ya vijiji na maeneo ya hifadhi nchini wananchi hao walielewa na kuahidi kushirikiana na mamlaka husika kukamilisha zoezi hilo kwa muda uliopangwa.  

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Pori hilo, Stanslaus Odhiambo alisema pori hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uwepo wa vijiji na vitongoji 13 ndani ya pori hilo, uchomaji moto maeneo ya hifadhi, ukataji miti hovyo, ujangili na uhaba wa vitendea kazi.

Pori la Akiba la Mpanga Kipengele lina ukubwa wa Kilometa za mraba 1574.25 katika wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya na Wilaya za Wanging’ombe na Makete Mkoani Njombe.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (waliokaa mbele katikati) akizungumza na watumishi wa Pori la Akiba Mpanga Kipengele alipotembelea makao makuu ya pori hilo jana katika Wilaya ya Wangin'ombe mkoani Njombe.
Baadhi ya watumishi wa Pori la Akiba Mpanga Kipengele wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (hayuko pichani).
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (wa pili kushoto) akisalimiana na Kaimu Meneja wa Pori la Akiba la Mpanga Kipengele, Stanslaus Odhiambo muda mfupi baada ya kuwasili makao makuu ya pori hilo jana katika Wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Machimbo wapatao kaya 308 katika Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya jana ambapo aliiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania kuwalipa fidia ya shilingi milioni 771.6  kabla ya Februari, 2018 ili wapishe eneo la Hifadhi katika Pori la Akiba la Mpanga Kipengele.
Baadhi ya wananchi wa kitongoji cha Machimbo wapatao kaya 308 katika Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ambaye aliwatembelea jana na kuagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania iwalipe fidia ya shilingi milioni 771.6 kabla ya Februari, 2018 ili wapishe eneo la Hifadhi katika Pori la Akiba la Mpanga Kipengele alipowatembelea.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kulia) akizungumza na wananchi wanaojishughulisha na kilimo cha umwagiliaji katika Skimu ya Igomelo, wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya ambao waligomea zoezi la uwekwaji wa vigingi vya mpaka kwenye eneo lao na Pori la Akiba la Mpanga Kipengele kwa hofu ya kupoteza maeneo hayo. Baada ya kuwaelimisha wananchi hao walikubali kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika ili kukamilisha zoezi hilo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad